Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi
Taifa, Rais Jakaya Kikwete amewataka wanachama wa chama hicho kuacha
unyonge na kusema uvumilivu una kikomo chake.
Aliyasema hayo jana wakati anafungua
kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec) ya CCM, kilicholenga kuweka
msimamo wa chama kuhusu Rasimu ya Katiba Mpya ambayo inaanza kujadiliwa
Jumanne wiki ijayo.
"Tuna uchaguzi mdogo, Iringa, Kalenga,
tumeshapata mgombea na tumefanya hiyo kazi kwa niaba yenu kwa sababu
hatukupata muda wa kuitisha Kikao cha Halmashauri Kuu, lakini mmetupatia
mamlaka ya kufanya hivyo na Katiba imetupa fursa ya kufanya uteuzi kwa
niaba yenu,"alisema.
CCM imemteua Godfrey Mgimwa ambaye ni
mtoto wa aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, marehemu Dk William Mgimwa,
kupeperusha bendera katika uchaguzi mdogo utakaofanyika baadaye mwaka
huu. Dk Mgimwa hadi anafariki dunia alikuwa Waziri wa Fedha.
Uchaguzi mdogo wa ubunge Jimbo la
Kalenga lililopo mkoani Iringa unatarajiwa kufanyika Machi 16, mwaka
huu, huku tayari vyama vya CCM na Chadema vikiwa vimetaja wagombea wake,
Chadema kikiwa kimetangaza, Grace Tendega Mvanda.
Rais Kikwete alisema chama hicho kinashindana na vyama vingine katika uchaguzi huo mdogo.
"Tunashindana na wenzetu wagomvi,
maana wao ugomvi ndiyo sehemu ya mwongozo wa kufanya kazi ya
siasa,"alisema Kikwete bila kutaja chama chochote cha siasa kwa jina.
Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-like page ya facebook ya Jambo Tz
"Tulizungumza nalo hilo kwenye Kamati
Kuu, tulikubaliana kuacha unyonge. Ndiyo, kwenye Kamati Kuu
tumekubaliana, tumesema jamani watu wote waende wakaseme tumekubaliana
kuacha unyonge," alisema huku akicheka na kupigiwa makofi na wajumbe wa
Nec.
Rais Kikwete ambaye pia ni Amiri Jeshi
Mkuu, alitolea mfano wa tukio lilitokea Kahama mkoani Shinyanga, ambapo
kijana mmoja alitolewa macho kwa bisibisi, na tukio la Igunga ambapo
kijana mmoja alimwagiwa tindikali katika uchaguzi mdogo wa jimbo hilo.
"Acheni unyonge na hata katika taarifa
ya habari leo (jana) mtoe hivyo hivyo. Na mwache habari zote mseme hii
tu (waandishi wa habari). Uvumilivu una ukomo wake," alisema huku
wajumbe wakiendelea kumpigia makofi.
"Nalisema kwa sababu yanayotokea
yanasikitisha sana. Pale Igunga kijana yule wamemwagia tindikali, pale
Kahama kijana ametolewa macho kwa bisibisi,"alisema.
Hata hivyo, Rais Kikwete aliwataka
wanachama wa CCM kujipanga vizuri katika uchaguzi huo, ili kuhakikisha
wanapata ushindi mnono.
Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-like page ya facebook ya Jambo Tz
"Mpaka sasa kwa dalili tulizonazo
hatuna mgawanyiko wala hakuna misukosuko maana lile la Arumeru (uchaguzi
mdogo katika Jimbo la Arumeru Mashariki) lilikuwa na misukosuko tangu
tumeanza hadi tumemaliza," alisema.
Katika uchaguzi huo, uliofanyika
Aprili mosi, 2012 mgombea wa Chadema, Joshua Nassari aliibuka mshindi
baada ya kumshinda Sioi Sumari wa CCM ambaye ni mtoto wa marehemu
Jeremiah Sumari, aliyewahi kuwa Naibu Waziri wa Fedha na Uchumi mwaka
2008 hadi 2010.
Alitumia fursa hiyo kuwapongeza
viongozi na wanachama wa CCM katika kata 23, ambazo CCM iliibuka na
ushindi na kuwataka kuweka nguvu zaidi katika kuzikomboa kata nne
zilizoangukia mikononi mwa wapinzani.
Kata ambazo wapinzani walishinda ni
Sombetini (Arusha Mjini), Kiboroloni (Moshi Mjini), (Njombe Mjini),zote
zilichukuliwa na Chadema. Kilelema mkoani Kigoma (NCCR Mageuzi).
Aidha, Rais Kikwete alisema awali
wakati wanaahirisha kikao cha Nec kilichopita, walikubaliana watakuwa
wakihamia mikoani kufanya vikao hivyo ambapo Mbeya waliomba kuwa wenyeji
na walikubaliwa.
Hata hivyo, alisema waliamua kufanya
tena kikao hicho mjini hapa, kwa sababu ya agenda watakazozizungumza
kwenye kikao hicho ambazo ni suala linalohusu mchakato wa Katiba Mpya.
"Ili tutakapoyamaliza, tujue tuweke
misimamo gani itakayokwenda kwenye Bunge la Katiba. Haina maana kuwa ile
agenda yetu ya Mbeya tumeifuta, ahadi iko palepale, kikao
kitakachofuata cha kawaida kitafanyikia Mbeya,"alisema.
Awali Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman
Kinana, akimkaribisha Rais Kikwete, alisema kuwa wajumbe wa Nec ni 372,
lakini waliohudhuria walikuwa ni 368 (sawa na asilimia 98.3) hadi kikao
kinafunguliwa.
Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-like page ya facebook ya Jambo Tz
No comments:
Post a Comment