Tume ya Mabadiliko ya Katiba nchini
Tanzania imepata pigo baada ya mmoja wa wajumbe wake Dr. Sengondo Mvungi
kufariki dunia nchini Afrika Kusini, ambako alikuwa akitibiwa.
Dr. Mvungi, alipelekwa Afrika Kusini
kwa matibabu zaidi baada ya kuvamiwa na watu wanaoaminika kuwa majambazi
nyumbani kwake mjini Dar, es Salaam, wiki iliyopita.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na
Katibu wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Bw. Assaa Rashid Dkt. Mvungi
alifariki majira ya saa 8:30 mchana kwa saa za Afrika ya Kusini akiwa
katika Hospitali ya Milpark.
"Kwa masikitiko makubwa, Tume
inawafahamisha wananchi kuwa Mjumbe wake, Dkt. Sengondo Mvungi aliyekuwa
akipata matibabu katika Hospital ya Milpark iliyopo jijini Johannesburg
nchini Afrika Kusini amefariki dunia leo Jumanne, Novemba 12, 2013 saa
8:30 mchana kwa saa za Afrika ya Kusini," amesema Bwana Rashid katika
taarifa yake fupi.
Amesema taratibu za kuusafirisha mwili wa marehemu kutoka nchini Afrika Kusini kuja nchini Tanzania kwa mazishi zinaendelea.
Marehemu Dkt. Mvungi alisafirishwa
siku ya Alhamisi, Novemba 7, 2013 kwenda nchini Afrika Kusini kwa
uchunguzi na matibabu zaidi akitokea Kitengo cha Mifupa Muhimbili (MOI)
alipokuwa amelazwa baada ya kuvamiwa nyumbani kwake.
Dkt. Mvungi pamoja na kuwa ni
mwanasheria aliyebobea katika fani ya Katiba, pia ni mwanasiasa ambaye
aliwahi kugombea urais mwaka 2005 kupitia chama cha NCCR Mageuzi.
No comments:
Post a Comment