Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Utamaduni, Bibi. Lilly Beleko kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo akimkabidhi Mzee Muhidini Gurumo barua kama ishara ya Serikali kutambua mchango wake uliotukuka katika tasnia ya Muziki nchini pamoja na kumpongeza kwa kustaafu kazi kazi hiyo, hivi karibuni nyumbani kwake Makuburi, Jijini Dar es Salaam. Wanaoshuhudia nyuma ya Mkurugenzi ni Rais wa Shirikisho la Muziki Tanzania, Bw. Addo Mwasongwe na kulia pembeni ya Mzee Gurumo ni Mkewe, Bibi. Pili Said Kitwana.
Nguli wa Muziki wa Dansi, Mzee Muhudini Gurumo (aliyevaa shati la drafti) akiwa na watumishi wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, walipomtembelea nyumbani kwake Makuburi Jijini Dar es Salaam hivi karibuni. Serikali kupitia Wizara hiyo ilimkabidhi barua rasmi Mzee huyo kutambua mchango wake katika tasnia ya Muziki na kumpongeza kwa kustaafu kazi hiyo.
Wa kwanza kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Utamaduni, Bibi Lilly Beleko, wa pili ni mke wa Mzee Gurumo, Bibi. Pili Said Kitwana na wa Pili Kushoto ni Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Wizara Upande wa Sanaa, Bibi. Joyce Hagu.
Picha zote na Concilia Niyibitanga
Serikali kupitia Wizara ya Habari,
Vijana, Utamaduni na Michezo imempongeza Mzee Muhidini Gurumo kwa
mchango wake uliotukuka katika tasnia ya Muziki nchini pamoja na
kumpongeza kwa kustaafu kazi hiyo.
Akiwasilisha barua ya Serikali ya
kutambua mchango wa nguli huyo juzi nyumbani kwake Makuburi Jijini Dar
es Salaam, Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Utamaduni kutoka Wizara ya
Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Bibi. Lilly Beleko amesema kuwa
Serikali inatambua na kuthamini mchango wake katika muziki wa Dansi hapa
nchini.
'Serikali inathamini mchango wako
katika Muziki hapa nchini na itaendelea kuzienzi kazi hizo na
inakupongeza kwa kazi nzuri ulioifanya ya kuelimisha, kuhamasisha na
kuburudisha jamii'. Amesema Bibi. Beleko.
Naye Rais wa Shirikisho la Muziki
nchini, Bw. Addo Mwasongwe, amesema kuwa Shirikisho linampongeza kwa
kazi zake nzuri na litaendelea kumtumia katika kazi za muziki ikiwa ni
pamoja na kutoa ushauri katika tasnia hiyo.
Nguli huyo wa muziki wa dansi nchini
katika enzi zake za uimbaji ametunga nyimbo za kuelimisha jamii kufanya
kazi kwa bidii, kudumisha usawa, amani na kuwakumbusha wazazi kutimiza
wajibu wao wa kuwalea watoto katika maadili mema.
Mzee Gurumo ambaye ameanza kazi ya
muziki mnamo miaka ya 1960 na kustaafu kazi hiyo mwaka huu amesema kuwa
anaishukuru Serikali kwa kutambua kazi yake na amefarijika kwa
kukabidhiwa barua ya kumtambua na kumpongeza kwa kustaafu kazi hiyo.
(na Concilia Niyibitanga- WHVUM)
MWISHO
No comments:
Post a Comment