KOCHA Mkuu wa Azam FC, Muingereza Stewart Hall amesema kwamba ni kazi ngumu Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kupata bingwa nje ya Simba na Yanga kwa sababu timu hizo zinapendelewa mno na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Akizungumza Hall amesema kwamba timu
nyingine nje ya Simba na Yanga SC ili kuwa bingwa inabidi ifanye kazi
ngumu sana ambayo kwa sasa yeye na timu yake, Azam FC wanajaribu.
Kwanza amesema ratiba ya Ligi Kuu
inapopangwa inakuwa katika mazingira mazuri kwa timu hizo na mazingira
magumu kwa timu nyingine ambazo zinaonekana zikitendewa haki zinaweza
kuzima ubabe wa timu hizo katika soka ya Tanzania.
Stewart alitoa mfano hadi sasa katika
mechi za Ligi Kuu ambazo tayari zimechezwa, Simba na Yanga kila moja
imecheza mechi mbili tu ugenini, wakati Azam FC imecheza mechi sita
ugenini, jambo ambalo amesema huwezi kulikuta katika ligi nyingine
yoyote duniani.
"Ligi lazima iwe ya uwiano sawa wa
mechi za nyumbani na ugenini kwa kila timu, lakini hiyo si kwa hapa
Tanzania, kuna ratiba maalum kwa ajili ya Simba na Yanga, namna hii
usitegemee soka ya nchi hii ikakua,"alisema.
Lakini pia, Stewart amesema wakati
timu nyingine zinacheza mechi 13 nyumbani na 13 ugenini, kwa Simba na
Yanga wanacheza mechi saba tu ugenini na hakuna sabau ya msingi katika
hilo.
"Sisi Azam ni washindani wa Simba na
Yanga katika mbio za ubingwa, lakini hatupati nafasi ya kucheza na hizo
timu Uwanja wetu wa nyumbani, tunacheza nao ugenini mechi zote. Kwa nini
hawaji Chamazi?"alihoji Stewart.
Lakini pia Stewart alihoji juu ya
sababu ya Azam, kwenda kucheza na Ruvu Shooting Uwanja wa Mabatini,
Mlandizi, wakati Simba na Yanga wanacheza na timu hiyo mechi zote Uwanja
wao wa nyumbani, Taifa, Dar es Salaam.
"Lakini hii si haki, na kwa namna hii
unafikiri lini timu nyingine nje ya Simba itakuwa bingwa hapa, ni vigumu
sana, lazima TFF wahakikishe haki inatendeka katika Ligi hii,"alisema.
Pamoja na hayo, Stewart amesema
malengo ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu kwa timu yake msimu huu yapo pale
pale pamoja na ukweli huo wa Simba na Yanga kubebwa na TFF.
"Tumeanza ligi katika mazingira
magumu, tumekuwa na majeruhi wengi na bahati mbaya mwanzoni tu, beki
wetu tegemeo Aggrey Morris akapewa kadi nyekundu, lakini tunapambana
kuhakikisha tunamudu kucheza ligi katika mazingira haya magumu,".
"Na unaweza kuona hatupo mbali na eneo
la ubingwa, tupo nafasi ya pili na wakati wowote tunaweza kupanda
kileleni, tunajituma sana kama timu na kila mtu binafsi kuhakikisha
tunatimiza malengo tuliyojiwekea msimu huu, kutwaa ubingwa,"alisema.
Chanzo: binzubeiry
No comments:
Post a Comment