Aliyekuwa mjumbe wa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba, Humphrey Polepole amesema makongamano na mijadala
inayohusu Katiba mpya yataendelea kwa sababu ni ya lazima pia ni haki ya
kikatiba.
Akizungumza kwenye Kongamano la Katiba
lilioandaliwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) jana, Polepole
alisema mtu anayezuia wananchi kuendelea kuzungumzia Katiba amepoteza
sifa za kuwa kiongozi wa nchi.
Huku akishangiliwa na washiriki wa kongamano hilo,
Polepole alisema Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni nchi ya
kidemokrasia, inayoheshimu haki za binadamu na utawala wa kiraia. Hivyo
inashangaza kusikia kuna kiongozi anajaribu kuwafunga mdomo wananchi. Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya neno Jambo Tz
“Nimesikia mtu mmoja anasema msifanye makongamano.
Sijamfahamu vizuri, lakini ninachokiona ni kwamba anaendelea kupoteza
sifa za kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano kama alikuwa anataka kufanya
hivyo,” alisema Polepole.
Ingawa hakumtaja jina, juzi Mwenyekiti wa Bunge la
Katiba, Samuel Sitta na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Rehema Nchimbi hivi
karibuni walikaririwa wakihoji uhalali wa mijadala inayoendelea sasa
kuhusu Katiba Mpya.
Sitta, akiongoza kikao cha Bunge la Katiba juzi,
alimtaka Waziri wa Habari na Utamaduni kuvichunguza vyombo vya habari
vinavyorusha matangazo ya watu aliodai wanapotosha ukweli kuhusu Katiba.
Ingawa Sitta hakukitaja chombo chochote, alikuwa
akielekeza maoni yake kwenye mdahalo uliorushwa Jumatatu wakati wajumbe
wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, wakiongozwa na Jaji Joseph
Warioba waliposhiriki na kujibu hoja mbalimbali zinazoonekana kuwa na
utata kwenye Rasimu ya Katiba.
Polepole aliongeza kusema: “Mimi nimsihi tu kwamba
kuongea ndiyo haki yetu na jadi yetu. Wakati tupo kwenye Tume, kila mtu
alikuwa anaongea na wakati huo kazi ilikuwa ngumu zaidi kwa sababu
tulikuwa hata hatufahamu rasimu itaonekana namna gani.”
Alisema kipindi hicho vyama vya siasa ndiyo
vilikuwa mstari wa mbele kuongea na kushinikiza wananchi kusema maneno
yasiyokuwa ya kwao na kushauri kuwa ni vyema kama viongozi hao wangewapa
watu elimu ya uraia.
Huku akiendelea kushangiliwa, Polepole alihoji:
“Sasa nashangaa tena hivi sasa tunaambiwa tusizungumze, tufunge midomo,
tukae kimya. Kwani sisi kazi yetu ni kazi gani? Tusiongee halafu
tukafanye kazi gani? Napenda nipeleke salamu hizo,” alisema.
Aliwataka wajumbe wa Bunge la Katiba kuacha
kuwapuuza wananchi kwa kudhani kwamba hawajui wanachotaka na kwamba ni
kosa kubwa kuwaambia Watanzania kitu cha kufanya, wakati wao wanajua
wanachofanya.
“Hizo zama zimepita na sidhani kama zipo kwenye
ulimwengu wa leo. Haikuwa na maana kuwafuata na kuwaambia watoe maoni,
halafu mwisho wa siku waletewe kitu cha ajabu,” alisema.
Mbali na Sitta, hivi karibuni Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Rehema
Nchimbi alikaririwa na baadhi ya vyombo vya habari akipiga marufuku
mijadala yoyote inayohusu Katiba na rasimu yake katika maeneo na viunga
vyote vya mji wa Dodoma.
Dk Nchimbi alisema kitendo hicho ni makubaliano ya Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Dodoma anayoiongoza yeye.
“Ni marufuku mikutano ya hadhara au makongamano
yoyote ya Katiba kufanywa nje ya Bunge la Katiba, kwa kuwa vitendo hivyo
vinaweza kuwavuruga wajumbe wa Bunge hilo,” alisema Dk Nchimbi.
Akizungumzia hatua hiyo, Mbunge wa Kigoma
Kaskazini, Zitto Kabwe alisema hatua hiyo ya kuzuia wananchi kujadili
masuala ambayo ni muhimu kwao na nchi yao ni kinyume na Katiba ya nchi.
“Hawana mamlaka ya kuzuia mijadala. Wananchi wana
haki ya kikatiba ya kujadili masuala mbalimbali hasa ya kimaendeleo kwa
mujibu wa Katiba,” alisema Kabwe.
Naye mjumbe wa Bunge hilo, Maria Sarungi alisema
mjadala wa Katiba ni haki ya kila mwananchi na kuzuiwa kutoa maoni yake
ni kumnyima uhuru wa kikatiba. Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya neno Jambo Tz
Na Mwananchi
Na Mwananchi
No comments:
Post a Comment