Friday, August 28, 2015

WATU 9 WA FAMILIA MOJA WATEKETEA KWA MOTO, ANGALIA PICHA ZAIDI


Askari na wakazi wa Buguruni Malapa, Dar es Salaam wakitazama nyumba iliyoteketea kwa moto na kuua watu tisa wa familia moja usiku wa kuamkia jana.

Watu tisa wa familia moja wameteketea kwa moto baada ya nyumba yao kuungua usiku wa kuamkia jana jijini Dar es Salaam, huku mashuhuda wakisema walikuta miili yao ikiwa imeshikana.

Juhudi za kuwaokoa watu hao waliofariki dunia wakiwa kwenye moja ya vyumba vya nyumba hiyo namba 40 iliyoko katika Mtaa wa Ulam, Buguruni Malapa wilayani Ilala, zilishindikana na chanzo cha moto huo hakijajulikana ingawa mashuhuda wanasema mtungi wa gesi ulilipuka baada ya moto kuwaka kwa muda mrefu.

Walioteketea katika tukio hilo ni mama wa familia hiyo, Samira Juma Ibrahim (42), maarufu kwa jina la Mama Aisha na watoto wake wanne, Ahmed Masoud (15) aliyekuwa mwanafunzi wa kidato cha kwanza, Aisha Masoud (17), aliyekuwa mwanafunzi wa darasa la sita, Abdillah Masoud (10) na Ashraf Masoud (5).

Wengine ni Bimdogo Masoud (72), ambaye alikuwa mgonjwa na mama wa Samira, pamoja na wadogo zake wawili wa kike, Samira Harood (17) na Wahat Saleh (27), ambaye alitokea Unguja, pamoja na Fahir Fesal mwenye umri wa mwaka mmoja na nusu. Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-like page yetu ya facebook bofya Jambo Tz sasa.
Mashuhuda wa tukio hilo walisema baada ya kusikia kelele za vilio, waliizunguka nyumba hiyo kwa lengo la kutaka kuwaokoa, lakini ilishindikana baada ya milango kutofunguka na moto kuwa mkali kiasi cha kushindwa kuingia.

“Katika namna ya kujaribu kujiokoa, Ahmed alijaribu hata kurusha nje funguo ili waweze kufunguliwa mlango, lakini ilishindikana. Hivyo alirudi chumbani wakashikana pamoja kusubiri kifo,” alisema Suleiman Bashraf (45), ambaye ni kaka wa Samira. 

Bashraf, anayeishi Mikocheni na ambaye anasema alifika eneo la tukio wakati dada yake na watoto wake wakiwa wameshafariki, alibainisha kuwa baba wa familia hiyo, Masoud Materu ambaye ni mfanyakazi wa kampuni ya Kimataifa ya Huduma za Kontena (TICTS) inayofanya kazi kwenye Bandari ya Dar es Salaam, alikuwa kazini wakati wa tukio hilo.

Alisema alipopigiwa simu hakuelezwa kuhusu tukio hilo, badala yake wafanyakazi wenzake walimsindikiza hadi Msikiti wa Ulam na baadaye saa tatu asubuhi alipelekwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambako maiti za waliofariki zimehifadhiwa.

Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema wamepokea taarifa ya tukio hilo na jeshi hilo linaendelea na uchunguzi.

Mashuhuda wasimulia

Shuhuda mmoja wa tukio hilo, Hassan Banda alisema ingawa alifika eneo hilo mapema, walishindwa kuingia ndani kuwa mlango wa nondo haukuweza kufunguka. 

Alisema baadaye, mmoja wao aliruka ukuta lakini alikuta hali ni mbaya kwani mlango wa nyuma wa kutokea jikoni ndiko moto ulikuwa umeanzia na ulikuwa mkali sana, hivyo akalazimika kurudi upande wa mbele. “Kuna kijana mmoja (marehemu Ahmed) ndiye tulikuwa tukiwasiliana naye tukimpa maelekezo akiwa ndani ya nyumba. Tulimwambia alete chuma cha kuvunjia, lakini akaleta funguo na kuurusha nje. Kwa kuwa kitasa kilishapata moto ilishindikana kufungua,” alisema. 

“Baadaye akasema anakwenda chumbani kwa bibi yao. Waliendelea kulia wakihitaji msaada, lakini baadaye kukawa kimya na hapakuwa na mawasiliano tena.” Shuhuda huyo alisema muda mfupi baadaye walisikia kishindo kikubwa cha kulipuka kwa mtungi wa gesi na kisha paa la nyumba likashuka chini, lakini akasema wakati huo tayari watu wote walishafariki dunia.

Shuhuda mwingine anayeishi mtaa wa pili kutoka eneo la tukio, Selemani Matumla alisema askari wa Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji walifika wakiwa na vifaa vya kuvunjia kama vile sululu na nyundo na kwamba ndipo walipovunja nyumba na kuingia ndani huku wakiendelea kuzima moto uliokuwa bado unaendelea. 

“Tulipofika chumba cha mwisho tulikuta watu tisa wameshafariki. Walikuwa wameungua vibaya kiasi kwamba haikuwa rahisi kuwatambua. Walifia pamoja chumbani wakiwa wameshikana,” alisema Matumla Ofisa Uhusiano Msaidizi wa Muhimbili, John Steven alisema maiti za watu hao zilihifadhiwa hapo.

Marehemu walizikwa jana kwenye Makaburi ya Kisutu baada ya ibada iliyofanyika katika Hospitali ya Taifa Muhimbili. Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-like page yetu ya facebook bofya Jambo Tz sasa.

No comments:

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...