Jana tulichapisha habari za kusikitisha kutoka
wilayani Urambo, mkoani Tabora kuhusu Pendo Sengerema, msichana wa miaka
15 mwenye ulemavu wa ngozi (albino), ambaye watu wenye imani za
kishirikina wamemkata mkono wa kulia na kuondoka nao.
Huu ni uthibitisho kwamba Watanzania wenzetu wenye
ulemavu wa ngozi wanaendelea kupoteza maisha au kupata vilema vya
kudumu kutokana na sehemu ya jamii yetu kukumbwa na imani potofu za
kishirikina kwamba viungo vya watu hao vinaleta utajiri mkubwa na wa
haraka.
Hatuna maneno stahiki ya kuelezea tukio hilo, isipokuwa tu kusema kwamba linasikitisha na kufadhaisha.
Kama msichana mdogo hivyo anaweza kufanyiwa
ukatili wa kiwango kikubwa kiasi cha kupoteza kiungo muhimu kama mkono,
ambao ungekuwa tegemeo kubwa kwake katika kufanya shughuli za kumwezesha
kujitegemea kimaisha, basi tukubaliane kwamba ushirikina umeigeuza
jamii yetu kuwa sawa na jamii ya wanyamapori.
Ni imani hizo potofu ambazo zimeikumba jamii yetu
tangu mwaka 2000 wakati nchi yetu ilipoanza kushuhudia mauaji ya kinyama
dhidi ya ndugu zetu hao wenye ulemavu wa ngozi.
Miaka 14 imepita sasa na vitendo hivyo
vinaendelea. Bahati mbaya Serikali imeshindwa kuonyesha dhamira ya
kutokomeza uovu huo, bali imebakia kutoa machozi ya mamba. Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya neno Jambo Tz
Tulitarajia Serikali na Bunge viweke mkakati wa
kupambana na watu wanaofanya uovu huo, angalau kwa kutunga sheria kali
dhidi yao na kuwatia mbaroni waganga wanaoendelea kuchochea vitendo
hivyo. Kesi nyingi za watuhumiwa wa vitendo hivyo zinasuasua mahakamani,
huku Serikali ikifumbia macho waganga wa kienyeji wanaopiga ramli.
Mfano ni wale wanaopiga ramli eti kuwawezesha watu
kupata utajiri, mvuto, vyeo, kufuta kesi mahakamani, kurudisha wapenzi,
kutibu ukimwi, kupata madaraka na kadhalika. Serikali inashindwaje
kuwabaini wakati wanaweka wazi anwani na namba zao za simu katika
matangazo wanayobandika barabarani na mitaani?
Jambo la ajabu ni kwamba Serikali inaendelea
kuikumbatia sheria dhaifu ya mwaka 1928. Hatuelewi sababu zinazoifanya
Serikali kushindwa kupitia upya Sheria ya Tiba Mbadala pamoja na
taratibu za usajili wa waganga wa kienyeji. Hii ni pamoja na udhibiti wa
shughuli zao kwa kuhakikisha wapiga ramli wanafutiwa leseni zao.
Tumesema yote hayo kuonyesha udhaifu wa Serikali
katika kusimamia na kuratibu vita dhidi ya mauaji ya albino. Sisi
tunadhani tumerudi nyuma kama taifa katika vita ya kukomesha unyama huo.
Kwa mfano, utafiti uliofanywa katika baadhi ya mikoa, ikiwamo Rukwa na
Tabora umebaini kwamba waathirika wa unyama huo sasa wanakatwa mikono.
Kwa muhtasari tu, tangu mwaka 2000 yamefanyika
mashambulizi zaidi ya 153 ambapo watu 76 wamepoteza maisha. Kati ya watu
34 walionusurika, wengi wao walikatwa viungo au kuumizwa vibaya, huku
makaburi 15 yakifukuliwa na viungo vya watu hao kuibwa. Ni majaribio
manne tu ya kufukua makaburi ndiyo yaliyoshindwa.
Serikali inastahili lawama kwa kuendelea kuwapo
kwa hali hiyo. Inakuwaje zaidi ya nusu ya waganga wa kienyeji bado
hawajasajiliwa? Na inakuwaje wanaachwa waendeshe shughuli zao kwa
kuegemea uchawi na ushirikina? Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya neno Jambo Tz
Je, waganga wa kienyeji hawana maadili au miiko inayosimamia kazi zao? Tunasubiri sasa kuona jinsi Serikali ilivyoguswa na kukatwa mkono kwa msichana Pendo Sengerema ambaye amelazwa katika Hospitali ya Urambo, mkoani Tabora.
Na Mwananchi
Je, waganga wa kienyeji hawana maadili au miiko inayosimamia kazi zao? Tunasubiri sasa kuona jinsi Serikali ilivyoguswa na kukatwa mkono kwa msichana Pendo Sengerema ambaye amelazwa katika Hospitali ya Urambo, mkoani Tabora.
Na Mwananchi
No comments:
Post a Comment