Ahmed Abdul Zaher amejitetea akisema hakunuia kuzua hisia za kisiasa
Mchezaji soka mmoja katika moja ya vilabu maarufu nchini Misri ametupwa nje ya mechi za klabu hiyo baada ya kuonekana kumuunga mkono rais aliyeondolewa mamlakani Mohammed Morsi.
Klabu ya Al Ahly, imesema kuwa Ahmed Abdul Zaher , hatashiriki mchuano wa FIFA wa klabu bingwa duniani baada ya kupiga saluti ya vidole vinne mnamo siku ya Jumapili.
Mchezaji huyo alikuwa anasherehekea bao lake la mchuano wa mabingwa wa Afrika ambapo Al Ahly ilishinda kwa mabao 2-0 dhidi ya Orlando Pirates wa Afrika Kusini.
Ishara hio imekuwa ikitumika kama ishara ya kumuunga mkono bwana Morsi.
Ishara hiyo pia ilitokana na
maandamano ya wafuasi wa Morsi waliotawanywa na maafisa wa usalama mnamo
mwezi Agosti baada ya kukesha katika eneo walilosema alikuwa amezuiliwa
Morsi.
Rais Morsi alikuwa rais wa kwanza wa
nchi hiyo kuchaguliwa kidemokrasia, na sasa anakabiliwa na kesi ya
kuchochea mauaji ya waandamanaji wakati wa ghasia zilizotokea mjini
Cairo mwaka jana.
Yeye mwenyewe aling'olewa kutoka uongozini mwezi Julai.
Abdul Zaher alisherehekea kwa ishara
ya vidole vinne baada ya kuingiza bao la Al Ahly la pili ambapo
waliibuka washindi dhidi ya Orlando Pirates.
"ndio nilitoa ishara hiyo ya Rabaa," alinukuliwa akisema kwenye mtandao wa FilGoal.
"lakini sikunuia kuzua hisia za
kisiasa kwa mtu yeyote, nilichonuia ni kumkumbuka mtu yeyote
aliyefariki, awe raia wa kawaida au hata polisi.''
Mnamo siku ya Jumatatu maafisa wa
klabu ya Al Ahly, walisema kuwa Ahmed Abdul Zaher hatashirikishwa kwenye
mechi itakayochezwa nchini Morocco.
No comments:
Post a Comment