WASIWASI umeibuka miongoni mwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam, kuhusu uwepo wa makamanda wa wapiganaji wa kikundi cha waasi wa M23, ambao wamejipenyeza nchini kwa kivuli cha kuendesha shughuli za kihoro katika baadhi ya makanisa.
Duru za uchunguzi zimeonyesha kuwa
baadhi ya watu walioingia nchini kwa mwamvuli wa uchungaji wakitokea
nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, majina yao yamo kwenye orodha
ya wapiganaji wa kikundi hicho cha waasi.
Taarifa mbalimbali zilizokusanywa na
gazeti hili zimeonyesha kuwa, raia hao wa Kongo mbali na kufanya kazi za
kiroho, pia wanajihusisha na shughuli mbalimbali za kijamii pamoja na
kufanya biashara ndogo ndogo.
Baadhi ya wachungaji waliozungumza Jumatano kuhusu suala hilo, walishindwa kukubali au kukanusha kuhusu taarifa hizo.
Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la
Mikocheni B, Assemblies of God, Getrude Lwakatare, ambaye pia ni Mbunge
wa Viti Maalum Mkoa wa Morogoro (CCM), alipoulizwa kupitia simu yake ya
kiganjani iwapo anazo fununu za uwepo watu wa aina hiyo ambao kwa kiasi
kikubwa wameanza kujenga taswira mbaya katika baadhi ya makanisa, alikaa
kimya kwa muda kisha akakata simu.
Alipopigiwa tena na tena hakupokea na hata alipotumiwa ujumbe mfupi kuulizwa jambo hilo hakujibu.
Afisa Uhamiaji wa Mkoa wa Dar es
Salaam, Grace Hokororo, yeye alipoulizwa kuhusu kuibuka kwa hofu hiyo na
iwapo idara yake imekwishapata taarifa hizo alisema hazijamfikia.
"Taratibu za kupokea wageni kweli
zinafahamika, lakini mpaka sasa hatujapata taarifa za uwepo wa watu wa
aina hiyo. Lakini kama kweli wapo nchini, tunaomba tupatiwe taarifa
kamili, wanasali wapi, lini na saa ngapi ili tufanye kazi yetu,"
alisema.
Aidha, Kamanda wa Polisi, Kanda
Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, alipotafutwa kuzungumzia
taarifa hiyo naye alisema hana taarifa hizo.
Kamanda Kova alisema jambo hilo
linaweza kuwa kweli, kutokana na mwingiliano mkubwa uliopo sasa wa raia
wa kigeni nchini na alitoa wito wa kupatiwa taarifa za uhakika ili
ziweze kufanyiwa kazi.
"Hilo suala ni la hatari sana na
linatisha, naomba uzidi kunipa taarifa kwa kina ili tuanze kuchukua
hatua za haraka, sikatai jambo hilo kuwepo kwa sababu ya mwingiliano
uliopo sasa, lakini nawaomba wananchi kama walivyovuja taarifa kwenu,
kwa sababu najua ninyi mko karibu sana na jamii, basi watusaidie na sisi
hivyo hivyo tufanye kazi yetu," alisema Kova.
Kwa muda sasa, taarifa za kuwepo kwa
watu wanaohofiwa kuwa wapiganaji wa kikundi cha waasi wa M23,
waliojificha katika baadhi ya nyumba za ibada, zimezagaa jijini Dar es
Salaam na baadhi ya makanisa ambayo wanaabudu yamekuwa yakitajwa.
Waasi wa kikundi cha M23, wanapigana vita na vikosi vya majeshi ya Serikali ya Kongo yanayosaidiwa na jeshi la Umoja wa Mataifa na hivi karibuni, ngome yao kuu ilisambaratishwa. Chanzo: Mtanzania
Waasi wa kikundi cha M23, wanapigana vita na vikosi vya majeshi ya Serikali ya Kongo yanayosaidiwa na jeshi la Umoja wa Mataifa na hivi karibuni, ngome yao kuu ilisambaratishwa. Chanzo: Mtanzania
No comments:
Post a Comment