Jeshi la Polisi mkoani Temeke,
linamshikilia dereva wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi,
aliyefahamika kwa jina la Bw. Samwel Mulagalazi, ambaye anadaiwa
kushirikiana na watu wawili waliotaka kumtapeli mteja wa Shirika la
Umeme nchini (TANESCO), sh. milioni 60.
Tukio hilo limetokea juzi saa 11 jioni
katika kiwanda kilichopo Mbagala, Dar es Salaam (jina tunalo), ambapo
matapeli (vishoka), waliojifanya wafanyakazi wa TANESCO, Makao Makuu,
Ubungo, walitaka kufanya utapeli huo kwa mmiliki wa kiwanda hicho.
Matapeli hao walimpigia simu mmiliki wa kiwanda hicho (jina tunalo), wakidai kiwanda chake kinaiba umeme hivyo walimtaka atoe sh. milioni 60 asiweze kukatiwa umeme.
Mmiliki huyo akitambua kuwa mita zake
hazikuwa na tatizo lolote na hahusiki na wizi huo, aliwasiliana na
Meneja wa TANESCO wilayani Temeke, Mhandisi Richard Mallamia na
kumweleza vitisho alivyopewa na matapeli hao na pesa waliyotaka kupewa.
Mhandisi Mallamia alimtaka mteja huyo
wa TANESCO, kutowakatisha tamaa matapeli hao badala yake awapigie simu
ili waende kuchukua pesa hizo.
Baada ya kumpa ushauri huo, Mhandisi
Mallamia alifanya mawasiliano na ofisi ya shirika hilo Idara ya Usalama
na Jeshi la Polisi mkoani Temeke ili wakaweke mtego.
Akizungumza na Majira, Mhandisi
Mallamia alisema baada ya matapeli hao kupigiwa simu ili waende kuchukua
pesa walizotaka, awali walikubali lakini baadaye walimpigia simu mteja
wao na kudai wanamtuma dereva.
Bw. Mulagalazi alifika kiwandani hapo
kama dereva aliyetumwa na matapeli hao akiwa na gari Land Cruiser
Hardtop, yenye namba SKT 3665 na kuingia mtegoni (kukamatwa).
Maofisa wa TANESCO na polisi walimtaka
mmiliki wa kiwanda awapigie simu matapeli hao na kuwajulisha tayari
ametoa pesa hizo kwa dereva wao. Vishoka hao walimpigia simu dereva na
kumtaka wakutane maeneo ya Mbagala.
Polisi na Maofisa wa TANESCO waliingia
ndani ya STK ambalo lilikuwa l ikiendeshwa na mtuhumiwa ili kwenda
kuwakamata matapeli hao ambao walipaki gari lao barabarani.
Chanzo chetu cha habari kilidai kuwa,
matapeli hao wakiwa na gari aina ya RAV 4, waliiona STK ikiwafuata
taratibu bila kujua ndani ya gari kulikuwa na Maofisa wa TANESCO na
polisi ambao walijificha ili wasionekane.
Dereva (mtuhumiwa), alisimama, kushuka
kwenye gari na kuwafuata matapeli hao akiwaambia TANESCO wamechukua
kitambulisho chake hivyo matapeli waliingia kwenye gari na kukimbia kwa
mwendo wa kasi.
Mtuhumiwa (dereva), alirudi katika
gari na polisi walimtaka warudi Kituo cha Polisi Mbagala. Hadi jana
mchana bado alikuwa akiendelea kuhojiwa.
Inadaiwa kuwa, katika maelezo yake
dereva huyo ambaye inadaiwa anamuendesha Mratibu wa Mradi wa Kibamba,
aliwataja watu waliomtuma kwa majina ya Godfrey Mjakamaarufu 'Makofia'
na Modest Kayombo Thomas.
Alidai Thomas ni mwanafunzi wa Chuo
cha Teknolojia Dar es Salaam (DIT) ambaye amejenga maeneo ya Vikindu na
Mjaka ni fundi umeme ambaye hupata tenda mbalimbali.
Katika utetezi wake baada ya
kukamatwa, inadaiwa mtuhumiwa alidai yeye hakuwa akifahamu lolote zaidi
ya kuambiwa akachukue mzigo ambao hakujua ni mzigo gani.
Taarifa za uhakika zinasema kuwa,
vishoka hao Mjaka na Thomas wana kesi Mahakama ya Kisutu, Dar es Salaam,
ambayo inaendelea kusikilizwa na itatajwa Oktoba 15 mwaka huu,
wakidaiwa kujifanya wafanyakazi wa TANESCO na walikamatwa wakiwa wamevaa
sare za shirika hilo.
Chanzo hicho kilidai watu hao
walikamatwa wakifanya utapeli kwa wateja wa TANESCO eneo la Kigamboni,
Dar es Salaam.Kamanda wa Polisi mkoani humo, Engelbert Kiondo, alisema
tukio hilo atalitolea ufafanuzi leo baada ya kupata taarifa kamili.
Mhandisi Mallamia alisema kukamatwa
kwa mtuhumiwa ni matokeo ya elimu wanayoendelea kuitoa kwa wateja wao
ambao wanatumia umeme mkubwa wakiwemo wamiliki wa viwanda, bekari za
mikati, hoteli pamoja na wateja wadogo ili wawe makini kujiepusha na
matapeli wa aina hiyo.
Alisema hivi sasa kuna mtandao mkubwa
ambao unalihujumu shirika hilo kupitia wateja wake na kuchafua sifa ya
TANESCO kwenye jamii jambo ambalo haliwezi kuvumilika.
Source:MAJIRA
No comments:
Post a Comment