Wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba wakitoka kwenye ukumbi wa Bunge mjini
Dodoma wakati wa mapumziko ya mchana. Picha na Emmanuel Herman.
Kamati za Bunge Maalumu
la Katiba zilizoanza vikao vyake juzi mjini Dodoma, zimejikuta
zikifanya kazi kwa kulipua kutokana na uchache wa muda uliotengwa,
ikilinganishwa na ukubwa wa kazi ya uchambuzi wa ibara za rasimu ya
Katiba hiyo.
Kamati hizo zimetengewa siku 14 kwa ajili ya
kujadili na kuchambua sura 15 za rasimu hiyo na siku mbili za kuandaa
taarifa ambazo zitaanza kuwasilishwa kwenye Bunge Maalumu, Septemba 2,
mwaka huu.
Hata hivyo, baadhi ya wajumbe wamekuwa
wakilalamikia ufinyu wa muda uliotengwa na kwamba kazi imekuwa
ikifanyika kwa kulipua, ili kuhakikisha kwamba wanamaliza katika muda
uliopangwa.
Malalamiko hayo yanatokana na ukweli kwamba
baadhi ya sura za rasimu zina ibara nyingi ambazo ni vigumu kuzijadili
kwa kina, kuzifanyia marekebisho kisha kuzipigia kura kwa lengo la
kuzipitisha.
Waraka wa mgawanyo wa sura kwa siku za mjadala
katika Kamati za Bunge Maalumu unaonyesha kuwa kamati zilipaswa kujadili
sura ya pili na ya tatu za rasimu hiyo siku ya kwanza zilipoanza
kuketi, sura hizo zina jumla ya ibara 13, kazi ambayo baadhi ya wajumbe
walisema ilikuwa ni vigumu kuikamilisha kwa siku moja.
Mwenyekiti wa Kamati namba tano, Hamad Rashid
Mohamed juzi alikiri kuwapo kwa changamoto ya muda lakini akasema: “Hiyo
ndiyo hali halisi, lazima tutumie muda huo ambao tumepewa na tufanye
kazi kwa ufanisi”. Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya neno Jambo Tz