Naibu waziri wa fedha, Saada Salum
Wakati Tanzania ikitajwa kuwa ni
miongoni mwa nchi zenye amani na utulivu, imebainika kuwa Watanzania ni
miongoni mwa watu wasio na furaha na waliokata tamaa hapa duniani.
Ripoti inayoonyesha orodha ya nchi
zenye furaha duniani ya mwaka 2013 (World Happiness Report 2013),
imeitaja Tanzania kuwa ni miongoni mwa nchi 10 za mwisho duniani kati ya
nchi 156 zilizofanyiwa utafiti huo.
Ripoti hiyo iliyoandaliwa na kundi la
wataalamu kutoka Umoja wa Mataifa (UN), kati ya mwaka 2010 na 2012,
inaonyesha kuwa Tanzania imeshika nafasi ya 151 ikiburuta mkia pamoja na
nchi za Rwanda, Burundi, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Benin na Togo.
Upatikanaji wa huduma za jamii,
mtazamo wa watu kuhusu rushwa, umri wa kuishi, ukosefu wa kazi, pato la
taifa na ukarimu wa watu katika nchi husika, ni baadhi ya vigezo
vilivyoangaliwa wakati wa kuandaa taarifa hiyo.
Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia
Kabaka alieleza kushtushwa na ripoti hiyo kwa maelezo kwamba ni asilimia
11.7 tu ya Watanzania wasio na ajira na kwamba wale wanaofanya kazi,
wanapata huduma zote za msingi, ikiwa ni pamoja na kwenda likizo na
mishahara inayolingana na taaluma zao.
"Watanzania wana furaha, kwa upande wa
wafanyakazi wanapata haki zao zote wanazostahili, sijui ni vigezo vipi
wametumia...kwa mujibu wa takwimu za 2006 ni asilimia 11.7 ya Watanzania
ndio waliokuwa hawana kazi, lakini wakati huo idadi ya watu ilikuwa
ndogo, hivi sasa imeongezeka," alisema Kabaka na kuongeza:"Usafiri ndiyo
tatizo linalowasumbua wafanyakazi wengi kwa kuwa wanachelewa kwenda
kazini."
Naye, Naibu Waziri wa Fedha, Saada
Salum alisema pamoja na vigezo vingine vilivyotumika kutambua furaha ya
Watanzania, umaskini ndiyo unaoweza kuwa chanzo cha Tanzania kushika
nafasi za mwisho.
"Inategemea na vigezo vingine
walivyovitumia, nakubali kuwa Tanzania ni maskini pengine hali hiyo
imeifanya nchi kushika nafasi ya mwisho," alisema Salum.
Nchi zilizoongoza
Taarifa hiyo imezitaja nchi tano;
Denmark, Norway, Uswisi, Netherlands na Sweden kuwa ndizo zinazoongoza
kwa watu wake kuwa na furaha zaidi duniani, huku Angola ikishika nafasi
ya kwanza Afrika na ya 61 duniani ikifuatiwa na Algeria (73), Libya
(78), Ghana (86), Zambia (91), Lesotho (98), Morocco (99) na Swaziland
(100).
Kwa upande wa Afrika Mashariki,
wananchi wa Uganda ndio walionekana kuwa na furaha zaidi kwani nchi hiyo
imeshika nafasi ya 120 wakifuatiwa na Kenya (123), Tanzania (151),
Rwanda (152) na Burundi (153).
Ripoti hiyo inabainisha kuwa kati ya
mwaka 2005 na 2012, nchi 60 duniani ziliongeza viwango vya furaha kwa
watu wake, kati ya hizo 16 zikiwa barani Afrika, Kusini mwa Jangwa la
Sahara.
Nchi 29 zilibaki katika viwango vya awali, huku watu kutoka nchi 41 wakipunguza viwango vyao vya furaha.
Ikilinganishwa na ripoti ilifanywa
kati ya 2005 – 2007, Tanzania imeshuka kutoka asilimia 40 hadi 37.
Ripoti hiyo inaeleza kuwa asilimia 10 ya watu duniani wanasumbuliwa na
matatizo ya akili ambayo yamewasababisha kukosa furaha.
Hata hivyo, imebainika kuwa mtu mmoja anaweza kukosa furaha kutokana na sababu zaidi ya moja.
"Mtu mmoja anaweza kukosa furaha
kutokana na sababu mbalimbali kama umaskini, ukosefu wa kazi, kuvunjika
kwa ndoa na kusumbuliwa na ugonjwa. Lakini sehemu kubwa, matatizo sugu
ya akili yamesababisha kukosekana kwa furaha," inasema sehemu ya ripoti
hiyo.
Alipoulizwa kuhusu ripoti hiyo, Waziri
wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Hussein Mwinyi alisema bado hajaiona na
kwamba atakapoisoma atakuwa tayari kuizungumzia.
"Sijaiona ripoti hiyo kwa hivyo siwezi
kusema chochote hadi niione, wewe si umeiona ndiyo maana ukatupa
maswali?" alihoji Dk Mwinyi.
Wataalamu wanena
Mwanasaikolojia Modesta Kimonga,
alisema Watanzania wengi wanakuwa na hasira kila wakati kutokana na
kukosa matumaini, baada ya mambo yao kushindwa kufanikiwa.
Alisema hali hiyo inatokana na watu wengi kushindwa kudhibiti magonjwa na matatizo mengine yanayowakabili.
"Watanzania wengi wanasumbuliwa na
mood disorder, wanakuwa wakali, wenye hasira kila wakati. Mambo yao
hayaendi wamekosa tumaini. Hali hiyo inawakumbwa hata watoto ambao
wanakosa mahitaji yao ya msingi," alisema Kimonga.
Hata hivyo, ripoti hiyo inaeleza kuwa
zipo sababu mbalimbali zinazowafanya watu kuwa na furaha: "Wanauchumi
wanasema furaha inaletwa na kipato kikubwa, wanasaikolojia wanaamini
furaha inakuja baada ya mtu kuwa na afya njema na viongozi wa dini
wanaamini furaha huletwa na maadili mema," inasema sehemu ya ripoti
hiyo.
Mhadhiri wa Uchumi wa Chuo Kikuu cha
Mzumbe, Dk Honest Ngowi alisema kuna uhusiano wa karibu kati ya umaskini
na furaha, kwa kuwa mtu asiye na kipato cha kununua mahitaji yake ya
msingi hawezi kuwa na furaha.
"Gharama za bidhaa zipo juu, mtu
masikini hawezi kuwa na furaha, hata hivyo haimaanishi kuwa nchi tajiri
ndizo zenye furaha. Nchi kama Norway pamoja na kuwa na uchumi mzuri,
lakini ina idadi kubwa ya watu wanaojinyonga," alisema Ngowi.
Akizungumzia ripoti hiyo, Mwenyekiti
wa Chama cha Kijamii, Costantine Akitanda, alisema taarifa hiyo iko
sahihi na kwamba karibu kila Mtanzania analalamika.
"Ukichunguza utagundua kuwa karibu
kila Mtanzania analalamika. Hata sera zilizopo hazina mfumo
unaowawezesha watu kunufaika na maliasili za taifa," alisema Akitanda.
Pamoja na msukosuko wa uchumi
ulioitikisa dunia kuanzia mwaka 2008, dunia imeshuhudia watu wakiongeza
viwango vyao vya furaha kutokana na sababu mbalimbali kulingana na
mahali nchi ilipo.
Mkazi wa Mabibo, Kinondoni jijini Dar
es Salaam, Vick Manonge, alisema ripoti hiyo inaonyesha hali halisi
ilivyo hivi sasa hapa nchini, kwa kuwa watu wengi wanaonekana kuwa na
hasira.
"Kama kuna mtu hakubaliani na hilo
(ripoti hiyo) aangalie kwenye daladala watu walivyo na hasira bila
sababu ya msingi, mwingine hataki aulizwe hata nauli, " alisema Manonge.
Katika siku za hivi karibuni baadhi ya
viongozi wakubwa duniani wamekuwa wakizitaka Serikali kutunga sera za
maendeleo zitakazoendana na hali halisi ya maisha ya watu wa eneo
husika, ili kuweka mazingira yatakayowaletea wananchi furaha.
Baadhi ya huduma zinazotolewa na
serikali ni afya, kutengeneza ajira, elimu na kuweka mazingira bora ya
kujiwezesha kichumi kwa kila Mtanzania.
Chanzo:mwananchi
No comments:
Post a Comment