Wednesday, November 13, 2013

SALAMU ZA RAMBIRAMBI KWA KIFO CHA DK MVUNGI KUTOKA CHADEMA

 

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe ametuma salaam za rambirambi ya kifo cha Dkt. Edmund Sengondo Mvungi, akitoa pole kwa familia, uongozi na wanachama wa NCCR-Mageuzi, Tume ya Mabadiliko ya Katiba Mpya na wananchi wote walioguswa na msiba huo. Akitoa kauli hiyo kwa niaba ya CHADEMA na wanachama wa chama hicho, Mwenyekiti Mbowe amesema kuwa amepokea kwa masikitiko na mshituko mkubwa taarifa za kifo cha Dkt. Mvungi, akimwelezea kuwa alikuwa mwanasiasa mwenye msimamo ambaye hakuwahi kutetereka kusimama na chama chake tangu alipojiunga nacho na kuanza kushiriki siasa za mageuzi nchini. “Kwa niaba ya CHADEMA na wanachama wetu nchi nzima, napenda kutoa salaam za pole sana kwa familia ya marehemu, mjane na watoto. Natoa pole kwa Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia na wanachama wa chama hicho, pia tunatoa pole kwa Jaji Mstaafu Joseph Warioba na makamishna wote wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba kwakifo cha Dkt. Mvungi. Tunaomba Mwenyezi Mungu awatie nguvu sana wakati huu wa majaribu na majonzi makubwa. “Dkt. Mvungi alikuwa mwanasiasa mwenye misimamo ambaye hakuwahi kukihama chama chake tangu alipoanza siasa za mageuzi nchini. Ni kati ya wasomi wachache waliokuwa na ujasiri na kuthubutu kujiunga na vyama vya upinzani tangu mapema. "Mvungi pia alikuwa mmoja wa wanasiasa wa mwanzo kabisa kupigania nchi yetu iwe na Katiba Mpya, ili hatimaye siasa zetu, hususan demokrasia ya vyama vingi nchini iendeshwe kwa misingi iliyo imara,” amesema Mwenyekiti Mbowe na kuongeza; “Mwenyezi Mungu alimjalia marehemu akaweza kushiriki kutimiza ndoto hiyo baada ya kuteuliwa kuwa mmoja wa makamishna wa Tume ya Mpya, kazi ambayo ameifanya hadi siku alipokutwa na tukio lililosababisha mauti yake.” Mwenyekiti Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni na Mbunge wa Hai, amesisitiza kuwa kwa namna ambavyo Dkt. Mvungi alikuwa mstari wa mbele katika suala hilo, Tume ya Katiba Mpya inao wajibu wa kuthamini mchango wake katika hatua iliyofikia sasa ya mchakato huo nyeti hadi utakapofika mwisho. “Wakati tukimwombea marehemu kwa Mungu, alazwe mahali pema peponi, ni matumaini yetu kuwa serikali kupitia vyombo vyake itahakikisha kuwa wale wote waliohusika katika tukio la lililosababisha kukatisha uhai wa Dkt. Mvungi wanapatikana na kuchukuliwa hatua zote zinazostahili kisheria,” amesema Mwenyekiti Mbowe.

No comments:

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...