Thursday, September 26, 2013

BABU WA LOLIONDO AINENEA MAZITO TANZANIA.....AMWELEZA PINDA MAMBO ALIYOOTESHWA NA MUNGU

 
MCHUNGAJI Ambilikile Mwaisapila wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) amesema Mungu ameendelea kujifunua kwake na kumuonyesha kuwa Tanzania itakuwa kioo cha Afrika na baadaye kioo cha dunia.

Ametoa kauli hiyo Jumanne, Septemba 24, 2013 mbele ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda wakati akizungumza na wakazi wa kijiji cha Samunge, wilayani Ngorongoro mkoani Arusha wakati msafara wa Waziri Mkuu uliposimama nyumbani kwake ili kumsalimia akiwa njiani kurejea mjini Arusha. 
Mchungaji Mstaafu Mwaisapila maarufu kama Babu wa Samunge alisema kuna mambo mengi ambayo yameandikwa kwenye Biblia lakini hayakutokea Israeli na sasa yatafanyika hapa Samunge. “Mungu ametupenda sana, yanakuja mambo makubwa na wala hayako mbali. Kama mimi ni mzee na nitayaona, kwa hiyo mtarajie kuwa hayako mbali kutokea,” alisema huku akishangiliwa. 

Alisema katika mafunuo aliyopewa na Mungu ameonyeshwa kwamba watu wengi zaidi watafurika kijijini Samunge kuliko ilivyokuwa hapo awali. Alitumia fursa hiyo kuishukuru Serikali kwa misaada iliyotoa wakati wa ‘kugawa kikombe’ ikiwemo mahema, maji na ulinzi.

Waziri Mkuu ambaye yuko mkoani Arusha kwa ziara maalum ya kusikiliza matatizo ya ardhi yanayowakabili wakazi wa wilaya ya Ngorongoro, katika tarafa za Ngorongoro, Loliondo na Sale alisema anakubaliana na utabiri wa Mch. Mwaisapila kwani Tanzania imejaliwa gesi nyingi na mafuta mengi ambavyo vitabadili sura ya Taifa hili.

“Mungu ametupa gesi nyingi sana, katika miaka miwili tutakuwa na umeme kila mahali. Tuna makaa ya mawe ambayo ni nishati kubwa na sasa tuna fursa ya kupata nishati ya umeme kutoka ardhini (geo-thermal) katika Ziwa Natron,” alisema.

Alisema Tanzania imekuwa kimbilio la kila mwekezaji na sababu kubwa ni amani na utulivu uliopo nchini.

Aliwaeleza wakazi wa Samunge kwamba mapema mwakani mkandarasi wa barabara atakuwa katika eneo lao kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya lami ambapo awamu ya kwanza itaanzia Wasso hadi Mto wa Mbu kupitia Samunge.

Akitoa ombi maalum kwa niaba ya vijana mbele ya Waziri Mkuu, Bw. Elias Kalumbwa alisema wanaomba kuchimbiwa bwawa ili waweze kujiajiri kupitia kilimo cha mbogamboga na matunda.

Bw. Kalumbwa ambaye amesomea masuala ya wanyamapori alisema eneo la kuchimba bwawa lipo katika mto wa msimu unaopita kijijini hapo. “Eneo la kuchimba bwawa lipo katika mto wetu, vijana tunaweza kujiajiri endapo tutapata bwawa ili tufanye kilimo cha umwagiliaji maji,” alisema huku akishangiliwa.

Naye Bibi Martha Sereri (70) alimweleza Waziri Mkuu kwamba wanaomba jimbo la Ngorongoro ligawanywe kwa sababu ni kubwa sana kiasi kwamba inamuwia vigumu mbunge wao kufika maeneo yote. Aliomba pia wapatiwe walimu wa sayansi na hisabati kwa ajili ya shule 10 za sekondari zilizopo kwenye tarafa yao.

Aliomba wapatiwe mikopo ya matreka ili waweze kuongeza ukubwa wa mashamba yao. “Tunaomba mikopo ya matrekta na plau, haya mashamba umeyaona njiani yamelimwa na Wakenya. Ukikodisha trekta kila ekari unatozwa sh. 100,000/-. Je tutafika wapi? Mkitukopesha matrekta mtakuwa mmetusaidia zaidi,” alisema.

Akijibu hoja hizo, Waziri Mkuu alisema hoja zao ni za msingi na kwamba suala la vijana kupatiwa bwawa ni jambo linalowezekana kupitia mipangpo ya maendeleo ya kilimo ya wilaya (DADPS).

Andaeni andiko lenu, inabidi litoke kwa wananchi na siyo Serikalini. Mkituletea ni jambo linalowezekana kwani liko ndani ya mipango ya wilaya.

Akijibu hoja kuhusu ukubwa wa jimbo, Waziri Mkuu aliwaambia wakazi hao kwamba inawezekana kuongeza jimbo isiwe suluhisho la matatizo yao kwa sababu ya jiografia ya eneo lao.

Kuongeza jimbo inaweza isiwe jibu la kila kitu kwani matatizo mnayopata yanatokana na jiografia ya eneo lenu, kutoka Ngorongoro, Loliondo hadi huku Sale. Mimi nadhani tuangalie pia uwezekano wa kuwapa Halmashauri ili kusogeza huduma kwa wananchi. Tutaangalia njia zote mbili na kuona ipi italeta majibu ya haraka kwenu,” alisema.

No comments:

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...