Kocha Hans van Pluijm akiwasili kwenye uwanja wa ndege wa kimatafa wa Julius Nyerere Dar es Salaam juzi.
UONGOZI wa Klabu ya soka ya Yanga jana asubuhi ulilazimika kumwondoa
mazoezini Kocha Mkuu, Marcio Maximo na kumrudisha klabuni ili kumalizana
naye kabla ya kuanza safari ya kurudi kwao Brazil, huku akiiacha timu
hiyo ikifundishwa na kocha anayetarajiwa kuchukua nafasi yake, Hans van
Pluijm.
Maximo aliondolewa mazoezini na kupakiwa kwenye basi dogo la timu
hiyo aina ya Toyota Hiace lililokuwa likiendeshwa na meneja wa timu
hiyo, Hafidh Salehe.
Aliambana na msaidizi wake, Leonard Neiva na kiungo Emerson de
Oliveira Roque aliyesajiliwa hivi karibuni akitokea nchini Brazil.
Kitendo hicho kilitokana na uongozi huo kufikia makubaliano ya
kumtimua kazi kocha huyo pamoja na msaidizi wake Neiva, kutokana na
kushindwa kuipa mafanikio tangu alipoanza kuifundisha timu hiyo katika
kipindi cha miezi minne.
Kibarua chake kiliingia katika majaribu makubwa baada ya kufungwa
mabao 2-0 na Simba katika pambano la Nani Mtani Jembe 2 mwishoni mwa
wiki kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam; matokeo yaliyosababisha
afukuzwe.
Gazeti hili lilifika kwenye Uwanja wa Shule ya Sekondari ya Loyola
ambako Yanga wanafanyia mazoezi na kumkuta Maximo, Neiva na Emerson
wakiwa ndani ya gari huku wengine wakiendelea na mazoezi na kumuuliza
nini tatizo.
“Siwezi kuzungumzia chochote kwa sasa kwa sababu hata mimi sielewi
tatizo ni nini, lakini ngoja tufike klabuni na baada ya mazungumzo na
uongozi, nitajua cha kuzungumza na waandishi,” alisema Maximo akiwa
ndani ya Hiace.
Baada ya gari hilo kuondoka Loyola, wachezaji wa Yanga waliendelea na
mazoezi kama kawaida wakiwa chini ya kocha Pluijm aliyekuwa anasaidiana
na makocha wazawa wakiwamo Juma Pondamali na Salvatory Edward.
Kwa upande wake, Pluijm aliyewasili nchini usiku wa kuamkia jana,
alikataa kuzungumza kwa sababu hajasaini mkataba, lakini ana matumaini
makubwa ya kufikia makubaliano baada ya kuzungumza na viongozi wa Yanga.
Taarifa ndani ya Yanga zinadai Maximo na wenzake wanatarajia kukutana
na uongozi ili kumalizana kwa kulipwa haki zao ili waondoke huku Andrey
Coutinho akiendelea kubaki kuitumikia timu hiyo kutokana na kuwa na
mkataba mrefu.
Uongozi umedai Maximo alishindwa kuiongoza timu hiyo kumudu ushindani
kwani licha ya kuwa nafasi nzuri katika Ligi Kuu Tanzania Bara, lakini
imeshindwa kupata ushindi inapokutana na timu kubwa kama Simba na Mtibwa
Sugar.
Maximo ameiongoza Yanga kushinda mechi tano za kimashindano kati ya
nane ilizocheza timu hiyo inayoundwa na nyota wengi kutoka ukanda wa
Afrika Mashariki na Kati na wengine kutoka Amerika Kusini.
Kwa mujibu wa taarifa ndani ya Yanga, Pluijm atapewa mikoba ya
Jangwani akisaidiana na Charles Boniface Mkwasa ambaye kwa pamoja
waliiongoza timu hiyo kwa takribani miezi mitano, kabla ya kuondoka
wenyewe kwenda kufundisha soka ya kulipwa katika Klabu ya Al Shoalah ya
Saudi Arabia.
Na Habari Leo
No comments:
Post a Comment