Wakuu wa Nchi Tano Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki
(EAC), leo Novemba 30, wanatarajiwa kutia saini mkataba wa kuwa na
sarafu moja.
Mkuu wa Idara ya Uhusiano na Mawasiliano wa EAC,
Richard Owora aliwaambia waandishi wa habari jijini hapa kuwa sherehe za
kutia saini mkataba huo utakaoanzisha mchakato wa miaka kumi hadi
kufikia lengo la kuwa na sarafu moja ya EAC, zitafanyika katika Viwanja
vya Kololo jijini Kampala.
Marais Jakaya Kikwete wa Tanzania, Yoweri Mseveni
wa Uganda, Paul Kagame wa Rwanda, Pierre Nkuruzinza wa Burundi na Uhuru
Kenyatta wa Kenya wanatarajiwa kuwa jijini hapa kuhudhuria mkutano wa
mwaka wa wakuu wa nchi za EAC.
Umoja wa sarafu ni moja kati ya mambo makuu manne
yaliyoainishwa katika mkataba wa EAC. Masuala mengine ni soko la pamoja
na umoja wa forodha ambayo tayari mikataba yake imesainiwa na kuanza
kutekelezwa, ingawa kwa kasi isiyotosheleza kutokana na vikwazo kadhaa.
Hatua ya mwisho na juu kabisa katika ushirikiano
wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ni shirikisho la kisiasa linalolenga kuwa
na nchi moja, hatua itakayozihakikishia nchi za ukanda huo nguvu ya
soko, biashara, majadiliano na uamuzi katika ngazi ya ndani na
kimataifa.
Huu ni mkutano wa kwanza kuwakutanisha wakuu wote
wa EAC tangu kuibuka kwa migongano ya kimawazo na mtazamo miongoni mwao
kuhusu utekelezaji wa makubaliano na miradi iliyo katika mipango ya EAC
pamoja na njia bora na sahihi ya kumaliza vita na migogoro ya wenyewe
kwa wenyewe ndani ya baadhi ya nchi wanachama.