MWENYEKITI wa Yanga SC, Alhaj Yussuf Mehboob Manji amewaambia wachezaji wa timu hiyo kwamba hana matatizo nao kwa matokeo ya awali ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara na amewataka waelekeze nguvu zao katika mechi zijazo.
Yanga imeambulia pointi sita
katika mechi tano za awali za Ligi Kuu ya Vodacom, kutokana na sare
tatu, kushinda moja na kufungwa moja, hivyo kuachwa kwa pointi tano
kileleni na wapinzani wao wa jadi, Simba SC.
Jana Manji alikutana kwa chakula
cha jioni na wachezaji wa timu hiyo katika hoteli ya Serena, Dar es
Salaam akiwa ameambatana na Makamu wake Mwenyekiti, Clement Sanga,
Mjumbe wa Kamati ya Utendaji, Isaac Chanji na Mjumbe wa Sekretarieti,
Patrick Naggi.
Katika kikao hicho, Manji aliwaambia
wachezaji wa Yanga hamlaumu yeyote kwa matokeo hayo, kwani ligi bado
mbichi, ila akawataka waunganishe nguvu zao kuelekea mechi zijazo, ili
kurejesha ushindi na furaha klabuni.
Pamoja na hilo, Manji alizungumzia suala la madai ya baadhi ya
Pamoja na hilo, Manji alizungumzia suala la madai ya baadhi ya
wachezaji ya fedha za usajili na
akaliweka sawa kwa wale ambao walikuwa wanadai kuwawekea utaratibu wa
malipo haraka, jambo ambalo Naggi ametakiwa kuhakikisha analishughulikia
mara moja.
Aidha, Manji baada ya kikao cha pamoja na wachezaji wote, alimvuta pembeni Mrisho Ngassa kujadiliana naye faragha.
Haikujulikana mara moja Manji
alizungumza nini na Ngassa, lakini inaweza kuwa kuhusu deni analotakiwa
kuilipa Simba SC, Sh. Milioni 45 kwa kosa la kusaini Mikataba na timu
mbili. Ngassa alifungiwa mechi sita za mashindano na kutakiwa kurejesha
fedha alizochukua Simba SC Sh. Milioni 30 pamoja na fidia ya Sh Milioni
15.
Habari za ndani zinasema, Yanga SC
inaweza kulipa deni hilo ili Ngassa aanze kucheza, lakini italazimika
kurejeshewa fedha hizo na mchezaji mwenyewe, kwa kuwa klabu
ilikwishamalizana naye katika usajili wake.
Kuna uwezekano deni hilo
likatumika kumuongezea Mkataba Ngassa Yanga SC kutoka wa miaka miwili
aliosaini sasa. Ngassa mwenyewe hakupatikana alipotafutwa leo
kuzungumzia suala hilo.
Yanga SC itamenyana na Ruvu
Shootings Jumamosi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mfululizo wa
ligi hiyo, wakati leo Rhino Rangers wanaikaribisha Ashanti United
Mwinyi, Tabora.
Mechi nyingine zitapigwa Jumapili,
Simba SC ikishuka dimbani Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kumenyana na
JKT Ruvu, Rhino Rangers na Kagera Sugar Uwanja wa Ally Hassan Mwinyi,
Tabora, Mbeya City na Coastal Union Sokoine, Mbeya, Mgambo JKT na JKT
Oljoro Mkwakwani, Tanga na Ashanti United na Mtibwa Sugar, Azam Complex,
Chamazi, Dar es Salaam. Chanzo: binzubeiry
No comments:
Post a Comment