Wednesday, February 08, 2017

MNYAA ATIMULIWA UANACHAMA WA CUF

Chama cha Wananchi (CUF) kimemtimua uanachama Mohamed Habibu Mnyaa, huku mwenyewe akidai bado ni mwanachama halali.

Mnyaa amefukuzwa na mkutano mkuu wa tawi la Chanjaani, Jimbo la Mkoani kisiwani Pemba, uliohudhuriwa na wajumbe 112 kati ya 113.

Taarifa iliyotolewa na Katibu wa tawi la Chanjaani, Kombo Mohamed Maalim, ilisema Mnyaa alifukuzwa kutokana na kukiuka katiba ya chama hicho Ibara ya 12 (6)(7)(16).

Alisema miongoni mwa mambo aliyofanya ni kuwa na mwenendo usiofaa wa kuwagawa wanachama, kueneza taarifa za upotoshaji dhidi ya viongozi na chama, kufanya vitendo vya hujuma za kutaka kukidhoofisha chama, kudharau na kushindwa kuhudhuria na kutoa ushirikiano kwa tawi lake kila alipotakiwa kufanya hivyo.

Akizungumzia hatua hiyo, Mnyaa ambaye amewahi kuwa mbunge wa Mkanyageni kwa vipindi viwili mwaka 2005-2015 alisema hukumu ya kufukuzwa kwake imechukuliwa katika tawi ambalo siyo lake, kwa kuwa alishalihama tangu mwaka jana.

WAFANYABIASHARA WA POMBE ZA KIENYEJI WATAKIWA KUWA NA LESENI

Wafanyabiashara wa Pombe za Kienyeji wanatakiwa kuwa na leseni ya kufanya biashara hiyo ambayo hutolewa na Halmashauri.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Selemani Jafo ameyasema hayo, Mjini Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum (CCM) Najma Giga juu ya Serikali imejipangaje kukabiliana na tatizo la ulevi wa kupita kiasi kwa pombe za kienyeji pamoja na sheria ya vileo ya mwaka 1969 kuwa ya zamani hivyo kutokidhi mabadiliko ya hali halisi ya vileo.

“Pombe za kienyeji zimeanishwa katika kifungu cha 2 cha tafsiri katika Sheria ya Vileo, Sura ya 77 ambapo kwa mujibu wa sheria hiyo, wafanyabiashara wote wanatakiwa kuwa na leseni ambayo inatolewa na Halmashauri,” alifafanua Jafo.

MBUNGE WA CCM AHOJI 'UTAJIRI' WA MAKONDA BUNGENI

Mbunge wa Geita Vijijini (CCM), Joseph Kasheku ameendeleza ‘vita’ yake dhidi ya Paul Makonda, akisema yupo tayari kusaidia vyombo vya dola kukamata vigogo wa dawa za kulevya na kuhoji ukimya wa mawaziri watatu dhidi ya kile alichodai utajiri wa mkuu huyo wa Mkoa wa Dar es Salaam.

Awali, Kasheku ambaye ni maarufu kwa jina la Msukuma, alitoa tuhuma dhidi ya Makonda juzi, alipotaka kujua wafadhili wa safari za mkuu huyo wa mkoa nje ya nchi na sababu za kubagua watuhumiwa wa biashara ya dawa za kulevya kwa kutaja baadhi na kuwaacha wengine, huku mawaziri wakisita kuchukua hatua.

Alitoa tuhuma hizo bungeni baada ya Makonda kuagiza watu 12, wakiwemo wasanii maarufu wa muziki na filamu, kuripoti Kituo Kikuu cha Polisi cha Dar es Salaam, akiwatuhumu kuhusika na utumiaji au biashara ya dawa za kulevya.

Jana, Msukuma aliibuka na hoja nzito zaidi akihoji sababu za mawaziri kutochukua hatua na pia kutaja baadhi ya mali alizopata Makonda katika kipindi kifupi alichoshika madaraka ya mkuu wa mkoa baada ya kuwa mkuu wa Wilaya ya Kinondoni pia kwa muda mfupi.

Mbunge huyo alitoa tuhuma hizo nzito muda mfupi baada ya kumalizika kwa kipindi cha maswali na majibu, wakati alipotumia kanuni ya 68 (7) kuomba mwongozo kutoka kwa Naibu Spika, Tulia Ackson.

WAANDISHI WA HABARI WAKAMATWA, WAHOJIWA NA POLISI

Waandishi wa habari wawili jana walikamatwa na kuhojiwa katika Kituo cha Polisi cha Usa River mkoani Arusha, huku aliyetoa amri ya kukamatwa kwao akizua utata.

Wakati taarifa za awali zikidai ni amri ya Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Alexander Mnyeti, yeye alikana kuhusika na agizo hilo.

Waliokamatwa ni Bahati Chume mwandishi wa kujitegemea wa gazeti la Mwananchi Mkoa wa Kilimanjaro na Dorine Alois kutoka kituo cha Sunrise Radio cha jijini Arusha.

Waandishi hao walikamatwa walipokuwa wakifuatilia habari ya mgogoro kwenye machimbo ya kokoto katika Kijiji cha Kolila mpakani mwa wilaya za Arumeru na Hai.

Mnyeti alipoulizwa alikana kutoa amri hiyo akisema yeye hana ugomvi na waandishi wa habari.

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...