TAARIFA KWA WADAU
Leo tarehe 25 Februari mwaka 2013 ndio ilikuwa iwe siku nyingine ya kihistoria katika medani ya muziki wa kizazi kipya.
Kwa siku kadhaa sasa tumekuwa
tukitangaza kwamba wimbo mpya wa MwanaFA ulio katika mahadhi ya Hip Hop
uitwao “Kama Zamani” aliowashirikisha Man'dojo, Domokaya na The
Kilimanjaro Band (Wana Njenje) ungeanza kuuzwa kupitia njia mbalimbali
kama ‘iTunes’, ‘Amazon’ na kupitia katika simu za mkononi.
Pia ndio tarehe ambayo Kama Zamani ingeanza kusikika katika vituo vya redio Tanzania na nchi za jirani.
Lifeline Music Inc. ndiyo
inayosimamia muziki wa MwanaFA kwa sasa, ikiwa ni kampuni ambayo
inafanya kazi za muziki, kuangalia na kuhakikisha kwamba wasanii
inaowasimamia wananufaika kwa kiasi kikubwa kutokana na kazi zao; na
kwamba muziki unaofanyika kwa sasa unafuata kanuni zote zinazosimamia
makubaliano ya biashara.
Kama mjuavyo, biashara yoyote ina
pande mbili na mafanikio yake yanategemea zaidi maridhiano baina ya
pande hizo na utimizaji wa vipengele tofauti ndani ya mikataba ya
biashara.
Katika kuboresha maslahi ya
wanamuziki husika na wimbo huu,pia kuboresha zaidi njia zitakazotumika
kuhakikisha ya kwamba burudani hii itawafikia washabiki wengi zaidi wa
muziki unaofanywa na MwanaFA, Kilimanjaro Band(Wana Njenje) na Man’Dojo
na Domokaya, tumefikia uamuzi wa kusubiri na kusogeza mbele siku ya
kuachia wimbo wa Kama Zamani kama ilivyopangwa hapo awali.
Tunachukua nafasi hii kuwaomba
radhi mashabiki ambao mmekuwa mnasubiri kwa hamu kusikia ni nini
muungano huu wa muziki wa kizazi kipya na moja ya bendi kongwe kabisa za
muziki yenye miaka zaidi ya 40 katika tasnia ya muziki Tanzania
umewaandalia.
Kwa niaba ya MwanaFA, uongozi wa
Lifeline Music Inc. unaomba uvumilivu na subira toka kwenu mashabiki na
wapenzi wa muziki. Tunaamini kwamba subira huvuta heri na mambo mazuri
hayahitaji haraka.
Tunawashukuru kwa dhati kwa ushirikiano wenu.
Henry Mdimu
PR Strategist
Lifeline Music Inc
No comments:
Post a Comment