- Magaidi wa Marekani, Uingereza, Syria wahusika
SHAMBULIO la kigaidi lililofanywa
nchini Kenya Jumamosi iliyopita na watu waliodhaniwa kuwa wafuasi wa Al-
Shabab, sasa limeelezwa kutekelezwa na mtandao mpana zaidi wa kigaidi
wa kundi la Al-Qaeda.
Baadhi ya wachambuzi na wachunguzi wa
masuala ya kiusalama na kimataifa, wameyataja mambo matatu ambayo
yanathibitisha pasipo shaka kwamba waliotekeleza tukio hilo la kuvamia,
kuteka nyara na kuua watu wapatao 68 katika Kituo cha Biashara cha
Westgate, ni wa aina ya kundi ambalo kinadharia na kimatendo linafanana
na lile la kigaidi duniani la Al-Qaeda. Mambo yanayotajwa na wachambuzi
na wachunguzi hao ni pamoja na mbinu, teknolojia na aina ya watu
waliotumika kutekeleza shambulio hilo.
Katika uchambuzi wao, wameeleza kuwa
mbinu iliyotumiwa na magaidi hayo kuvamia pasipo kujulikana mara moja na
vyombo vya ulinzi na usalama vya nchini Kenya, lakini pia aina ya
silaha walizokuwa nazo, inaonyesha kuwa kundi hilo limeamua kutumia
kivuli cha Al-Shabab kufikisha ujumbe kwa dunia kwamba lipo licha ya
uongozi wake kubadilika.
Kwamba mbali na mbinu pamoja na
teknolojia, pia aina ya watu waliohusika kutekeleza shambulio hilo ambao
wamebainika kutoka katika mataifa mbalimbali duniani, ndio ambao
wamewafanya wachambuzi na wachunguzi hao waanze kupata shaka kwamba
huenda kuna kundi kubwa zaidi lililotekeleza shambulio hilo, ambalo
limejivika taswira ya Al-Shabab.
Watu wanaotajwa kuvamia kituo hicho
cha biashara na kutekeleza unyama wa kutisha, wanaelezwa kutoka katika
mataifa ya Somalia, Uingereza, Marekani na Syria.
Taarifa hizi zinathibitishwa na kauli
iliyotolewa juzi na Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, Amina Mohamed
ambaye katika mahojiano yake na Kituo cha Televisheni cha Al-Jazeera,
alisema kuwa Al-Shabab hawakuwa peke yao katika shambulio hilo.
Mohamed aliiambia Al - Jazeera kuwa al-Qaeda ndio waliokuwa nyuma ya tukio hilo na si Al-Shabab.
"Al-Shabab hawafanyi peke yao, hili shambulio ni sehemu ya kampeni ya ugaidi wa kimataifa," alisema Mohamed.
Waziri huyo alisema zaidi ya magaidi
20 wakiwemo wanawake, walikuwa nyuma ya shambulio hilo na kwamba watu
hao wametoka katika mataifa tofauti tofauti duniani.
"Al-Shabab wanataka kujionyesha kwenye
ngazi ya kimataifa, hasa baada ya kubadili uongozi na wanataka
kuionyesha dunia kwamba wana nguvu bado, hivyo kuwekwa kwenye kundi la
kulifikiria," alisema.
Katika mahojiano yake mengine na kituo
cha cha PBS cha nchini Marekani, Waziri Mohamed alisema washambuliaji
kama wawili au watatu wamebainika kuwa ni raia wa Marekani na Mwingereza
mmoja.
Ni kutokana na taarifa hizo, baadhi ya wachambuzi wanasema kuwa shambulio hilo la kigaidi lina ajenda zaidi ya Kenya.
Zipo hisia kwamba shambulio hilo
halikuwa na lengo la kuiumiza Kenya pekee, kutokana na hatua yake ya
kupeleka majeshi yake kwenda kupambana na kundi la kigaidi la Al-Shabab
nchini Somalia, bali pia kumuumiza Rais wa Marekani, Barack Obama,
ambaye kwa asili anatoka nchini humo.
Obama ambaye nchi yake imekuwa
ikiongoza mapambano dhidi ya makundi ya kigaidi ikiwamo lile la
Al-Qaeda, ambapo hivi karibuni ilifanikiwa kumuua kiongozi wake, Osama
bin Laden, baba yake ni raia wa Kenya.
Baadhi ya wachambuzi wanasema kuwa,
kitendo cha magaidi kuamua kukishambulia kituo hicho cha biashara cha
Westgate, kinatokana pia na ukweli kuwa watu wengi wanaopenda kutembelea
hapo ni raia kutoka mataifa ya Magharibi wakiwemo Wamarekani, hivyo
ulikuwa ni mkakati wa kumuumiza Obama kwa njia hiyo.
Katika hotuba yake aliyoitoa siku ya
Jumatatu, Rais wa Somalia, Hassan Sheikh Mohamud, alilielezea kundi la
Al-Shabab kuwa ni tishio jipya kwa dunia. Chanzo: mtanzania
No comments:
Post a Comment