Viongozi
wa vyama vikuu vya upinzani nchni kutoka kushoto: James Mbatia (NCCR
Mageuzi), Freeman Mbowe (Chadema) na Profesa Ibrahimu Lipumba (CUF).
Viongozi wa vyama vikuu vya upinzani vyenye wabunge bungeni
wanatarajia kukutana leo na Rais Jakaya Kikwete Ikulu, jijini Dar es
Salaam kuzungumzia utata wa baadhi ya masuala yaliyojitokeza katika
mchakato unaoendelea wa kupata Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania. Kama wengi tunavyotegemea, mazungumzo hayo kwa vyovyote ni ya masuala nyeti ambayo yamesababisha mvutano na kuibua hisia kali miongoni mwa makundi ya kijamii, pengine kwa kutambua fika kwamba kupuuza madai ya wapinzani ingekuwa sawa na kumwaga petroli katika nyumba inayoungua, busara za rais wetu zimemfanya awaite viongozi wa kisiasa kuteta nao Ikulu.
Wakati viongozi hao, Freeman Mbowe wa Chadema, James Mbatia wa NCCR Mageuzi na Profesa Ibrahimu Lipumba wanakutana na kiongozi wa nchi leo, pengine akiwa hajasaini Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ambao ulipelekwa mezani kwake baada ya kupitishwa bungeni na wabunge wa CCM wiki chache zilizopita, watampa mwanga kilichowafanya waugomee bungeni, maana katika hotuba yake alisema ameambiwa hiki na kile sasa atasikia laivu kutoka kwao.
Naamini wazo la Mwenyekiti wa Tume ya Marekebisho ya Katiba, Jaji Joseph Sinde Warioba ambaye alizungumza na wanahabari hivi karibuni na akaonesha kushangazwa muswada huo kuwekwa kipengele cha kuivunja tume hiyo mara baada ya kukabidhi rasimu ya mwisho ya Katiba, litajadiliwa.
Kwa maoni yake Jaji Warioba, baada ya tume yake kuvunjwa haiwezi tena kuhusishwa katika mchakato wa katiba kwa sababu itakuwa haipo tena kisheria.
Mwenyekiti huyo alifafanua kuwa haitakuwa sahihi kisheria tume hiyo baadaye kuitwa katika Bunge Maalumu la Katiba kutolea ufafanuzi masuala yatakayohitaji kufafanuliwa, wala kupewa jukumu la kusimamia Kura ya Maoni kama inavyopendekezwa katika muswada huo ambao Rais Kikwete akiutia saini utakuwa sheria.
Mimi naamini kuwa Jaji Warioba amefanya vyema kubainisha mkanganyiko uliomo katika muswada huo, hasa wakati huu ambapo viongozi wa vyama vikuu vya siasa wanakwenda kuonana na kiongozi wa nchi.
Tayari viongozi wa vyama vya upinzani walishaanza kufanya kampeni nchi nzima kuhamasisha wananchi kuupinga muswada huo.
Pamoja na kupinga uwakilishi mdogo wa makundi ya kijamii katika Bunge Maalumu la Katiba, wanasiasa na wanaharakati wanapinga mapendekezo ya kumpa rais mamlaka ya kuteua wajumbe 166 wa kuingia katika Bunge hilo, huku pia wakipinga Tume ya Warioba kuvunjwa kabla ya kupatikana Katiba Mpya.
Mambo mengine yanayotarajiwa kujadiliwa na wanasiasa hao Ikulu ni pamoja na malalamiko kuhusu uwakilishi mdogo wa Zanzibar katika Bunge hilo na Wazanzibar kutokushirikishwa kikamilifu katika kutoa maoni kuhusu muswada huo.
Mimi naamini kuwa bado viongozi wana nafasi ya kuangazia kwa kina kasoro hizo kubwa, kwani Rais Kikwete bado anayo fursa ya kurekebisha hali hiyo kama ambavyo bado anayo nafasi ya kuamuru kuboreshwa kwa vifungu vinavyolalamikiwa na makundi mbalimbali katika jamii kabla hajatia saini muswada huo kuwa sheria.
Niliwahi kuwashauri wapinzani kupitia safu hii kwamba maandamano hayasaidii ila kinachotakiwa ni pande zote mbili, serikali na wapinzani kukaa katika meza moja ya mazungumzo ili kuondoa upungufu uliojitokeza badala ya wanasiasa kuuteka mchakato huo kwa sababu za kiitikadi.
Bado naamini kuwa hakuna mwananchi aliye na chembe ya shaka kuhusu utendaji na uadilifu wa Tume ya Jaji Warioba ambayo tuna uhakika itatufikisha kule tunakotaka kwenda.
Hakuna atakayebisha nikisema kwamba wananchi walio wengi ni mashahidi jinsi wajumbe wa tume hiyo walivyoweka itikadi zao pembeni na kuweka mbele masilahi ya taifa kwa kuhakikisha katiba hiyo ijayo inakidhi matakwa ya Watanzania wote.
Binafsi niseme wazi kuwa nimefarijika na kutiwa moyo na Jaji Warioba mwenyewe alipokanusha uvumi wa kejeli dhidi ya tume hiyo ambao umekuwa ukitolewa na baadhi ya wanasiasa kuwa zimewavunja moyo baadhi ya wajumbe wa tume, hivyo wanataka kujiuzulu.
Hakika kutokana na msimamo thabiti wa Jaji Warioba niwaombe Watanzania wote kuiunga mkono tume hiyo na nimuombe Rais Kikwete ahakikishe kuwa yale ambayo yanalalamikiwa ambayo ni ya masilahi kwa taifa letu, ayatatue kabla ya kuwa sheria na kikao hicho naamini kitatoa majibu ya maswali yanayojitokeza na lawama zilizoibuka mara baada ya wabunge wa CCM kuupitisha muswada huo unaolalamikiwa.
Naamini kabisa kuwa mkutano wa viongozi hao wa siasa ni mwanga wa amani katika nchi yetu na ni kitu cha kujivunia kwa sababu mkutano huo wa leo ni wa kujenga nchi na siyo kubomoa. Jipu limepasuka, siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli. GPL
No comments:
Post a Comment