NAIBU Spika, Job Ndugai ametetea uamuzi wake wa kuagiza kutolewa ndani ya ukumbi wa Bunge, Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe akisema alikuwa sahihi.
Mabishano hayo ambayo yalisababisha kuibuka kwa vurugu bungeni yalitokea mwishoni mwa wiki, muda mfupi baada ya kipindi cha maswali na majibu, ambapo kiongozi huyo wa Bunge aliruhusu mjadala kuhusu Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba uendelee.
Kutokana na hali hiyo, Mbowe alisimama kutaka kutoa ufafanuzi juu ya mjadala huo, lakini Ndugai alimzima na kumtaka kukaa chini, jambo ambalo halikumfurahisha Mbowe na kumfanya agomee agizo lake.
Akizungumza na MTANZANIA jana kwa njia ya simu, Ndugai alitumia muda mwingi kutetea uamuzi wake na kukosoa hoja za watu wanaompinga juu ya uamuzi wake huo.
Ndugai alisema katika kikao hicho, Mbowe alifanya jeuri kubishana na kiti na kueleza kuwa kanuni za Bunge zinasema hakuna mbunge yeyote atakayesimama kuzungumza bila kuruhusiwa na kwamba uamuzi wa kiti ndiyo wa mwisho.
Ndugai alisema wanaomtuhumu kwamba hakutenda haki kumuamuru Mbowe akae chini, wanafanya hivyo kwa vile hawajui kanuni za Bunge.
Ndugai alisema kwa mujibu wa kanuni, ni Rais wa Jamhuri pekee ndiye anayeruhusiwa kulihutubia Bunge kwa wakati anaoona yeye unafaa, lakini si mbunge.
“Hata rais mwenyewe ni lazima amwandikie barua spika, huu ndiyo utaratibu lakini si mbunge au waziri anayeruhusiwa kusimama kwa wakati anaoutaka yeye kuzungumza akaruhusiwa, ni lazima ataomba ruhusa kwa Spika na kama ipo nafasi ya kufanya hivyo Spika atamruhusu, kama haipo hataruhusiwa.
Alipoulizwa kwamba haoni kama alivunja kanuni kwa kumzuia Kiongozi wa Upinzani bungeni wakati kanuni za mabunge ya Jumuiya ya Madola zinatoa upendeleo kwa kiongozi huyo na waziri mkuu ndani ya Bunge, Ndugai alisema:
“Katika vikao vya Bunge, uamuzi wowote wa Spika unakuwa wa mwisho na hauwezi kupingwa na mbunge au waziri yeyote.
“Mbowe nilimuomba kwa heshima sana atupishe kwanza, nilimuelekeza karibu mara tatu…lakini mtu mzima anavunja utaratibu.
“Huyu Mbowe amejivunjia heshima mwenyewe, hata kanisani anayeendesha ibada ni mtu mmoja tu, na wengine wanapaswa kufuata utaratibu.
“Kwanza Mbowe alijitoa mwenyewe kwenye orodha kwa maandishi na ninayo hapa.... yeye na Halima Mdee, sasa alisimama kufanya nini kama sio ujeuri?
“Kanuni anazijua mimi ningemruhusu tu, lakini kwa ujeuri hakufanya hivyo. Kuna taratibu za bunge, mbunge anakaa chini pale Spika anaposimama na wasome kanuni, sasa hapo mjeuri ni nani?
“Tujifunze kanuni haiwezekani mtu yeyote asimame saa yoyote, kila mmoja hawezi kufanya anavyotaka, kuna taratibu zake, kiti kikimuona atapewa nafasi kama ipo na iwapo kiti kikiridhika,” alisema Naibu Spika.
Awatetea askari wa Bunge
Akizungumzia hatua ya kuwaamuru askari wa bunge kuingia ndani ya ukumbi wa Bunge na kumtoa Kiongozi wa Upinzani, iwapo kama amevunja kanuni, Ndugai alisema hakuvunja kanuni na kufafanua kila askari aliye kwenye viunga vya bunge yuko chini ya himaya ya kiti.
“Kila askari aliye kwenye eneo la bunge au viunga vya bunge kuanzia polisi, usalama wa taifa na wengine wote siwezi kuwataja hapa, hao wote wako chini ya bunge ni Sajent at Arms.
“Askari polisi wote unaowaona bungeni wanaletwa na RPC Dodoma na wanakuwa chini yetu, hakuna askari aliyetoka nje siku ile…. Ni uongo na hawajui kanuni.
“Uamuzi wa kuita wanausalama ndani ya ukumbi ulikuwa ni uamuzi sahihi, hakuna askari aliyetoka nje ya bunge,” alisisitiza Ndugai.
Msekwa amuunga mkono Ndugai
Naye Spika Mstaafu aliyeongoza Bunge la nane, Pius Msekwa alimtetea Ndugai akisema kuwa haoni kosa lolote lililofanywa na kiongozi huyo wa Bunge.
Msekwa ambaye alipata kuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM (Tanzania Bara), alisema ni jambo la kawaida ndani ya Bunge, Spika kumuamuru mbunge au waziri kukaa chini pale anapoona inafaa.
“Spika ni sawa na mwenyekiti wa kikao chochote, anayo madaraka ya kuruhusu nani aseme, nani asiseme.
“Tuje bungeni sasa, Ndugai ndiye anayeamua nani aseme, ni sahihi ndiye mwenye mamlaka hayo na ni jambo la kawaida kabisa,” alisema Msekwa.
Akitoa uzoefu wake wa bunge alilokuwa akilisimamia, Msekwa alisema matukio yanayotokea bungeni sasa yamegubikwa na hisia za ujana zaidi na kusisitiza wazee walio nje ya bunge wanatafakari cha kufanya kabla hali haijaharibika.
“Sisi yetu macho… lakini kila zama na kitabu chake, hizi ndio zama za vijana, wakati wetu haya hayakuwapo…lakini ikifikia hatua ya kutaka kuliteketeza bunge lazima tutachukua hatua… lakini dalili sio nzuri,” alisema Msekwa.
-Mtanzania
No comments:
Post a Comment