Kwa ufupi
Mahakama ya
Afrika inayoshughulikia haki za binadamu yenye makao yake jijini Arusha
imeamuru Serikali ya Libya kuendesha kesi inayomkabili mtoto wa
kiongozi wa zamani wa Libya, Muammar Gadaffi kwa uhuru na haki.
Saif
al-Islam Gaddafi, ambaye ni mtoto wa pili wa Gadaffi amekuwa
akishikiliwa na vyombo vya usalama vya Libya tangu Novemba 19, 2011
baada ya kukamatwa wakati akijaribu kukimbia nchi hiyo baada ya kuuawa
kwa baba yake na kaka yake, Mtassim Gaddafi, Oktoba 20, 2011.
Tume ya
Haki za Binadamu ya Afrika yenye makao makuu mjini Addis Ababa, Ethiopia
ndiyo iliyowasilisha shauri hilo kwenye Mahakama ya Afrika kwa kuwa
Serikali ya Libya haijaridhia mikataba ya kimataifa kuhusu haki za
binadamu.
Kutokana na hali hiyo, hata familia ya Gadaffi ilishindwa kufungua
kesi hiyo kwani taasisi au watu binafsi wa Libya hawana uwezo wa
kisheria wa kufungua kesi kwenye mahakama hiyo kutokana na kikwazo cha
Serikali yao.
Shauri hilo lenye namba 002/2012 lilisikilizwa na majaji kumi na moja
walioongozwa na Rais wa Mahakama hiyo, Jaji Sophia Akuffo kutoka Ghana,
Ijumaa iliyopita.
Wengine waliokuwemo kwenye jopo hilo ni pamoja na Makamu wake, Jaji
Fatsah Ouguergouz, Jaji Mkuu wa zamani, Augustine Ramadhan pamoja na
Majaji Sylvain Ore, Duncan Tambala, Gerald Niyugeko, Bernard Ngoepe,
Elsie Thompson, Hadji Guisse, Kimelabalou Aba na Ben Kioko.
Jopo hilo la majaji pia limeiamuru Serikali ya Libya kuruhusu ndugu,
jamaa na marafiki wa mtuhumiwa huyo kumtembelea kipindi chote shauri
dhidi yake linaposikilizwa.
Serikali ya Libya imetakiwa kutoa taarifa mahakamani kuhusu
utekelezaji wa amri hiyo siku 15 tangu kupokelewa kwa nakala ya hukumu.
Familia ya Gadaffi imekuwa haifurahishwi na mwenendo wa kesi ya Saif huko Libya.
No comments:
Post a Comment