Waziri Mkuu Mizengo Pinda.
Waziri Mkuu Mizengo Pinda amewajibu wabunge waliokosoa kitendo cha mawaziri watano waliotajwa kwenye kashfa za Operesheni Tokomeza na akaunti ya escrow, akisema Ikulu haikuhusika kuwasafisha bali ilitangaza matokeo ya uchunguzi wa tume.
Mtendaji huyo mkuu wa Serikali pia amesema mawaziri hao bado wanachunguzwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na Jeshi la Polisi, kuhusu kuhusishwa kwao na operesheni hiyo iliyotekelezwa kwa kukiuka haki za binadamu, na sakata la escrow lililohusisha uchotwaji wa Sh306 bilioni zilizokuwa Benki Kuu.
Wakichangia hotuba ya Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu wiki iliyopita, baadhi ya wabunge walihoji kitendo cha Ikulu kuwasafisha mawaziri wachache na kuwaacha wengine waliojiuzulu kisiasa kutokana na wizara zao kukumbwa na kashfa na kumtaka Waziri Mkuu atoe majibu wakati akifanya majumuisho ya mjadala.
Waliotangazwa kusafishwa ni Emmanuel Nchimbi, aliyekuwa Waziri wa Ulinzi, Shamsi Vuai Nahodha (Mambo ya Ndani), Balozi Hamisi Kagasheki (Maliasili na Utalii) na David Mathayo, aliyekuwa Waziri wa Kilimo na Mifugo.
Wote walishinikizwa na Bunge kujiuzulu kutokana na kashfa iliyotokana na utekelezaji wa Operesheni Tokomeza iliyolenga kukomesha ujangili.
Pia Profesa Sospeter Muhongo, aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, aliyedaiwa kutowajibika ipasavyo katika sakata la escrow na kusababisha Serikali ipoteze mapato, pia amesafishwa sambamba na katibu mkuu wa wizara hiyo, Eliackim Maswi, ambaye aliidhinisha fedha hizo kutolewa.
Akifanya majumuisho hayo jana, Waziri Pinda alisema kitendo cha viongozi hao kujiuzulu nyadhifa zao, kuhojiwa na Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma huku wengine wakisimamishwa kazi, hakikusitisha utaratibu wa kuchunguzwa zaidi na vyombo hivyo.
Pinda alisema kikao cha Mei 8 mwaka huu kati ya Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue na vyombo vya habari, kufafanua kuwa Katibu Mkuu kiongozi huyo alitoa taarifa mbili, kuhusu sakata la escrow na Operesheni Tokomeza.
“Taarifa ya kwanza iliyomhusu Maswi na ilitokana na kazi iliyokuwa imefanywa na timu ya makatibu wakuu baada ya Tume ya Maadili kuwa imemaliza kazi yake. Taarifa ya pili ilikuwa inahusiana na Operesheni Tokomeza,” alisema Pinda.
Katika maelezo ya Balozi Sefue kuhusu Profesa Muhongo na Maswi, alisema waziri huyo wa zamani wa nishati na madini alionekana hana hatia na ndiyo maana hakupelekwa mbele ya Kamati ya Maadili ya Viongozi wa Umma, ambayo pia ilimchunguza Maswi na kumuona kuwa hakuhusika katika uchotwaji huo wa fedha wala kupata mgawo.
“Tume ilisema wengine walioona kuwa wana kesi ya kujibu wanaendelea nao (kuwahoji) mpaka mwisho. Na wakaniambia katika suala hili vyombo vingine (Takukuru na polisi) vinafanya uchunguzi wa kitaalamu na vikipata ushahidi hakutakuwa na pingamizi hata kama Tume imetoa uamuzi wake,” alisema.
“Uamuzi wa Tume si kwamba wahusika wote hawawezi kushtakiwa. Haya (ya Tume na Takukuru) ni mambo mawili tofauti yenye misingi tofauti.”
Alisema kuwa Takukuru wanaendelea na uchunguzi wao na muda ukifika watatoa uamuzi wao na kama itaonekana kuna ushahidi mzito wahusika wote watafikishwa mahakamani.
Kuhusu Operesheni Tokomeza alisema: “Taarifa ya Ikulu haikulenga kumsafisha mtu. Ile ilikuwa ni taarifa kwa umma juu ya kazi ya uchunguzi kuhusu operesheni hiyo.” Huku akikiri wazi kuwa baadhi ya maelezo yaliyotolewa na Sefue yaliwahishwa zaidi, Pinda alisema “kama ni kuwasafisha ingekuwa ni baada ya Rais kutoa uamuzi wake. Kilichotolewa na Ikulu ilikuwa ni taarifa tu ya utekelezaji wa uchunguzi”
Alisema ufafanuzi huo wa Ikulu hauwezi kuondoa uwajibikaji wa kiasiasa kwa mawaziri hao licha ya ripoti kubainisha kuwa hawakuhusika moja kwa moja katika Operesheni hiyo iliyolalamikiwa kukiuka haki za binadamu.
Wakati wakishinikiza mawaziri hao wajiuzulu, wabunge waliwaeleza kuwa suala la kujiuzulu ni uwajibikaji na si kwamba walihusika na kutoa mfano wa Rais wa Serikali ya Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi ambaye aliwahi kujiuzulu kutokana na mauaji yaliyotokea Shinyanga na baadaye akawa Rais wa Jamhuri ya Muungano.
Akerwa na kauli za wwapinzani
Pinda pia alionyesha kukerwa na kauli za wapinzani kwamba Serikali ya CCM haijafanya lolote mpaka sasa katika kila sekta, kumuomba Spika wa Bunge, Anne Makinda ili atoe ufafanuzi juu ya kauli hizo.
No comments:
Post a Comment