MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa
Assad (pichani) aliyeapishwa juzi na Rais Jakaya Kikwete amekemea tabia
ya wanasiasa na wafanyabiashara kuingilia kazi za kitaaluma, akisema kwa
upande wake hatapenda kuona watu wa makundi hayo wakifanya hivyo na
kusisitiza kuwa, kufanya hivyo ni kosa.
Aliyasema hayo jana mbele ya waandishi wa habari mara baada ya
ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa kila mwaka wa Wahasibu na Wakaguzi (NBAA)
kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Arusha (AICC), jijini hapa.
Alisema ofisi ya CAG na watendaji wengine watafanya kazi kwa kufuata
maadili ya kazi, huku akiendelea kusisitiza wanasiasa na wafanyabishara
kila mmoja aheshimu taaluma ya ukaguzi wa hesabu za serikali kwa faida
ya nchi.
Alifafanua kuwa iwapo kila mmoja atawajibika katika nafasi yake na
kuaminiana katika shughuli za kila siku, kamwe hakutakuwa na matatizo
yoyote.
‘’Matatizo ya watu binafsi yasichanganywe na shughuli za kila siku za
ofisi ya CAG na wale wenye kufanya siasa na biashara pia wawajibike
katika nafasi zao na ofisi yangu itafanya mambo kwa kufuata Katiba ya
nchi inavyoelekeza, na sio vinginevyo,” alisema Profesa Assad
aliyekabidhiwa mikoba ya Ludovick Utouh aliyestaafu kwa mujibu wa
sheria.
Alitumia fursa hiyo kuwaasa wahasibu na wakaguzi, akisema wanatakiwa
kufanya kazi kwa weledi mkubwa na kiwango cha hali ya juu ili taaluma
yao iweze kuheshimika nchini. Asante
kwa kutembelea blog hii na endelea kuwa nasi siku zote, ukitaka kuwa wa kwanza
kupata habari zetu Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya
neno Jambo Tz
Assad alisema kila mtaalamu wa fani hiyo anapaswa kujifunza mambo
mapya, kwani kila kukicha teknolojia inakuwa hivyo nao wanapaswa kwenda
na wakati.
Awali akifungua Mkutano huo wa NBAA, Naibu Waziri wa Fedha, Adam
Malima aliwataka wataalamu wa uhasibu na ukaguzi kuwa wazalendo wa kweli
kwa kulinda rasilimali za nchi ikiwa ni pamoja na kufuata maadili ya
kazi yao bila kuyumbishwa.
Alisema iwapo hilo litazingatiwa ana uhakika mkubwa uchumi wa nchi
kukua kwani taaluma hiyo ni kiini cha matatizo yote ya ulaji fedha hivyo
wanapaswa kuwajibika kikamilifu.
Alisema baadhi wa wataalamu wa fani hiyo wanafanya kazi nzuri sana
lakini wengine hawafanyi vizuri hivyo kila mmoja wao ajue kuwa fani hiyo
ni muhimu kwa nchi na inafika wakati wa kupaswa kukemeana kwa
wanaukiuka maadili yao.
‘’Fahari ya kazi hii ni kufanya kazi kwa kufuata maadili na si
vinginevyo na nyie ni lazima mjione kuwa ni watu muhimu sana kwa maslahi
ya nchi,’’ alisema. Naye Mwenyekiti wa Bodi ya NBAA, Isaya Jairo
aliwataka wataalamu hao kufanya kazi katika viwango vya kimataifa kwa
maslahi ya nchi.
Jairo alibainisha kwamba sasa Bodi hiyo itawaleta wataalamu kutoka
nje kwa ajili ya mafunzo ya kazi katika sekta ya gesi na madini ili
waweze kufanya shughuli hiyo kwa weledi mkubwa. Asante
kwa kutembelea blog hii na endelea kuwa nasi siku zote, ukitaka kuwa wa kwanza
kupata habari zetu Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya
neno Jambo Tz
No comments:
Post a Comment