Monday, November 25, 2013

BALAA TENA SIMBA SC…BASI LAO LA YUTONG LAKAMATWA, KISA MADENI ...!!!

BASI_LA_SIMBA_85a15.jpg
Na Mahmoud Zubeiry, Dar es Salaam
BASI kubwa la klabu ya Simba aina ya Yutong, walilopewa na wadhamini wao, kampuni ya Bia Tanzania (TBL) linashikiliwa na kampuni ya MEM kutokana na deni la zaidi ya Sh. Milioni 40.
Basi hilo lenye thamani ya Sh. Milioni 200 linashikiliwa kwa siku ya pili sasa, linaweza kupigwa mnada baada ya siku 14, iwapo Simba SC itashindwa deni hilo.
Hali hiyo inatokea wakati klabu inakababiliwa na mgogoro mkubwa baina ya Wajumbe wa Kamati ya Utendaji na Mweyekiti wao, Alhaj Ismail Aden Rage, Mbunge.
Rage hakupokea simu alipopigiwa jioni hii ili kuzungumzia suala hilo na Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Evodius Mtawala simu yake haikupatikana kabisa.
Jumanne wiki hii Kamati ya Utendaji ya Simba SC ilitangaza kumsimamisha Rage katika kikao chake cha Jumatatu usiku kwa sababu anaendesha klabu kwa kufanya maamuzi yake mwenyewe bila kushirikisha kamati ikiwemo kutoitisha vikao vya kamati ya utendaji kwa mujibu wa Ibara ya 31 (a).
Kaimu Makamu Mwenyekiti wa Simba SC, Joseph Itang'are 'Kinesi' alisema sababu nyingine ni Rage kuahirisha mkutano Mkuu maalum wa katiba ulioidhinishwa na mkutano mkuu bila kuishirikisha kamati.




Aidha, sababu nyingine ni mkataba wa kukiuza kipindi cha Simba Tv bila kuishirikisha kamati hiyo kinyume na ibara ya 30 (b) ya ibara ya katiba ilihali kamati hiyo na Mwenyekiti akiwa na taarifa ilikuwa na mazungumzo na Zuku Tv, kuuza kipindi hicho ambapo maongezi yalikuwa yamefikia Dola za Marekani 300,000 kwa mwaka pamoja na fungu la usajili kila mwaka ambalo lilikuwa bado halijajadiliwa.
Hata hivyo, baadaye Baraza la Wadhamini la klabu hiyo, likasema halitambui uamuzi huo wa Kamati ya Utendaji na kumuandikia barua Kinesi aliyeendesha kikao hicho kumtaka awape muhtasari wa kikao na pia aeleze wajumbe waliohudhuria.
Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini la Simba, Hamisi Kilomoni, alisema ingawa Baraza lake bado halijajulishwa rasmi uamuzi wa kumsimamisha Rage, lakini wamekubaliana kwamba kuna makosa yalifanyika kwenye kikao hicho kulingana na katiba ya Simba, hivyo kutaka muhtasari huo kwa vile wao ndiyo wasimamizi wa masuala ya Simba.
Jana TFF imemtaka Rage aitishe Mkutano Mkuu wa Dharura wa klabu ndani ya siku 14 kuanzia jana, baada ya kubaini kuna mgogoro katika klabu kufuatia kupokea barua mbili; moja kutoka Kamati ya Utendaji ikielezea kumsimamisha uongozi Rage, na nyingine kutoka kwa Mwenyekiti huyo ikielezea kutotambua kusimamishwa huko.
Uamuzi wa TFF umefanywa kwa kuzingatia Ibara ya 1(6) ya Katiba ya Simba inayosema: "Simba Sports Club ni mwanachama wa TFF, itaheshimu Katiba, kanuni, maagizo na uamuzi wa TFF na FIFA, na kuhakikisha kuwa zinaheshimiwa na wanachama wake."
Na TFF imesema itatuma wawakilishi wake katika mkutano huo, na kumuagiza Mwenyekiti wa Simba kuhakikisha wanachama wote wenye hoja wanapata fursa ya kusikilizwa. Hata hivyo, leo Rage amezungumza na Waandishi wa Habari na kusema hawezi kuitisha Mkutano ndani ya siku 14 kama alivyoagizwa na TFF kwa madai atakuwa anakiuka katiba ya klabu yake.

No comments:

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...