Yanga imeendelea kutoa
dozi Ligi Kuu Bara baada ya kuichapa 2-1 JKT Ruvu katika mechi
iliyochezwa jana kwenye Uwanja wa Taifa huku Mtibwa Sugar ikiichapa
Mgambo Shooting 1-0 kwenye Uwanja wa Manungu, Morogoro na kujikita
kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo.
Hii ni mechi ya pili kwa Yanga kushinda katika
Ligi Kuu kwani iliichapa Tanzania Prisons 2-1, lakini katika mechi yake
ya ufunguzi wa msimu huu ilichapwa 2-0 na Mtibwa hivyo kuanza safari
yake ya kusogea katika nafasi za juu katika msimamo wa ligi kwa mwendo
mdogo mdogo.
Katika mechi ya jana, hadi mapumziko Yanga ilikuwa
ikiongoza kwa bao 1-0 ambalo lilifungwa kwa shuti kali na beki Kelvin
Yondani dakika ya 35 akiunganisha pasi safi ya Haruna Niyonzima.
Bao la pili la Yanga lilifungwa na Niyonzima kwa
mpira wa faulo uliokwenda moja kwa moja nyavuni dakika ya 73 huku bao la
JKT Ruvu likifungwa dakika ya 90 kwa shuti kali na Jabir Aziz akiwa nje
ya 18. Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya neno Jambo Tz
Baada ya kupata bao la kwanza, Yanga iliongeza kasi huku ikimiliki zaidi mpira, lakini ilishindwa kutengeneza pasi za mabao.
Hata, hivyo katika kipindi cha kwanza JKT Ruvu
inayoundwa na wachezaji wanaoifahamu Yanga kama Jackson Chove, Jabir
Aziz, Idd Mbaga na Reliant Rusajo itabidi ijilaumu kwa kushindwa kutumia
vizuri nafasi ilizopata.
Kipindi cha pili, JKT ilifanya mabadiliko kwa
kuwatoa Lusajo na Gido Simon na nafasi zao kuchukuliwa na Ally Bilali na
Amos Edward, mabadiliko ambayo yaliisaidia kupeleka mashambulizi katika
lango la Yanga.
Yanga yenyewe kipindi cha pili ilicheza taratibu
huku ikitengeneza mashambulizi ya kushtukiza, pia ilifanya mabadiliko
kwa kuwatoa Edward Manyama na Andrey Coutinho na nafasi zao kuchukuliwa
na Salum Telela na Mrisho Ngasa. Mabadiliko hayo yaliisaidia Yanga kwani
dakika ya 73 walipata bao la pili ambalo lilifungwa na Niyonzima kwa
mpira wa faulo nje kidogo ya 18. Yanga ilipata faulo hiyo baada ya
Hassan Dilunga kuchezewa rafu na Mohamed Faki.
Baada ya kufungwa bao hilo, JKT Ruvu ilifanya tena
mabadiliko kwa kumtoa Mbaga na nafasi yake kuchukuliwa na Najim Maguli,
pia Yanga ilimtoa Niyonzima na kumuingiza Nizar Khalfan.
Katika mechi hiyo, JKT Ruvu ilipata bao la kufutia machozi dakika ya 90 ambalo lilifungwa kwa shuti kali na Jabir Aziz.
Akizungumza baada ya mechi kumalizika kocha wa
Yanga, Marcio Maximo alisema,”Timu yoyote ikicheza na Yanga inakaba sana
na ndivyo ilivyokuwa kwa JKT Ruvu, lakini tulicheza vizuri kipindi cha
pili, ligi ni ngumu.”
Kocha wa JKT Ruvu, Fred Minziro alisema,”Mechi ilikuwa ngumu, tatizo bahati haikuwa yetu ila tulicheza vizuri.”
Katika mechi nyingine iliyochezwa jana kwenye
Uwanja wa Manungu, Morogoro, Mtibwa Sugar iliichapa 1-0 bao lilikufungwa
na Ally Shomari katika kipindi cha kwanza. Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya neno Jambo Tz
No comments:
Post a Comment