Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora inayosikiliza kesi ya
kupinga matokeo ya uchaguzi wa Jimbo la Kigoma Kusini iliyofunguliwa na
aliyekuwa mgombea kupitia Chama cha NCCR-Mageuzi, David Kafulila
inatarajia kutoa hukumu Mei 17, mwaka huu.
Jaji wa mahakama hiyo anayesikiliza kesi hiyo mjini Kigoma, Ferdinand
Wambali, alisema kuwa amepanga kutoa hukumu tarehe hiyo baada ya pande
zote mbili kuwasilisha ushahidi na maelezo yao.
Baada ya kukamilika kwa ushahidi huo, Jaji Wambari aliomba kupatiwa
muda wa kutosha kupitia ushahidi na vielelezo vilivyowasilishwa
mahakamani hapo ili aweze kutoa hukumu ya haki.
Aliyekuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Uvinza, Ruben Mfune ambaye
alikuwa msimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo ni mshtakiwa wa tatu katika
kesi hiyo. Katika kesi hiyo namba 2 ya mwaka 2015, Kafulila anaishawishi
mahakama itengue matokeo yaliyompa ushindi aliyekuwa mgombea wa CCM,
Hasna Mwilima badala yake imtangaze yeye kama mshindi halali wa jimbo
hilo.
Walalamikiwa katika kesi hiyo ni pamoja na Mbunge wa jimbo hilo
Hasna, aliyekuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Uvinza, Ruben Mfune ambaye
alikuwa msimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo na Mwanasheria wa Serikali
ambaye anaiwakilisha Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Katika kesi hiyo, Wakili Kenedy Fungamtama anamtetea Husna huku
Kafulila akitetewa na mawakili watatu, Profesa Abdallah Safari, Tundu
Lissu na Daniel Rumenyela.
No comments:
Post a Comment