Wakati wajumbe wa Bunge la Katiba
wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) wakiendelea na msimamo wa
kususia vikao vinavyotarajiwa kuanza leo mjini Dodoma, mmoja wa wajumbe
wake jana aliripoti bungeni na kujiandikisha.
Mjumbe huyo, Clara Mwatuka ambaye pia ni Mbunge wa
Viti Maalumu (CUF), alionekana katika Viwanja vya Bunge saa 6:30 mchana
akiwa ameongozana na wabunge kadhaa wa CCM wakiwamo Livingstone Lusinde
(Mtera) na Jerome Bwanausi (Lulindi).
CUF ni moja ya vyama vinavyounda Ukawa, pamoja na
Chadema na NCCR Mageuzi na tayari viongozi wakuu wa vyama hivyo, Profesa
Ibrahim Lipumba, Freeman Mbowe na James Mbatia wametangaza kwamba
wajumbe wote wanaotokana na umoja wao hawatashiriki vikao vya Bunge
hilo.
Mwatuka baada ya kujaza fomu maalumu za kujiandikisha, alielekea lango la Magharibi na kuingia kwenye gari la Bwanausi.
Awali, alipoulizwa kwenye Viwanja vya Bunge kuhusu
kuwapo kwake Dodoma, alikataa kuzungumza lakini alikiri kujiandikisha
bungeni.
Baadaye alipoulizwa imekuwaje akajiandikisha
ilhali uongozi wa chama chake umesema hawatashiriki, Mwatuka alijibu:
“Kwa hapo ni mapema sana kuzungumzia suala hilo, nitazungumza kesho
(leo) kule bungeni ukinitafuta.” Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya neno Jambo Tz
Hata hivyo, baada ya dakika kama 30 kupita,
Mwatuka alimpigia simu mwandishi na kumwambia: “Sasa kuhusu mimi kuja
Dodoma, ni kweli kwamba niko hapa maana nasomesha na nilipofika nimeamua
kwenda pale bungeni kuripoti.”
Aliogeza: “Ila mimi pamoja na kujiandikisha,
sitashiriki vikao vya Bunge mpaka hapo tutakapokuwa tumepewa mwongozo,
maana tuliambiwa kwamba majadiliano yanaendelea kwa hiyo tukiruhusiwa
nitakwenda, vinginevyo sitashiriki kabisa, ndiyo hivyo.”
Bwanausi kwa upande wake alisema alimpa lifti
Mwatuka kutoka Dar es Salaam baada ya mbunge huyo wa CUF kuomba msaada
wa usafiri kwenda Dodoma.
“Ni jambo la kawaida, tulionana Dar es Salaam na
akaniuliza iwapo ninakwenda Dodoma na mimi kweli nafasi ilikuwapo kwenye
gari, kwa hiyo tumekuja naye hadi hapa, sasa zaidi ya hapo mimi
sifahamu,” alisema.
Wajumbe kutoka Zanzibar na wale wa kundi la 201
ndiyo waliokuwa wengi katika usajili wa jana na wajumbe ambao wanatokana
na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hasa kutoka Tanzania Bara
wakionekana wachache.
Milango yote ya kuingia katika eneo la Bunge
ilikuwa imefungwa na kuacha lango moja tu la Magharibi, hali
iliyosababisha baadhi ya wajumbe kuhangaika hadi pale walipopata msaada
wa polisi waliokuwa wakilinda.
Mkutano wa Bunge Maalumu ambao unafanyika kwa mara ya pili,
unatarajia kuchukua miezi miwili ambayo wajumbe wake wanapaswa kuitumia
kukamilisha kazi ya kupitia sura 15 za Rasimu ya Katiba zilizosalia na
kupiga kura kuamua kuhusu sura mbili zinazohusu Muungano.
Katika mkutano uliomalizika Aprili mwaka huu,
wabunge walikuwa wametumia zaidi ya siku 70 na walifanikiwa kupitia sura
ya kwanza na sita ambazo hata hivyo, hazikupigiwa kura.
Hadi jana jioni Mwenyekiti wa Bunge Maalumu,
Samuel Sitta alikuwa akiongoza kikao cha Kamati ya Uongozi, lakini
hakukuwa na taarifa rasmi kuhusu ratiba wala ajenda za mkutano
unaotarajiwa kuanza leo. Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya neno Jambo Tz
Na Mwananchi
Na Mwananchi
No comments:
Post a Comment