Rais Jakaya Kikwete
anatarajiwa kuwasili Dodoma keshokutwa, ikiwa ni siku moja kabla ya
kuwasilishwa kwa Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2014/15.
Habari zilizopatikana jana zinasema
Rais ataongoza kikao cha Baraza la Mawaziri kitakachopewa muhtasari
kuhusu Bajeti ya Serikali ya mwaka ujao wa fedha na baadaye atafuatilia
uwasilishaji wa bajeti hiyo bungeni akiwa Dodoma.
Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Salva
Rweyemamu alisema asingeweza kuzungumzia suala hilo kwa kuwa yuko
likizo lakini akaweka bayana kwamba kwa kawaida kabla ya bajeti
kuwasilishwa bungeni, lazima Baraza la Mawaziri lipewe muhtasari wa
bajeti husika.
"Ni kawaida kabla ya bajeti
kuwasilishwa, Rais huongoza kikao cha Baraza la Mawaziri yaani pre
budget cabinet meeting ambako Waziri wa Fedha hutoa briefing (muhtasari)
kuhusu maeneo muhimu ya bajeti, kwa hiyo siyo jambo jipya ni suala la
kawaida," alisema Rweyemamu.
Itakumbukwa kuwa mwaka jana kabla ya
kusomwa kwa bajeti ya 2013/14, Rais Kikwete alikuwa Dodoma ambako pamoja
na kukutana na mawaziri, pia alifanya kikao na Kamati ya Bunge ya
Bajeti.
Hata hivyo, uwepo wake mjini Dodoma
safari hii umekuja wakati kukiwa na dalili za mvutano mkubwa kati ya
Bunge na Serikali kutokana na kutotolewa kwa fedha za kutosha za
maendeleo kwa mwaka wa fedha unaoisha Juni 30 mwaka huu. Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya neno Jambo Tz
Taarifa zinasema bajeti inayomalizika
mwishoni mwa mwaka huu, inapungukiwa kiasi cha Sh1.8 trilioni, huku
Serikali ikilaumiwa na wabunge kwa kutoa misamaha ya kodi inayofikia
Sh1.52 trilioni, ambayo ingepunguza nakisi iliyopo kwenye bajeti kwa
asilimia 84.4.
Wakati wa mjadala wa bajeti za wizara
tangu kuanza kwa Bunge la Bajeti Mei 6 mwaka huu, wabunge wamesikika
mara kadhaa wakilalamika kwamba fedha za maendeleo zilizotolewa kwa
wizara katika bajeti ya 2013/14 ni kati ya asilimia 25 na 30, jambo
ambalo limesababisha kukwama kwa miradi mingi.
Keshokutwa itakuwa siku ya mwisho ya
mashauriano baina ya Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Bunge kupitia
Kamati yake ya Bajeti inayoongozwa na Mbunge wa Bariadi Magharibi,
Andrew Chenge.
Mazungumzo hayo yaliyoanza Juni 5
mwaka huu, yalilenga kuangalia uwezekano wa kutafuta vyanzo vipya vya
mapato ili kuwezesha kuzingatiwa kwa ushauri wa wabunge, pamoja na
kusaka fedha kuziba pengo la Sh1.8 trilioni katika bajeti ya 2013/14.
Alipoulizwa jana, Chenge hakuwa tayari
kuzungumzia hatua iliyofikiwa katika mashauriano hayo na badala yake
alisema kwa ufupi: "Ndugu yangu mambo ya Bunge, tutakutana kwenye
taarifa yetu ya kamati tutakayoiwasilisha bungeni." Kamati ya Bajeti
katika maoni yake iliyoyatoa Juni 17 mwaka jana kuhusu Bajeti ya
Serikali ya 2013/14, iliweka bayana kuwapo kwa udhaifu mkubwa katika
ukusanyaji wa mapato, baadhi ya wizara kutumia fedha nyingi kuliko
ilivyoidhinishwa na Bunge na Serikali kuwa na matumizi makubwa kuliko
mapato yake.
Sehemu ya taarifa hiyo iliyosomwa na
Chenge ilibaini kuwa katika bajeti ya 2011/12 Serikali ilitumia kiasi
cha Sh1.3 trilioni ya mapato yake na mwaka wa fedha uliofuata 2012/13
ilizidisha kiasi cha Sh1.5 trilioni
"Hali hii imesababisha Serikali
kuendelea kukopa kutoka nje na ndani kwa ajili ya kufidia pengo la
upungufu wa fedha. Kamati imebaini kuwa kuendelea kukopa ambako hakuendi
sambamba na juhudi za ukusanyaji wa mapato, kutaendelea kuwa mzigo kwa
nchi kwani itaendelea kukopa na kuongeza kiasi cha matumizi," inasomea
sehemu ya taarifa hiyo.
Mashauriano
Habari zilizopatikana kutoka Dodoma
zinasema vikao vya majadiliano baina ya Serikali na Bunge vinaendelea
leo baada ya kusitishwa Jumamosi saa tano usiku, huku kukiwa na mjadala
mkali kuhusu uwezekano wa kupatikana kwa fedha za kutekeleza bajeti
inayofikia ukomo wake mwezi huu.
"Kwa kweli mvutano umekuwa mkali kati
ya Waziri wa Fedha na watendaji wa wizara hiyo kwa upande mmoja, dhidi
ya wajumbe wa Kamati ya Bajeti kwa upande mwingine. Kubwa ni kutizama
vyanzo vipya vya mapato," kilidokeza chanzo chetu.
Habari zinasema katika kikao
kilichofanyika Ijumaa, hoja iliyotawala ilikuwa ni kutafutwa kwa vyanzo
mbadala vya mapato na wajumbe wa kamati hiyo waliibana Serikali
wakiitaka iondokane na utamaduni wa kutoza fedha kutoka kwenye soda,
bia, maji na sigara pekee.
Hata hivyo, wiki iliyopita Spika wa
Bunge, Anne Makinda alisema katika kikao hicho cha Kamati ya Bajeti na
Serikali hakuna fedha zitakazoongezwa na kitakachofanyika ni kutoa fedha
kutoka eneo moja na kupeleka eneo jingine lenye umuhimu na uharaka
katika utekelezaji wake.
Miongoni mwa maeneo ambayo wabunge
wanaitaka Serikali kuongeza fedha ni sekta ya maji ambayo inapendekezewa
iundiwe mfuko wa maji vijijini ili kuikabili kero hiyo ambayo imekuwa
na athari kubwa kwa wananchi.
Shinikizo la wabunge kuhusu suala la
mfuko wa maji limekuja wakati Wizara ya Maji hadi sasa ikiwa inahitaji
kupewa kiasi cha Sh126 bilioni ambazo ziliidhinishwa katika bajeti ya
2013/14.
Katika kujaribu kupunguza nakisi hiyo,
Serikali ilikubali kutafuta kiasi cha Sh100 bilioni kabla ya mwaka huu
wa fedha kumalizika ili zielekezwe katika miradi ya maji na taarifa
zinasema tayari imetoa Sh80 bilioni.
Wakati wa mjadala wa Wizara ya Afya,
wabunge pia walichachamaa wakikosoa hatua ya kupunguzwa kwa kiasi cha
Sh131 bilioni ikilinganishwa na mwaka wa fedha unaomalizika na kwamba
punguzo hilo litaathiri kwa kiasi kikubwa tiba na huduma za afya nchini.
Mwaka ujao wa fedha, wizara hiyo
imeidhinishiwa Sh622 bilioni, ikilinganishwa na kiasi cha Sh753 bilioni
zilizoidhinishwa 2013/14.
Wizara ya Uchukuzi nayo ilikuwa na
wakati mgumu wakati wa mjadala wa makadirio yake ya matumizi, pale
wabunge walipochachamaa wakitaka fedha ziongezwe kwa ajili ya Shirika la
Ndege (ATCL), ukarabati wa meli ya MV Victoria na upanuzi wa Uwanja wa
Ndege wa Mwanza. Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya neno Jambo Tz
No comments:
Post a Comment