Dodoma. Mjumbe wa Bunge la Katiba, kutoka Kundi
la 201, Thomas Mgoli amelazwa katika Hospitali ya Dodoma baada ya
kupigwa na watu aliodai kuwa ni wafuasi wa Chadema.
Mjumbe huyo alidai kuwa kati ya watu waliompiga
yumo mtumishi wa Bunge na ameshamshtaki kwa Mwenyekiti wa Bunge Maalumu,
Samuel Sitta huku akisema akimuona anaweza kumtambua.
Mgoli ambaye anatokea Chama cha Alliance
Democratic Change (ADC), alisema kuwa alipokea kipigo kikubwa juzi
katika maeneo ya Area A karibu na Shule ya Msingi Chamwino A.
Akiwa katika wodi ya daraja la kwanza hospitalini
hapo, alieleza kuwa chanzo cha mapigano hayo ni mabishano waliyokuwa
nayo na vijana wanne mmoja aliyemtaja kwa jina la Vampaya. Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya neno Jambo Tz
“Nimepanga nyumba katika eneo hilo, juzi (jana)
saa mbili usiku nilitoka kwenda grocery (duka la vinywaji) kuchukua
kinywaji ili nirudi nyumbani. Niliwakuta vijana hao ambao wakati wote
tumekuwa tukitaniana,” alisema na kuongeza:
“Mara baada ya kufika wakaniuliza katika mchango
wangu bungeni ni kwa nini nilimtukana Profesa Kabudi (Palamagamba),
nikajaribu kueleza kilichotokea bungeni na kuhusu mchango wangu, basi
wakaanza kunipiga ngumi nilipotaka kukimbia nikapigwa na kipande cha
tofali.”
Mjumbe huyo alidai kuwa ni kawaida kukutana na vijana hao katika duka hilo na kupata vinywaji huku wakitaniana.
Sitta alifika hospitalini hapo kumjulia hali na alielezwa mkasa mzima.
Baadaye Sitta aliwaonya wajumbe wa Bunge lake kuwa
mijadala ya Katiba inapaswa kufanyika ndani ya Bunge na siyo nje huku
akiwasihi Watanzania kuwa wavumilivu ili Katiba bora ipatikane.
Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk Mzee Nasoro
alisema hali ya mgonjwa huyo inaendelea vizuri na kwamba alikuwa na
maumivu ya juu katika maeneo ya usoni na mdomoni.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, David Misime,
alisema tukio lilitokea wakati mjumbe huyo alipokuwa akipata kinywaji
katika duka hilo ndipo kukatokea mabishano yaliyosababisha kupigwa
kwake.
Alisema polisi wanaendelea kuwahoji watu watatu ili kupata ukweli wa jambo hilo. Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya neno Jambo Tz
No comments:
Post a Comment