Siku moja baada ya kuwasilisha maelezo yake ya utetezi baada ya
kuvuliwa nyadhifa zake ndani ya Chadema, aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa
chama hicho, Zitto Kabwe amekata rufaa Baraza Kuu kupinga hatua hiyo.
Zitto pamoja na aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema
Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba na Mjumbe wa Kamati Kuu, Dk Kitila
Mkumbo walivuliwa nyadhifa zao na Kikao cha Kamati Kuu kilichofanyika
Novemba 20 na 21 jijini Dar es Salaam.
Akizungumza jana, Mwanasheria wa Zitto, Albert
Msando alitaja sababu mbili za kukata rufaa kuwa ni kukiukwa kwa
taratibu za kuchukua hatua za nidhamu na sababu zilizotolewa kutokuwa
sahihi.
Hata hivyo, Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa
Chadema, John Mnyika alisema mambo hayo yalishatolewa ufafanuzi na chama
na kwamba kukata rufaa ni haki ya kikatiba kwa mwanachama yeyote.
“Kukata rufaa ni haki ya kikatiba ya wanachama
yeyote. Rufaa ikatwe tu, itashughulikiwa kwa mujibu wa katiba, kanuni,
maadili na itifaki ya chama. Hata hivyo, ieleweke, rufani inahusu
kuvuliwa nafasi za uongozi, kusudio hilo haliwaondolei wajibu wa
kujieleza kwa maandishi mbele ya Kamati Kuu kwa nini wasifukuzwe
uanachama,” alisema Mnyika.
Sababu za kukata rufaa
Akifafanua sababu za kukata rufaa, Msando alitaja
kifungu cha 6.5.6 cha Kanuni ya Uendeshaji ya chama hicho, akisema
utaratibu uliotakiwa kufuatwa kabla ya kumchukulia hatua za kinidhamu
kiongozi kwa mujibu wa Katiba na Kanuni ni kupewa kwanza mashtaka kwa
maandishi ili apate nafasi ya kujibu.
“Kiongozi yeyote hatachukuliwa hatua za kinidhamu
bila kwanza kupewa mashtaka yake kwa maandishi na mamlaka husika na
kupewa nafasi ya kujibu mashtaka kwa maandishi,” alisema na kuongeza:
“Kwa mujibu wa ibara ya 5.4.3 na 5.4.4 ya Katiba
mwanachama yeyote hatachukuliwa hatua za kinidhamu ama kuonywa ama
kuachishwa ama kufukuzwa uanachama bila kujulishwa makosa yake kwa
maandishi na kutakiwa kutoa majibu katika muda usiopungua wiki mbili.”
Alitaja vipengele vingine ni kupewa nafasi ya
kujitetea mbele ya kikao kinachohusika na atajulishwa kwa maandishi
uamuzi wa kikao ndani ya wiki mbili baada ya kusikilizwa.
Hata hivyo, kipengele ‘d’ kinasema: “Kamati Kuu
inaweza kuchukua hatua za dharura bila kuzingatia utaratibu (b), (c)
hapo juu kama itaona masilahi ya chama kwa ujumla yanaweza kuathiriwa
isipokuwa mwanachama au kiongozi anayelalamikiwa atalazimika kuitwa
kwenye kikao husika.
Alifafanua kuwa, siku ya kikao cha Kamati Kuu,
Zitto hakupewa mashtaka yake bali aliyakuta ndani ya kikao baada ya
kupewa taarifa kwa ujumbe wa simu (text message au sms). Zitto hakuwepo
katika mkutano wa jana na waandishi wa habari.
Mwananchi
Mwananchi
No comments:
Post a Comment