Mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph
Warioba amesema kuendelea vikao vya Bunge Maalumu la Katiba bila kuwapo
maridhiano baina ya pande zinazovutana na upande mmoja ukibaki nje ya
Bunge, ni sawa na kutumia vibaya fedha za Watanzania.
Amesema kauli kwamba akidi ya wajumbe wa Bunge
hilo imetimia na vikao vinaweza kuendelea haiwezi kuzaa Katiba
itakayokubaliwa na wananchi wote na ni tofauti na Sheria ya Mabadiliko
ya Katiba inavyoeleza katika sehemu ya kufanya uamuzi.
Akizungumza katika mahojiano na mwandishi wetu
ofisini kwake Dar es Salaam jana, Jaji Warioba alisema, “Kama uwezekano
wa kukutana upo, kwa nini Bunge liendelee kutumia fedha wakati mnajua
kuwa mwisho hamtafikia uamuzi? Jambo la msingi ni kujitahidi kuafikiana
na Bunge liwe na wajumbe wote.”
Kauli ya Warioba imeungwa mkono na Naibu Waziri wa
Fedha, Mwigulu Nchemba wakati akichangia hoja ya mabadiliko ya kanuni
ya Bunge hilo kwa kulitaka bunge hilo kujitathimini iwapo baada ya
mjadala litaweza kufikia uamuzi, ili kuepuka matumizi mabaya ya fedha za
walipakodi. Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya neno Jambo Tz
Akitoa hadhari hiyo bungeni jana, Nchemba ambaye
pia ni Mbunge wa Iramba Magharibi na Naibu Katibu Mkuu wa CCM, alisema
ni vyema Bunge hilo likajiridhisha kuhusu namna linavyoweza kutumia siku
60 zilizowekwa kwa uhakika na umuhimu wa kuziondoa siku za Jumamosi
kitendo kinachosababisha kuongezeka hadi kufikia 84.
“Tujiridhishe na kukubali ukweli kwamba kukaa hapa
kwa siku 84 bila uhakika wa kupatikana kwa theluthi mbili kwa pande
zote mbili inayohitajika kupitisha rasimu hii haiwezi kueleweka kwa
Watanzania. Ni lazima Watanzania watatuuliza tumefanya nini,” alisema.
Alisema kwa namna moja, ni vyema kujua idadi
halisi ya wale wanaoshiriki katika awamu ya pili ya Bunge hilo na wale
wasioshiriki, ili kutoa uthibitisho wa kihesabu kwamba uamuzi wa
kuendelea kwa bunge unaweza kuwa na maana.
Hata hivyo, Nchemba alisema ni vyema wakiendelea
kujadili masuala muhimu na kwa kuwa wanakwenda kujadili sura muhimu
zinazogusa moja kwa moja maisha ya Watanzania, lakini kwa uhakika kwamba
hatua hiyo itakuwa na manufaa kwa Watanzania katika hatua ya mwisho.
Alisisitiza kwamba iwapo hatua hiyo itashindikana,
utetezi wa mwisho hautaweza kueleweka kwa sababu suala la kutimia kwa
akidi kwa mujibu wa Katiba ni muhimu katika kufikia uamuzi na hasa
kuangalia upya umuhimu wa kufikia maridhiano kwa sasa.
Bunge la Katiba lilianza jana mjini Dodoma bila
kuwapo kwa wajumbe wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) na
baadhi ya wajumbe 201 wa kuteuliwa na Rais waliosusa vikao hivyo.
Ukawa wanashinikiza kujadiliwa kwa rasimu ya
Katiba iliyotolewa na iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba na si ile
iliyodai inaingizwa kinyemela na wajumbe wanaounga msimamo wa CCM wa
serikali mbili badala ya tatu zilizopendekezwa na rasimu.
Licha ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji
Francis Mutungi kuitisha kikao cha mashauriano kati yake, CCM na Ukawa,
mwafaka haukupatikana.
No comments:
Post a Comment