Catherine Ashton Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja (kushoto) na Waziri wa mambo ya nje wa Iran Mohammad Javad Zarif wakiwa katika mkutano na waandishi wa habari mjini Geneva baada ya kushindwa kufikiwa kwa makubaliano. (10.11.2013).
Mazungumzo magumu yanaanza leo kati ya Iran na mataifa makubwa kutafuta makubaliano kwa mpango wa nyuklia wa Iran ambayo pia yatawaridhisha wanasiasa wa msimamo mkali huko Marekani, Israel na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Mazungumzo hayo yanafanyika Geneva wakati kukiwa na hali ya mvutano inayoongezeka Mashariki ya Kati ambapo waziri wa mambo ya nje wa Iran akiishutumu Israel kwa kujaribu kuvuruga mchakato huo kufuatia mirupuko miwili ya mabomu iliouwa takriban watu 23 nje ya ubalozi wa Iran mjini Beirut hapo jana.Wizara ya mambo ya nje ya Iran imeilaumu Israel na mamluki wake kwa kuhusika na miripuko hiyo.
Israel imekanusha madai hayo na Waziri
Mkuu wake Benjamin Netanyahu leo hii anatarajiwa kuendeleza kampeni
yake dhidi ya kufikia makubaliano ya nyuklia na Iran wakati
atakapokutana na Rais Vladimir Putin wa Urusi mjini Moscow.
Iran ina matumaini
Iran Waziri wa mambo ya nje wa Iran
Javad Zarif ameonekana kutokata tamaa kuhusu nafasi za kufikiwa kwa
makubaliano mjini Geneva ikiwa ni siku 10 baada ya mazungumzo kati ya
Iran kwa upande mmoja na kwa upande wa pili Marekani, China, Urusi,
Uingereza, Ufaransa na Ujerumani kushindwa kufikia
makubaliano.Amekaririwa akisema kwamba anadhani kuna kila uwezekano wa
mafanikio.
Lakini Rais Barack Obama wa Marekani
ambaye amekuwa akiwashawishi wabunge wa Marekani kutoiwekea vikwazo
zaidi Iran ameonekana kuwa na msimamo wa hadhari zaidi juu ya uwezekano
wa kufikiwa kwa makubaliano na mapema. amekaririwa akisema "Hatujuwi
iwapo tutaweza kufikia makubaliano na Iran wiki hii au wiki ijayo."
Wabunge wa Marekani hapo jana
wameitaka serikali ya Marekani iwe na msimamo mkali katika mazungumzo
yake na Iran kuhusu mpango wa nyuklia wa nchi hiyo.
Ofisi ya Waziri Mkuu wa Uingereza
David Cameron ilisema jana kwamba waziri mkuu huyo pia alizungumza kwa
simu na Rais Hassan Rouhani wa Iran ambayo yalikuwa ni mawasiliano ya
kwanza kati ya viongozi wa nchi hiyo katika kipindi cha muongo mzima na
viongozi hao wamekubali kwamba ni muhimu kuitumia fursa iliopo.
Vitisho na vikwazo vikomeshwe
Shirika la habari la serikali la Iran
IRNA limemkariri Rouhani akimwambia Cameron kwamba nchi hiyo imeazimia
kuhakikisha kwamba shughuli zake za nyuklia zinaendelea kwa ajili ya
matumizi ya amani na itatetea kwa nguvu haki zake za nyuklia. Ameongeza
kusema hawatokubali ubaguzi katika suala hilo na kwamba lugha ya heshima
lazima ichukuwe nafasi ya ile ya vitisho na vikwazo.
Mataifa makubwa yanataka kufikiwa kwa
makubaliano ya awamu ya kwanza ambapo kwayo Iran inatakiwa isitishe
sehemu ya shughuli zake nyeti kabisa za nyuklia wakati makubaliano ya
muda mrefu yakiandaliwa.Lakini suala ni iwapo Iran yenye kupigania
kuregezwa kwa vikwazo vya Umoja wa Mataifa,Marekani na Umoja wa Ulaya
ambavyo vimeathiri sana usafirishaji nje wa mafuta ya nchi hiyo
itakubali kile kinachopendekezwa badala yake.
Wataalamu wanasema iwapo haiba ya
uchangamfu anayoitumia Rais Rouhani kuwasiliana na mataifa ya magharibi
itashindwa kuupatia ufumbuzi mzozo wa nyuklia wa nchi hiyo atakuwa
katika hatari ya kuacha kuungwa mkono na kiongozi mkuu wa nchi hiyo Ali
Khamenei ambaye leo amesema mataifa ya magharibi lazima yaheshimu
mistari mekundu ya nchi hiyo na pia kuitaka serikali ya Iran kuheshimu
mistari hiyo na kutotiwa kiherehere na makelele ya maadui na wale
walioko dhidi ya Iran.
Mwandishi: Mohamed Dahman/AFP
No comments:
Post a Comment