Hata hivyo, huu hakika sio wakati wa
kumtafuta mchawi, kwa maana ya kutaka kujua nani hasa serikalini alitoa
amri ya kulifungia gazeti hili kwa sababu ambazo sisi tunaona hazikuwa
na chembe ya mashiko. Tulishangazwa kuona amri hiyo ya Serikali
ikitolewa wakati mkuu wa nchi, Rais Jakaya Kikwete akiwa nje ya nchi,
tena akiwa katika majukumu mazito ambayo dunia nzima ilikuwa
ikiyafuatilia kwa shauku na umakini mkubwa.
Kulifungia gazeti wakati huo hatuoni kama ilikuwa kwa masilahi ya taifa kwa sababu hatua hiyo iliichafua taswira ya nchi yetu na bila shaka Rais Kikwete alijikuta katika wakati mgumu kila alipoulizwa kuhusu hatua hiyo iliyochukuliwa na Serikali yake.
Kulifungia gazeti wakati huo hatuoni kama ilikuwa kwa masilahi ya taifa kwa sababu hatua hiyo iliichafua taswira ya nchi yetu na bila shaka Rais Kikwete alijikuta katika wakati mgumu kila alipoulizwa kuhusu hatua hiyo iliyochukuliwa na Serikali yake.
Ni habari zipi zilizolipeleka gazeti
hili kifungoni? Habari ya kwanza ilikuwa juu ya waraka kuhusu mishahara
mipya ya watumishi wa Serikali ambayo tuliithibitisha pasipo kuacha
shaka yoyote kutoka katika vyanzo vyetu vya habari vya kuaminika katika
mamlaka za juu serikalini.
Tuliuchukulia kama taarifa muhimu sana
kwa watumishi wa Serikali na wananchi kwa jumla na hatukuona sababu ya
Serikali kutaka wananchi wafichwe kuhusu kuwapo kwa mishahara mipya kwa
watumishi wake.
Itakumbukwa kuwa, wiki chache kabla ya
gazeti hili halijachapisha habari hiyo, lilikuwa pia limechapisha
habari kuhusu mishahara mipya katika sekta binafsi kwa mujibu wa waraka
wa Serikali uliotolewa na Wizara ya Kazi na Ajira. Swali linalojitokeza
hapa ni hili: Inakuwaje mishahara mipya ya watumishi wa Serikali iwe
siri na mishahara mipya kwa sekta binafsi iwe kinyume chake?
Tunaamini kwamba utamaduni wa Serikali
kuficha habari na taarifa zenye manufaa kwa umma siyo utawala bora hata
kidogo. Ni hivi majuzi tu Rais Kikwete alipomwagiwa sifa na Rais
Barrack Obama kwa kutia saini mkataba wa uendeshaji wa shughuli za
Serikali kwa uwazi.
Habari ya pili iliyochapishwa Agosti
17 mwaka huu na kusababisha gazeti hili kufungiwa ilihusu Serikali
kuimarisha ulinzi katika maeneo ya karibu na misikiti jijini Dar es
Salaam jana yake kufuatia kuwapo tetesi kwamba waumini wa Kiislamu siku
hiyo wangeandamana kupinga kitendo cha Jeshi la Polisi kumuweka mahabusu
Kiongozi wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa
Ponda. Baadhi ya waumini walikuwa wameonyesha kukasirishwa na kitendo
cha polisi kumwondoa Sheikh Ponda katika Taasisi ya Mifupa Muhimbili
(Moi) na kumpeleka katika Gereza la Segerea, jijini Dar es Salaam.
Habari hiyo yenye kichwa cha habari;
'Waislamu wasali chini ya ulinzi mkali wa polisi' ilichapishwa ikiwa na
mmoja wa mbwa waliokuwa na polisi katika doria kutokana na hofu ya
kuzuka vurugu baada ya Swala ya Ijumaa, Agosti 16. Habari hiyo ilisema
Waislamu hawakuandamana na waliswali kwa amani na utulivu na kwamba
polisi hao waliokuwa na mbwa, huku wengine wakitumia pikipiki kufanya
doria walitanda katika mitaa mbalimbali kwa lengo la kuimarisha ulinzi.
Lakini kwa mshangao wetu, Serikali katika kujaribu kuhalalisha
kulifungia gazeti hili ilitoa tafsiri ya uongo kwamba habari
tuliyochapisha ilisema kwamba mbwa walipelekwa katika maeneo ya ibada,
wakati habari hiyo haikuwa na kitu kama hicho. Serikali ilidai katika
taarifa hiyo, kwamba lengo la habari hiyo lilikuwa kuichonganisha na
waumini wa Kiislamu ili waichukie pamoja na vyombo vyake vya ulinzi na
usalama, kwani kwa Waislamu mbwa ni haramu na picha hiyo iliudhalilisha
Uislamu. Taarifa hiyo potofu ya Serikali imetuthibitishia pasipo kuacha
shaka kwamba haikuwa na nia njema na gazeti hili.
Hatua ya kulifungia gazeti hili kwa
sababu za kufikirika imesababisha maumivu kwa watu wengi. Vijana
(vendors) waliokuwa wakiuza na kusambaza gazeti hili pamoja na familia
zinazowategemea wameumia. Waandishi wa kujitegemea wanaolipwa kutokana
na habari wanazotuma gazetini wameumia pamoja na familia zao. Hivyo
hivyo, watoa matangazo na wasomaji waliokuwa wakilitegemea gazeti hili
kwa habari za uhakika nao pia wameumia. Hasara ambayo MCL imepata
kutokana na hatua hiyo ya Serikali haitamkiki.
Pengine huu ni wakati mwafaka wa
kuikumbusha Serikali kwamba, gazeti hili pamoja na mengine
yanayochapishwa na Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd (MCL), ni
magazeti makini sana yenye waandishi wa habari wanaoheshimu maadili ya
taaluma yao. Hatusemi kwamba hatuwezi kufanya makosa, kwani sisi ni
binadamu.
Hata hivyo, inapotokea tukafanya
makosa tunafanya masahihisho stahiki haraka kwa lengo la kupunguza
maumivu kwa yeyote tuliyemkosea. Makosa ya makusudi kama kuandika habari
za uongo hayavumiliki na kila mwandishi wa kampuni yetu anatambua fika
kwamba kufanya hivyo ni kujitakia kiama.
MCL imeweka miongozo ya sera na
malengo ya uhariri kwa waandishi. Lengo ni kuhakikisha habari
zinazochapishwa ni sahihi, zinatenda haki na haziegemei upande wowote.
Kwa maana hiyo, vyombo vyake vya habari vinasimamia ukweli na haki na
waandishi wake wana jukumu la kuhakikisha wanakuwa na kiwango cha juu
cha weledi na maadili ili kuwawezesha kutoa habari kwa umma.
Tumetoka kifungoni tukiwa na somo
muhimu. Kwamba sheria kandamizi kama Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976
haisimamii masilahi ya taifa, bali kundi la watu wachache. Ni sheria
kandamizi ambayo kwa umoja wetu tunaweza kuifuta. Tungependa kuwashukuru
wasomaji wetu na wananchi kwa jumla kwa kuwa nasi katika kipindi kigumu
tulichokuwa kifungoni. Vilevile, tunavishukuru kwa namna ya pekee
vyombo vyote vya habari vya ndani na nje ambavyo vilisimama imara
kupinga hatua ya Serikali kufungia magazeti.
Tutakuwa watu wasio na shukurani kama
hatutatambua mshikamano mkubwa ulioonyeshwa na asasi za kiraia, mabalozi
na watu mbalimbali kupinga matumizi ya sheria hii kandamizi. Hatujakata
tamaa, bali tumetoka kifungoni tukiwa na hamasa kubwa kuendelea kuwapa
habari wananchi pasipo woga wala upendeleo.
Hatupambani na Serikali, lakini
tutaendelea kuikosoa pale inapofanya makosa na tutaipongeza pale
inapotimiza wajibu wake. Tunawaomba wasomaji wetu mwendelee kutuunga
mkono.
1 comment:
Siku zote ukweli ni MATESO na uongo ni FURAHA ya wachache!!
Post a Comment