Siku moja baada ya Kamati Kuu ya Chadema kumvua uongozi
aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu Taifa wa chama hicho, Zitto Kabwe, mama yake
mzazi, Shida Salum ametoa ya moyoni akieleza kuwa kilichomkuta mwanaye
kimefunika mabaya mengi yaliyopangwa afanyiwe.
“Kwa upande wangu naona kama ni ushindi kwa Zitto
kutokana na jinsi ninavyojua hali ilivyo, mambo yalikuwa ni mengi mno na
nikwambie tu, Zitto kuvuliwa uongozi kumefunika hayo yaliyokuwa
yamekusudiwa kufanywa dhidi yake. Nilikuwa naomba Mungu kila siku ili
afukuzwe Chadema,” alisema mama huyo wakati akizungumza na gazeti hili
nyumbani kwake Tabata, Dar es Salaam.
Shida Salum alisema kuwa Mungu amemnusuru mwanaye
na kusisitiza, “Watu walikaa na kutengeneza ripoti ya siri kuhusu Zitto
na kuiweka kwenye mtandao kisha kuituma kwa wanachama wa Chadema
wanaowafahamu.
Mpaka wanafikia hatua hiyo maana yake ni kwamba wamejaribu njia zote za kummaliza, lakini wameshindwa.”
Mpaka wanafikia hatua hiyo maana yake ni kwamba wamejaribu njia zote za kummaliza, lakini wameshindwa.”
Alisema kutokana na hali ilivyo hivi sasa
amemnyang’anya mwanaye kwa muda simu zake zote za mkononi, kompyuta
mpakato (Laptop) pamoja na iPad ili asiwasiliane na watu, kwa maelezo
kuwa wapo wenye nia mbaya wanaomsaka kumpa pole za kinafiki. “Kwa sasa
nataka mwanangu atulize akili.”
Shida Salum, mbali na kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya
Chadema, pia ni mwasisi wa Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu
(Shivyawata) na Mwenyekiti wa Chama cha Watu Wenye Ulemavu wa Viungo
(Chawata)
Zitto pamoja na Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama
hicho, Dk Kitila Mkumbo juzi walivuliwa uongozi kutokana na uamuzi wa
kikao cha Kamati Kuu kilichokutana kwa siku mbili, kuanzia Novemba 20
mwaka huu katika Ukumbi wa Blue Pearl jijini Dar es Salaam,
wakituhumiwa kukisaliti chama.
Mbali ya kuwavua uongozi Zitto, Dk Mkumbo pamoja
na aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho mkoani Arusha, Samson Mwigamba,
pia Kamati Kuu imewapa siku 14 wajieleze kwa nini wasifukuzwe uanachama.
Kwa uamuzi huo Zitto amebaki na wadhifa wa ubunge
wake wa Jimbo la Kigoma Kaskazini na Uenyekiti wa Kamati ya Bunge ya
Hesabu za Serikali (PAC).
Katika ufafanuzi wake wa jana, Shida aliwataka
wanachama wa Chadema kuwa watulivu kwa maelezo kuwa Zitto hajafukuzwa
uanachama, “Siku nyingi walikuwa wanamwinda na hata hilo jambo ambalo
Chadema wanasema amefanya, hawana uhakika nalo.”
Juzi wakati akisoma uamuzi wa Kamati Kuu,
mwanasheria wa Chadema, Tundu Lissu alisema wamebaini kuwapo kwa mkakati
mkubwa wa watu hao kutimiza malengo hayo ambao umeandikwa katika waraka
unaoitwa ‘Mkakati wa Mabadiliko 2013’, ambao umeandaliwa na kikundi
kinachojiita ‘Mtandao wa Ushindi’.
Alisema kikundi hicho vinara wake wapo wanne,
Zitto anajulikana kama Mhusika Mkuu (MM), Mkumbo (M1), Mwigamba (M3) na
mtu mwingine wa nne ambaye alieleza kuwa hajatambulika na anatumia jina
la M2.
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment