Maandamano ya walimu
kuingia katika Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba kuadhimisha Siku ya Walimu
Duniani, jana yalipata mtafaruku baada ya polisi kuyaingilia na kuchana
bango mojawapo lililohoji posho za wajumbe wa Bunge la Katiba.
Bango hilo la kitambaa cheupe lilikuwa na
maandishi yanayohoji posho ya Sh300,000 waliyokuwa wanapata wajumbe wa
Bunge la Katiba, yakilinganishwa na kazi kubwa wanayofanya walimu.
Ujumbe wenyewe ulisomeka hivi: “Haki iko wapi
usawa uko wapi, posho ya mjumbe wa Bunge la Katiba kwa siku shilingi
laki tatu, mshahara wa mwalimu shilingi 370 kwa mwezi. No big results
without big salary (Hakuna matokeo makubwa bila mshahara mkubwa)”.
Ujumbe huo ulikuwa ukifanya rejea ya viwango vya
malipo ya Sh300,000 kwa siku ambazo walikuwa wakilipwa wajumbe wa Bunge
Maalumu zikiwa ni Sh230,000 kama posho ya kujikimu na Sh70,000 ambazo ni
posho ya vikao. Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya neno Jambo Tz
Hata hivyo bango hilo lilichanwa hatua chache
kabla ya walimu hao hawajaingia uwanjani humo, ambapo mgeni rasmi
alikuwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
Mwenyekiti wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT),
mkoani Kagera Dauda Bilikesi, alisema amesikia habari za bango hilo
kuharibiwa lakini akasema asingezungumza kwa kina kuhusu suala hilo kwa
kuwa hayo yamepita.
Waibuka na shairi
Muda mfupi baada ya polisi kuharibu bango hilo
lisionekane uwanjani, walimu hao walipiga chenga kiana wakaibuka na
ujumbe ule ule kwa njia ya shairi.
Kupitia shairi hilo liliposomwa mbele ya Pinda,
walimu walihoji ukubwa wa posho za wajumbe wa Bunge la Katiba
zikilinganishwa na mshahara wanaopata, hali iliyosababisha umati wa
walimu uliokuwa uwanjani hapo kulipuka kwa sauti kubwa za shangwe.
Shairi hilo lililosomwa na Mwalimu Betwel Magoso
kutoka Wilaya ya Biharamulo, lilisababisha kuvurugika kwa muda kwa
utaratibu uliopangwa kwa mujibu wa ratiba, pale alipohoji wajumbe wa
Bunge la Katiba kupata Sh1 milioni kwa siku tatu ambazo ni mkopo wa
mwalimu kwa miaka mitatu.
Mwalimu Magoso alimgusa Pinda ambaye kabla ya
kuanza hotuba yake alianza kwa kusema kuwa mwalimu huyo alitumia ujanja
kufikisha ujumbe wake na kuwa baadhi ya maneno katika shairi lake
yalikuwa ni mazito.
Kanuni za mafao zasitishwa
Katika hatua nyingine, Serikali imesitisha
matumizi ya kanuni mpya za ukokotoaji mafao ya pensheni ambao umeibua
malalamiko kuwa malipo ya mkupuo yalipunguzwa kutoka asilimia hamsini
hadi ishirini na tano.
Kanuni hizo ni zile zilizotungwa na Mamlaka ya
Udhibiti wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) na kutangazwa Agosti 6,
mwaka huu mjini Dodoma na Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudentia Kabaka.
Tangu kutangazwa kwake kanuni hizo zilizua
malalamiko kutoka kwa wadau mbalimbali hususan wafanyakazi ambao
walisema kuwa hayalengi kuboresha wala kuhuisha mafao, bali yanapunguza
stahili hiyo tofauti na ilivyokuwa mwanzo. Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya neno Jambo Tz
Akihutubia sherehe hizo, Pinda alisema suala hilo linarejeshwa tena serikalini kuangaliwa upya.
“Acha suala hili tulirejeshe serikalini
tukalitazame upya kwa sababu halikubaliki na hatuwezi kulishurutisha kwa
sababu nyie ndiyo wadau, siyo sisi. Tutawaambia walitazame tena na
warudi wawashirikishe vizuri wawaeleze mlikubali au mlikatae,” alisema
Pinda.
Waziri Mkuu alisema pamoja na kuwa lengo lilikuwa
ni kuboresha maisha ya wafanyakazi kwa kuleta mfumo mpya wa ukokotoaji
wa mafao ya pensheni, suala hilo lilihitaji ushirikishwaji mpana zaidi
ikiwa ni pamoja na wadau wenyewe.
Katika kuunga mkono kilio cha walimu, Pinda alitoa
mfano wa wabunge wanaopata mafao yao yote wanapomaliza kipindi cha
uwakilishi kwa miaka mitano na kuwa kabla ya hapo mafao hayo yalitolewa
baada ya kumaliza miaka kumi, jambo ambalo halikupendelewa na wabunge.
Kauli hiyo ilitokana na risala ya walimu
iliyosomwa na Katibu Mkuu wa CWT, Yahya Msulwa aliyesema mabadiliko hayo
yamezua manung’uniko makubwa hasa kwa walimu wanaobeba idadi kubwa ya
watumishi.
Alisema mfumo wa ukokotoaji wa mafao wa zamani,
pamoja na kuwa mishahara yao ni midogo, ulifanya mafao yao ya uzeeni
yawe na unafuu kwa kiwango fulani, ikilinganishwa na mfumo mpya ambao
ukokotoaji unafanyika kwa kuangalia wastani wa mishahara ya miaka mitatu
ya mwisho.
Kabla ya mapendekezo hayo, ukokotoaji wa mafao
ulifanyika kwa kuangalia mshahara wa mwisho wa mtumishi na malipo
yalitolewa kwa asilimia hamsini ya mafao yote baada ya ukokotoaji
kufanyika. Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya neno Jambo Tz
Na Mwananchi
Na Mwananchi
No comments:
Post a Comment