********
Watanzania wawili wanahojiwa na Polisi wa Afrika Kusini baada ya kukamatwa jana na kilo 55 za dawa za kulevya.
Watu hao wawili wanatazamiwa kufikishwa mahakamani
kesho kujibu tuhuma za kukamatwa na dawa hizo zenye thamani ya Rand75
milioni (Sh11.7 bilioni).
Maofisa wa Kikosi Maalumu cha Kupambana na Makosa
ya Jinai na Rushwa cha Afrika Kusini (The Hawks), kiliwakamata watu hao
katika Kitongoji cha Kempton Park, Ekurhuleni, Jimbo la Gauteng.
Msemaji wa Hawks, Paul Ramaloko alisema jana kuwa
maofisa hao walivamia nyumba waliyokuwa wanaishi Watanzania hao na
kukuta mzigo huo.
Hata hivyo, alikataa kutaja majina ya watu hao kwa
kuhofia kuharibu uchunguzi akisema bado walikuwa wanawasaka watuhumiwa
zaidi wakiwamo raia wa Afrika Kusini.
Alisema kikosi chao kimepata mafanikio makubwa kwa
kukamata dawa nyingi kiasi hicho... “Tunakaribia kuwakamata vinara wa
biashara hiyo, maana tumeelezwa kuna kundi kubwa la watu wazito,”
alisema Ramaloko. Hii inakuwa mara ya pili katika kipindi cha miezi
minne kwa Watanzania kutuhumiwa kubeba dawa hizo.
Julai mwaka huu, wasanii wawili Agness Gerald
`Masogange’ na Melissa Edward walikamatwa kwenye Uwanja wa Ndege wa
Oliver Tambo, Johannesburg wakiwa na kilo 180 za kemikali aina ya
ephedrine zenye thamani ya Sh7 bilioni.
Baada ya kukaa miezi miwili jela, Masogange
alipatikana na hatia ya kuingiza kemikali hiyo, ambayo hutumika
kutengeneza dawa za kulevya na kutozwa faini ya Rand 15,000 (Sh2.3
milioni).
Melissa aliachiwa huru baada ya kuonekana hana hatia.
Wasafirishaji sasa watumia samaki
Katika hatua nyingine, wasafirishaji wa dawa za
kulevya inasemekana wamebuni mbinu mpya ya kutumia samaki kusafirisha
bidhaa hiyo haramu.
Akizungumza jana wakati wa uteketezaji wa dawa za
kulevya, Mkuu wa Kitengo cha Kudhibiti Dawa za Kulevya, Kamishna
Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), Godfrey Nzowa alisema wanatumia
samaki kwa kuwa wana harufu kali.
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment