Mbunge wa Kahama, James
Lembeli amemtuhumu Katibu Mkuu wa zamani wa CCM, Yusuph Makamba kwamba
alikuwa nyuma ya mpango mahususi wa kumhujumu ili akose ubunge katika
Uchaguzi Mkuu wa 2010.
Lembeli, mmoja wa wabunge walio mstari wa mbele
katika vita dhidi ya ufisadi, alisema mpango huo ulitekelezwa kwa
kueneza taarifa za kuanzisha jimbo la Ushetu ambalo alitakiwa agombee
badala ya Kahama, lakini baadaye msamaria mwema alimpa taarifa kwamba
jimbo hilo ni halipo.
Lembeli katika mahojiano yake maalumu na gazeti
hili mjini Dodoma alisema alipewa taarifa hizo saa chache kabla ya muda
wa mwisho wa kurudisha fomu za kugombea ubunge na kwamba tukio hilo
lilimfanya afute fomu yake ya kugombea mara mbili.
“Ulikuwa ni uhuni na ufisadi wa hali ya juu
kisiasa,” alisema mwanahabari huyo wa zamani katika mahojiano hayo
maalumu yaliyofanyika mjini Dodoma mapema wiki iliyopita. Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya neno Jambo Tz
Alisema mara ya kwanza alijaza kwamba anagombea
Jimbo la Kahama lakini alifuta na kuandika jimbo la Ushetu baada ya
kupewa taarifa za kuanzishwa kwa jimbo hilo na baadaye alifuta Ushetu na
kuandika tena Kahama baada ya kugundua kuwa ulikuwa mchezo mchafu.
“Baada ya kuruka viunzi, viongozi waandamizi wa
CCM wa Shinyanga, akiwamo Mwenyekiti wa Mkoa, Hamisi Mgeja walisusa
kunifanyia kampeni,” aliongeza Lembeli ambaye aliibuka na ushindi wa
asilimia 54.5 kati ya kura zilizopigwa.
Alisema mpango huo wa kumhujumu ulianza mapema
pale baadhi ya viongozi walipokuwa wakieneza kwamba yeye (Lembeli)
hatakiwi na kwamba ukweli siyo kwamba alikuwa hatakiwi na wananchi bali
baadhi ya viongozi.
Hata hivyo, Makamba alipoulizwa alisema ni uzushi
kwa kuwa kazi ya kugawa majimbo ni ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi, CCM
kazi yake ni kusimamisha tu wagombea.
“Niacheni nipumzike niendelee kula pensheni yangu.
Sasa niko Bumbuli natoka kuswali na ninakwenda kula Iddi, niacheni
nipumzike jamani, kama kuna maswali zaidi aulizwe katibu mkuu wa sasa,”
alisema Makamba.
Hata hivyo, Lembeni katika mahojiano hayo
alisisitiza: “Ninachodhani walikaa chini na mambo haya yalifanyika Dar
es Salaam na mbaya zaidi katika ofisi ya Makao Makuu ya CCM kwa sababu
ndio walioleta taarifa.”
Kwa mujibu wa Lembeli, taarifa kwamba kuna jimbo jipya la Ushetu
ambako ndiko alikozaliwa, zilimfikia yeye na wagombea wenzake saa 9:30
wakati mwisho wa kurudisha fomu ilikuwa saa 10:00 jioni.
“Wagombea wote tulikuwa tumesharejesha fomu ya
kugombea Jimbo la Kahama. Ilipoletwa hiyo taarifa, Katibu wa CCM wa
wilaya ya Kahama akawapigia simu wagombea wote kuwa anatuita ofisini,”
alisema mtangazaji huyo wa zamani wa Shirika la Utangazaji la Ujerumani,
Deutche Welle na kuongeza:
“Tulipofika pale akatuambia kuna habari mpya
kwamba kuna jimbo jipya la Ushetu, kwa hiyo hapa yako majimbo mawili
kuna Jimbo la Kahama na kuna jimbo la Ushetu.”
Pia, mwandishi huyo wa zamani wa gazeti la
Kiongozi alisema katibu huyo aliwaambia kuwa maelekezo aliyopewa kutoka
makao makuu ya CCM ni kuwataka kila mmoja afanye uamuzi papo hapo kama
anagombea Kahama au Ushetu.
Lembeli alidai baada ya kuelezwa hivyo, alihoji sana ili kupata ukweli kama jimbo hilo jipya limetangazwa na CCM au NEC.
“Yule katibu akapiga simu kwa mzee (katibu mkuu wa
CCM wa wakati huo, Yusuf Makamba) akawa ameacha sauti tusikie.
Akamwambia ‘mzee hapa wagombea wanahoji maswali mengi’,” alisema
Lembeli.
“Makamba akauliza nani huyo, akaambiwa ni Lembeli,
akasema ‘huyo kijana ni mkorofi sana, mbishi sana huyo, kama hataki
aache’. Nikachukua fomu nikafuta Kahama nikaandika Ushetu.”
Lembeli alisema mpango uliokuwapo ni kumfanya
(yeye) achukue fomu ya jimbo ambalo halipo na atakapokuja kushtuka, muda
wa kurudisha fomu na kampeni uwe umeshakwisha.
“Wakati ule mtandao wa simu ulikuwa haujasambaa
kwenye jimbo zima. Muda wa mimi kufanya mashauriano kule kijijini
haukuwapo na Ushetu ni eneo ambalo nilizaliwa,” alisema.
“Nafsi ikaniambia nikigombea huku mjini bila kuwa
nimewaarifu kule nitakuwa nimewavunjia heshima kwa hiyo nikaamua iwe
Ushetu. Sasa tukawaambia leteni fomu mpya tujaze wakasema ‘futa hapo
kwenye Kahama andika Ushetu’. Nikafuta nikaandika Ushetu.”
Lembeli (58) alidai baada tu ya kufanya uamuzi
huo, Mgeja ambaye wakati huo alikuwa Dar es Salaam kwenye ofisi ya makao
makuu ya chama, akamtuma mke wake kuja kuchukua fomu za Jimbo la
Kahama.
Kwa mujibu wa Lembeli, siku iliyofuata walianza
kampeni kwa ajili ya kura za maoni ndani ya chama wakati huo wakiwa
wanaamini kuna jimbo jipya la Ushetu limetangazwa na Nec.' Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya neno Jambo Tz
Aliyemwokoa
Lembeli alisema: “Namshukuru sana (mtangazaji wa
TBC jina tunalo). Yeye ndio aliniambia ‘Lembeli mbona nasikia sikia
jambo, huko kuna nini?”
Alisema baada ya kampeni nzito za siku nne na
walipokuwa wakiingia siku ya tano ya kampeni hizo ndani ya chama,
akahisi kuwa kuna mchezo mchafu unaendelea.
“Nilipiga simu Tume ya Uchaguzi kuulizia
nikaambiwa unasemaje, eti jimbo la Ushetu? Ushetu ndio mnyama gani.
Mzee, nilipata tumbo la kuharisha,” alisema Lembeli.
“Yaani nilipoulizwa tu Ushetu ni mnyama gani
nilipata tumbo la kuharisha nikajua tayari nimeshapoteza nafasi,”
alisema Lembeli katika mahojiano hayo.
“Siku ya tano ikaja simu kutoka CCM ya kutuita
wale tuliokuwa tunagombea Ushetu wakatuambia makao makuu walikuwa
wameghafilika kulikuwa hakuna jimbo linaitwa Ushetu.”
“Kwa hiyo nyie mlikuwa mnagombea Ushetu kama
mnataka kuendelea kugombea Jimbo la Kahama futeni hapo Ushetu weka
Kahama. Nikafuta Ushetu nikaweka Kahama na hapo hapo Mgeja akajitoa,”
alisema.
“Mimi naamini kulikuwa na mchezo kwa sababu
kulikuwa na haja gani ofisi kuu ya chama kusema kitu ambacho hakipo?
Hata baada ya kushinda kura ya maoni, bado vita ilihamia Dodoma,”
alisema.
Baada ya kutokea sakata hilo, Mkurugenzi wa
Uchaguzi wa wakati huo, Rajabu Kiravu alilazimika kutoa ufafanuzi kuwa
Tume ya Uchaguzi haikuwa imeanzisha jimbo jipya la Ushetu kama
ilivyokuwa imetangazwa awali na Katibu wa CCM wa Wilaya ya Kahama,
Sospeter Nyigoti ambaye ndiye aliyewaambia wagombea kuwa Ushetu ni jimbo
jipya.
Jina lake kupitishwa
Alisema katika majina yaliyochukua muda mrefu
kujadiliwa katika vikao vya chama vya uamuzi ya wagombea mjini Dodoma,
lilikuwa lake.
“Namshukuru sana Rais Jakaya Kikwete kwa sababu
ndiye aliyesimama kidete kutaka haki itendeke,” alisema Lembeli ambaye
pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira.
Lembeli alisema baada ya jina lake kupitishwa,
viongozi wakubwa ndani ya chama Mkoa wa Shinyanga hawakukanyaga kwenye
Jimbo la Kahama kumfanyia kampeni diwani, mbunge wala Rais.
“Viongozi waandamizi wa chama hawakugusa kabisa
kwenye kampeni kwenye jimbo langu. Kwa maana hiyo, mkoa haukumfanyia
kampeni Rais kwenye jimbo la Kahama,” alisema.
“Niliachwa peke yangu lakini walitaka kumuonyesha
mwenyekiti (Kikwete) siwezi ili kama nikishindwa, waseme ‘si unaona
tulikwambia kwamba huyu bwana hakubaliki’.”
Lembeli alisema pamoja na yeye kushinda kura ya
maoni kwa tofauti ya kura nne tu, lakini alipokwenda kwa wananchi
aliibuka na ushindi wa kishindo kwa kupata kura 32,531.
Wagombea wengine katika jimbo hilo walikuwa Dotto
Lubala wa Chadema aliyepata kura 20,912 na Hassan Makapa wa CUF
aliyeambulia kura 3,950. Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya neno Jambo Tz
Na Mwananchi
Na Mwananchi
No comments:
Post a Comment