Naibu
Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Amos Makalla, jana
alitoa taarifa kwa umma akieleza bayana kwamba yeye ndiye aliyeliruhusu
gazeti hili kuendelea kutolewa kwa njia ya mtandao (online) na Gazeti la
Rai kutolewa kila siku.
Makalla
alitoa ufafanuzi huo muda mfupi baada ya Idara ya Habari-Maelezo kutoa
taarifa kwamba Serikali imesikitishwa na Gazeti la Mwananchi na gazeti
dada la Rai, Mtanzania kukiuka masharti ya adhabu walizopewa.
Septemba 27, mwaka huu Serikali iliyafungia Mwananchi kwa siku 14 na Mtanzania siku 90.
Wakati
likianza kutumikia adhabu yake, Mwananchi ambalo tayari limemaliza
kuitumikia, liliendelea kutoa taarifa kwenye tovuti yake wakati Kampuni
ya New Habari (2006) Ltd ambayo inamiliki Mtanzania ilianza kuchapisha
kila siku gazeti la Rai ambalo awali lilikuwa likichapishwa kila wiki.
Katika ufafanuzi wake alioutoa
jana
Makalla alisema: "Nimelazimika kueleza haya baada ya taarifa mpya ya
Idara ya Habari-Maelezo iliyohoji uhalali wa gazeti la Mwananchi kuwa
online (mtandaoni) na gazeti la Rai kutoka kila siku, badala ya mara
moja kwa wiki (Alhamisi)."
Katika
ufafanuzi wake Makalla alisema kuwa Oktoba 4 mwaka huu, alifanya
mazungumzo na viongozi wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited
(MCL) na New Habari Corporation (2006) Limited na Msajili wa Magazeti na
kwamba katika kikao hicho yaliwasilishwa maombi matatu.
"Waziri
aliombwa kupitia upya adhabu iliyotolewa kwa magazeti hayo. Katika hili
majibu yangu niliwaambia kwamba mwenye mamlaka juu ya suala hilo ni
waziri mwenye dhamana na masuala ya habari pekee," alisema.
Kuhusu
gazeti la Mwananchi kuwekwa katika mtandao, Makalla alisema naibu
msajili wa magazeti alisema kuwa hakuna sheria yoyote inayoweza kuzuia
gazeti hilo kuwa mtandaoni, lakini aliwataka lisionekane gazeti zima
kama lilivyo, pia wabadili nembo ya gazeti na kuweka ya MCL.
"Baada ya
maelezo hayo niliridhia gazeti hilo liwe mtandaoni kwa kuzingatia
angalizo lililotolewa na naibu msajili wa magazeti," alisema Makalla.
Kuhusu
Rai kutoka kila siku, alisema kuwa awali Kampuni ya New Habari iliwahi
kuomba kwa maandishi kwamba gazeti la Rai litoke kila siku ambapo naibu
msajili wa magazeti licha ya kukiri kulikuwa na tatizo la kiufundi
katika kurejea maombi hayo, alisisitiza kuwa hakuna kinachozuia gazeti
hilo kutoka kila siku.
"Niliruhusu
Mwananchi na Rai kuendelea na mambo yote niliyoyaeleza baada ya
kuridhika kwamba hakukuwa na ukiukwaji wa sheria yoyote uliofanywa na
waombaji," alisisitiza.Alisema ameamua kuweka sawa jambo hilo kutokana
na taarifa ya Idara ya Habari Maelezo kutolewa bila kuwepo kwa
mawasiliano kati yake na waziri, naibu waziri wa wizara hiyo pamoja na
naibu msajili wa magazeti.
"Ndiyo
maana kuanzia Oktoba 10 mwaka huu, gazeti la Rai lilianza kuchapwa kila
siku na kusambazwa, gazeti la Mwananchi likaanza kuwa mtandaoni kwa
kuzingatia maelekezo ya naibu msajili wa magazeti," alisema.
Ziafutazo ni taarifa mbili zinazokinzana za serikali;-
TAARIFA YA NAIBU WAZIRI WA HABARI, VIJANA, UTAMADUNI NA MICHEZO, MH. AMOS MAKALLA KWA VYOMBO VYA HABARI
Napenda
kuufahamisha umma kwamba mimi ndiye NILIYERUHUSU Gazeti la Mwananchi
kuendelea na utoaji wa taarifa/habari kwenye tovuti yake, pia Gazeti la
Rai kutoka kila siku.
Ninalazimika
kutoa ufafanuzi kwa njia ya maandishi kutokana na kupigiwa simu nyingi
na waandishi wa habari kuhusiana na tamko jipya la Mkurugenzi wa Habari –
Maelezo, Ndg xxxxxxxxx kuhoji uhalali wa Gazeti la Mwananchi kuwa
online na Gazeti la Rai kutoka kila siku, badala ya mara moja kwa wiki
(Alhamisi).
Tarehe
4/10/2013 nilifanya mazungumzo na viongozi wa Kampuni ya Mwananchi
Communication Ltd (MCL) na New Habari Corporation (2006) Ltd kwa upande
mmoja na msajili wa magazeti kwa upande mwingine.
Katika kikao hicho cha pamoja na viongozi wa Magazeti ya Mwananchi na Mtanzania maombi matatu yaliwasilishwa;
1. Ombi
la kumuomba waziri apitie upya adhabu iliyotolewa kwa mageazeti hayo.
Katika hili Majibu yangu niliwaambia kwamba mwenye mamlaka juu ya suala
hilo ni waziri mwenye dhamana na masuala ya habari pekee.
2. Ombi la Gazeti la Mwananchi kuwa online na Gazeti la Rai kutoka kila siku badala ya kutoka siku ya Alhamis.
2.1 New
Habari walieleza kuwa siku zilizopita waliwahi kuomba kwa maandishi
(barua) kwamba gazeti la Rai litoke kila siku. Maelezo ya Naibu Msajili
wa Magazeti katika kikao hicho yalikuwa kwamba, kulikuwa na tatizo la
kiufundi katika kurejea maombi hayo na akakiri kuwa hakuna kinachozuia
gazeti la Rai kutoka kila siku. Kutokana na maelezo hayo mimi niliridhia
gazeti hilo sasa liruhusiwe kutoka kila siku.
2.2
Kuhusu gazeti la Mwananchi kuwa online, Naibu Msajili alisema hakuna
sheria yeyote inayoweza kuzuia gazeti hilo kuwa onlineila aliwataka
lisionekane gazeti zima kama lilivyo pia wabadili nembo (Master Head)
kwamba waweke nembo ya MCL na siyo ya gazeti husika ambalo limefungiwa.
Pia baada ya maelezo hayo niliridhia gazeti hilo liwe mtandaoni kwa
kuzingatia angalizo lililotolewa na Naibu Msajili wa Magazeti.
3. Hoja
ya tatu ilikuwa ni ile ya Serikali kupitia Idara ya Habari - Maelezo
kuwa na uhusiano mzuri na vyombo vya habari, ili kuepuka misuguano isiyo
ya lazima.
3.1
Pendekezo hili nililipokea na niliwasilisha kwa Mhe Waziri wa Habari kwa
hatua zaidi, likiwamo suala la kupitia upya adhabu na ushauri wa
kujenga uhisiano na vyombo vya habari.
3.2
Masuala ya Gazeti la Mwananchi kuwa online na Rai kutoka kila siku,
NILILITOLEA UAMUZI siku hiyo hiyo, na uamuzi ni kwamba niliwaruhusu
baada ya kuridhika kwamba hakukuwa na ukiukwaji wa sheria yoyote
uliofanywa na waombaji.
Nimeamua
kuweka sawa jambo hili kutokana na taarifa ya Mkurugenzi wa Maelezo
ambayo ninaamini kwamba kutolewa na kusambazwa kwake ni kukosekana kwa
mawasiliano kati yake kwa upande mmoja na Mhe. Waziri, Naibu waziri na
Naibu Msajili wa Magazeti kwa upande mwingine.
Hivyo
aliyeruhusu Gazeti la Mwananchi kuwa online na Rai ni mimi na ndiyo
maana kuanzia tarehe 5/10/2013 Gazeti la Rai lilianza kuchapwa kila siku
na kusambazwa, na Gazeti la Mwananchi likaanza kuwa mtandaoni kwa
kuzingatia maelekezo ya Naibu Msajili wa Magazeti.
Imetolewa na:
Amos G. Makalla
Naibu Waziri wa Habari,Vijana, Utamaduni na
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
MichezoIdara
ya Habari – MAELEZO, inapenda kuufahamisha umma wa Watanzania kwamba
Mheshimiwa xxxxxxxx Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo
amepokea maombi kutoka kwa wamiliki wa Magazeti ya Mwananchi na
Mtanzania wakiomba kupunguziwa adhabu au kusamehewa adhabu
wanazozitumikia kuanzia 27 Septemba, 2013.
Wakati
Mheshiwa Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo anatafakari
maombi hayo, amesikitishwa kuona kwamba magazeti haya mawili yamekiuka
masharti ya adhabu walizopewa.
Wamiliki
wa Gazeti la Mtanzania baada ya kufungiwa wameamua kuligeuza gazeti la
kila wiki la RAI kuwa la kila siku bila ya kibali cha Msajili wa
Magazeti. Kwa mujibu wa ratiba ,gazeti la RAI linapaswa kutoka kila siku
ya Alhamisi.
Wamiliki wa gazeti la Mwananchi nao wameendelea kuchapisha gazeti hilo katika mtandao kinyume na agizo la kufungiwa.
Serikali
inawataka wamiliki wa vyombo habari nchini kuwa na utamaduni wa kutii
sheria za vyombo vya habari zinazotumika wakati huu. Hivyo serikali kwa
mara nyingine tena inawataka wamiliki wa Gazeti la MTANZANIA, kuzingatia
ratiba yao ya kutoa gazeti lao kila siku ya ALHAMISI.
Aidha,
serikali inawataka wamiliki wa Gazeti la Mwananchi kuacha mara moja
kuchapisha gazeti lao katika mtandao kama amri ya kufungiwa
ilivyoanisha.
Imetolewa na,
Idara ya Habari – MAELEZO
10 Oktoba, 2013
11 Oktoba 2013: CHANZO MWANANCHI.
No comments:
Post a Comment