Rais Jakaya Kikwete jana aligoma kupokea zawadi ya dhahabu kutoka Kampuni ya Nyamigogo Grand Vezir Holdings ya mkoani Geita.
Taarifa iliyotolewa na Ikulu jana
ilisema viongozi wa kampuni hiyo walitaka kumkabidhi Rais Kikwete gramu
227 za dhahabu safi wakati alipotembelea mgodi huo.
Rais Kikwete badala yake aliwaelekeza waiuze dhahabu na fedha zitakazopatikana zitumike kuwasaidia watoto yatima.
Alikabidhiwa zawadi hiyo wakati wa
sherehe ya kuzindua mgodi wa uchenjuaji dhahabu wa kampuni hiyo nje
kidogo ya mji mdogo wa Kharuma ambao ni makao makuu ya wilaya mpya ya
Nyang'hwale, Geita.
Gramu hizo 227 zina thamani ya Sh16 milioni kwa bei ya sasa ya soko la dhahabu duniani.
Baada ya kukabidhiwa zawadi hiyo, Rais
Kikwete aliuliza: "Sasa nifanye nini na zawadi hii? Nawarudishieni hii
dhahabu, iuzeni popote mnakotaka na fedha itakayopatikana tutawapa
watoto yatima."
Akizungumza na wananchi katika mgodi
huo, Rais Kikwete aliupongeza uongozi wa mgodi huo akisema umeongeza
thamani ya dhahabu na maisha ya wananchi katika eneo hilo... "Mmefanya
vizuri na mgodi huu, ni mradi wa maana kwa kuongeza thamani ya dhahabu
na kuboresha maisha ya wananchi katika eneo hili. Ubunifu huu unastahili
pongezi," alisema Rais Kikwete.