KIINGILIO MECHI YA STARS, MOROCCO 5,000/-
Kiingilio cha chini katika mechi ya mchujo
ya Kombe la Dunia kati ya Tanzania (Taifa Stars) na Morocco (Lions of
the Atlas) itakayochezwa Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam
ni sh. 5,000 kwa viti vya rangi ya kijani.
Viti
vya kijani katika uwanja huo wenye uwezo wa kumeza watazamaji 60,000
viko 19,648. Kwa upande wa viti vya rangi ya bluu ambavyo viko 17,045 ni
sh. 7,000. Kiingilio kwa viti vya rangi ya chungwa ambavyo viko 11,897
ni sh. 10,000.
Viingilio
vya daraja la juu ni kama ifuatavyo; VIP C yenye watazamaji 4,060 ni
sh. 15,000 wakati sh. 20,000 ni kwa VIP B yenye watazamaji 4,160. VIP A
yenye watazamaji 748 kiingilio chake ni sh. 30,000.
Tiketi
kwa ajili ya mechi hiyo itakayoanza saa 9 kamili alasiri zitaanza
kuuzwa siku mbili ya mchezo (Ijumaa na Jumamosi) katika vituo
vifuatavyo; Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, Sokoni Kariakoo, mgahawa
wa Steers ulioko mtaa wa Ohio/Samora, Oilcom Ubungo, Kituo cha Mafuta
Buguruni na Dar Live Mbagala.
Katika
vituo hivyo tiketi zitauzwa katika magari maalumu. Magari hayo pia
yatafanya mauzo ya tiketi uwanjani siku ya mechi. Vilevile tunapenda
kuwakumbusha watazamaji kutonunua tiketi mikononi mwa watu au katika
maeneo yasiyohusika ili kuepuka kununua tiketi bandia, hivyo kukosa
fursa ya kushuhudia mechi hiyo.
SAMATA, ULIMWENGU WARIPOTI STARS
Washambuliaji
wa Taifa Stars, Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu wanaochezea timu ya
TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) wamewasili nchini
jana usiku na kwenda moja kwa moja kambini.
Ujio
wa washambuliaji hao unafanya idadi ya wachezaji walioripoti kambini
kufikia 20 kati ya 23 walioitwaa baada ya mshambuliaji Khamis Mcha
aliyekuwa na kikosi cha timu yake ya Azam nchini Liberia naye kuripoti
kambini leo asubuhi.
Wachezaji
John Bocco na makipa Mwadini Ally na Aishi Manula ambao pia nao
walikuwa Liberia na timu yao ya Azam wataripoti kambini leo alasiri.
Wachezaji hao ni sehemu ya msafara wa timu ya Azam ambao utakuja na
ndege ya mchana kutokea Nairobi kwa vile ile ya asubuhi waliyotangulia
nayo wenzao kuwa imejaa.
No comments:
Post a Comment