Rais Jakaya Kikwete jana aligoma kupokea zawadi ya dhahabu kutoka Kampuni ya Nyamigogo Grand Vezir Holdings ya mkoani Geita.
Taarifa iliyotolewa na Ikulu jana
ilisema viongozi wa kampuni hiyo walitaka kumkabidhi Rais Kikwete gramu
227 za dhahabu safi wakati alipotembelea mgodi huo.
Rais Kikwete badala yake aliwaelekeza waiuze dhahabu na fedha zitakazopatikana zitumike kuwasaidia watoto yatima.
Alikabidhiwa zawadi hiyo wakati wa
sherehe ya kuzindua mgodi wa uchenjuaji dhahabu wa kampuni hiyo nje
kidogo ya mji mdogo wa Kharuma ambao ni makao makuu ya wilaya mpya ya
Nyang'hwale, Geita.
Gramu hizo 227 zina thamani ya Sh16 milioni kwa bei ya sasa ya soko la dhahabu duniani.
Baada ya kukabidhiwa zawadi hiyo, Rais
Kikwete aliuliza: "Sasa nifanye nini na zawadi hii? Nawarudishieni hii
dhahabu, iuzeni popote mnakotaka na fedha itakayopatikana tutawapa
watoto yatima."
Akizungumza na wananchi katika mgodi
huo, Rais Kikwete aliupongeza uongozi wa mgodi huo akisema umeongeza
thamani ya dhahabu na maisha ya wananchi katika eneo hilo... "Mmefanya
vizuri na mgodi huu, ni mradi wa maana kwa kuongeza thamani ya dhahabu
na kuboresha maisha ya wananchi katika eneo hili. Ubunifu huu unastahili
pongezi," alisema Rais Kikwete.
Mgodi wa Nyamigogo ni wa marudio kwani
unazalisha dhahabu kutokana na mchanga ambao awali ulishafuliwa na
kutoa dhahabu. Ulianzishwa mwaka 2011 na mpaka sasa kiasi cha Sh 1.6
bilioni kimewekezwa kuuendeleza.
Uongozi wa mgodi huo ulisema mgodi huo
unaozalisha kiasi cha gramu kati ya 500 na 600 kwa mwezi, na unaajiri
watu 45 kati yao wanawake 10.
Rais Kikwete alizindua mgodi huo ikiwa
sehemu ya kukagua na kuzindua miradi ya maendeleo katika ziara yake
Geita ambao ni moja ya mikoa minne aliyoianzisha mwaka jana. Mikoa
mingine ni Simiyu, Njombe na Katavi.
Amtetea Magufuli
Rais Kikwete amewataka viongozi wa CCM
kuacha kulalamikia utendaji wa viongozi na badala yake kuelimisha
wananchi juu ya utendaji wa Serikali.
Akizungumza wakati wa kikao cha
majumuisho ya ziara yake ya siku tano mkoani Geita, Rais Kikwete alisema
viongozi hao walimpinga Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli wakati akiwa
Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi alipokuwa akipambana na uvuvi
haramu.
"Walimwona mbaya, tena hata wazee wa
CCM walilalamika na kupiga kelele... anatuharibia kura, sasa hayupo,
samaki wamekwisha ziwani. Watu wenu wamebaki kuwa maskini na hakuna
samaki," alisema.
Aliwahimiza viongozi wa Mkoa wa Geita
kufikiria mpango wa kufuga samaki akitoa mfano wa Vietnam ambayo sasa
inafuga sato na sangara kwa kiasi kikubwa.
Chanzo:Mwananchi
No comments:
Post a Comment