Tuesday, September 10, 2013
JALADA LA SUGU LATUA KWA DPP
JALADA la Kesi inayomkabili Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi (CHADEMA), limefikishwa katika Ofisi ya Mwanasheria wa Serikali. Mbilinyi maarufu kwa jina la ‘Sugu’(pichani), anadaiwa kumjeruhi askari wa Bunge katika vurugu zilizotokea Bungeni mwishoni mwa wiki iliyopita. Kwa mujibu wa Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Susan Kaganda alisema polisi wameshapeleka jalada la mbunge huyo katika Ofisi ya Mwanasheria wa Serikali na kwamba upelelezi unaendelea.
“Tayari jalada la kesi yake lipo katika Ofisi ya Mwanasheria wa Serikali na upelelezi unaendelea,” alisema.
Kwa mujibu wa vyanzo kutoka Jeshi hilo, Sugu alikwenda Polisi kujisalimisha siku ya kuahirishwa Bunge na kwamba aliambiwa arudi tena kuripoti Jumatano (kesho). “Kama akiripoti Jumatano, ndiyo itajulikana na kama jalada lake litakuwa limeshafikishwa mahakamani au bado,” kilieleza chanzo hicho.
Habari za uhakika kutoka katika Mahakama ya Mkoa wa Dodoma hadi jana mchana, hakukuwa na jalada lolote lililokuwa limefika mahakamani linalomuhusu Sugu. “Kwa leo (jana), majalada yaliyopokelewa hadi sasa ni mawili tu na yote yanahusu ‘Trafiki kesi’ kilieleza chanzo hicho.
Kusakwa kwa mbunge huyo kulitokana na vurugu zilizotokea katika ukumbi wa Bunge ambao uligeuka ulingo wa masumbwi, baada ya wabunge wa kambi ya upinzani kupigana hadharani na askari wa Bunge.
Wabunge hao walichapana ndani na nje ya ukumbi, hali iliyosababisha tafrani kubwa, huku maofisa usalama na askari polisi kutoka kituo kikuu mjini Dodoma, wakilazimika kuitwa kwenda kuongeza nguvu ili kukabiliana na hali hiyo.
Hatua ya vurugu hizo, ilikuja baada ya Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe kunyanyuka ili kutaka kutoa hoja, ambapo Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai alimtaka kukaa chini hali iliyowafanya wabunge wote wa upinzani kunyanyuka wakiashiria kumuunga mkono.
Katika vurugu hizo, ‘Sugu’, inadaiwa alimpiga kichwa, ngumi na kumjeruhi jicho la upande wa kulia Koplo Nikwisa Nkisu.
Chanzo cha vurugu hizo ni madai ya wabunge kutoka vyama vya Chadema, CUF na NCCR- Mageuzi kutaka kuahirishwa kwa Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba kwa kuwa mchakato wa kuandaliwa kwake haukuwashirikisha Wazanzibari. Mwisho MTANZANIA
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment