Naibu
Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Amos Makalla, jana
alitoa taarifa kwa umma akieleza bayana kwamba yeye ndiye aliyeliruhusu
gazeti hili kuendelea kutolewa kwa njia ya mtandao (online) na Gazeti la
Rai kutolewa kila siku.
Makalla
alitoa ufafanuzi huo muda mfupi baada ya Idara ya Habari-Maelezo kutoa
taarifa kwamba Serikali imesikitishwa na Gazeti la Mwananchi na gazeti
dada la Rai, Mtanzania kukiuka masharti ya adhabu walizopewa.
Septemba 27, mwaka huu Serikali iliyafungia Mwananchi kwa siku 14 na Mtanzania siku 90.
Wakati
likianza kutumikia adhabu yake, Mwananchi ambalo tayari limemaliza
kuitumikia, liliendelea kutoa taarifa kwenye tovuti yake wakati Kampuni
ya New Habari (2006) Ltd ambayo inamiliki Mtanzania ilianza kuchapisha
kila siku gazeti la Rai ambalo awali lilikuwa likichapishwa kila wiki.
Katika ufafanuzi wake alioutoa
jana
Makalla alisema: "Nimelazimika kueleza haya baada ya taarifa mpya ya
Idara ya Habari-Maelezo iliyohoji uhalali wa gazeti la Mwananchi kuwa
online (mtandaoni) na gazeti la Rai kutoka kila siku, badala ya mara
moja kwa wiki (Alhamisi)."