KUFUNGIWA MAGAZETI - WAHAFIDHINA SASA WANAONGOZA
Zitto Kabwe, Mb
Kwa
mshtuko na masikitiko makubwa kuanzia jana jioni tumepokea taarifa za
kufungiwa kwa magazeti mawili ya kila siku hapa nchini ya Mwananchi na
Mtanzania. Serikali imechukua uamuzi huo kwa kutumia sheria ya kidikteta
ya magazeti ya mwaka 1976 ambayo Tume ya Jaji Francis Nyalali
iliiorodhesha kama sheria kandamizi. Sababu zilizotolewa kuhalalisha
uamuzi huu ni sababu zisizo na maana na ambazo Serikali ingeweza
kufungua mashtaka ya kawaida kabisa mahakamani kushtaki magazeti hayo
iwapo haikupendezwa na habari walizochapisha.
Moja
ya sababu ya kufungiwa kwa gazeti la Mwananchi ni kuchapisha taarifa
kuhusu mishahara ya Serikali. Serikali inasema habari hii ni siri.
Serikali hii hii ambayo imesaini makubaliano ya kuendesha serikali kwa
uwazi (Open Government Initiative) na kumwagiwa sifa na Rais Barack
Obama wa Marekani inalifungia gazeti kwa kuandika habari za mishahara ya
watumishi wa Serikali. Mishahara kuanzia mshahara wa Rais mpaka wa
mtendaji wa Kijiji haipaswi kuwa jambo la siri.
Kuonyesha
kuwa jambo hili linapaswa kuwa wazi mkutano ujao wa Bunge tutatafuta
kila namna kutaja mshahara wa Rais, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu na
baadhi ya Watendaji wa Mashirika makubwa ya Umma kama njia ya kuwaunga
mkono gazeti la Mwananchi kwa habari yao hiyo. Mapato ya Mbunge
yanajulikana sasa kuwa ni shilingi milioni 11.2 kwa mwezi kabla ya
kuongeza posho za vikao za shilingi laki 200,000 kwa siku na posho ya
kujikimu ya shilingi 130,000 kwa siku. Watanzania wana haki ya kujua
wanawalipa kiasi gani watumishi wao. Tutaanza na mshahara wa Rais!
Gazeti
la Mtanzania limefungiwa pamoja na mambo mengine kwa kuandika
'mapinduzi ni lazima'. Inashangaza Serikali ya Chama cha Mapinduzi
inaogopa neno mapinduzi. Marehemu Mzee Steven Salum Nandonde, aliyekuwa
mbunge wa Jimbo la Tandahimba alipata kusema bungeni kuwa 'lazima nchi
ipinduliwe'. Ni matumizi ya lugha tu. Mzee Nandonde yeye alikuwa
analalamikia maendeleo duni ya mikoa ya kusini na kutaka Kaskazini iwe
Kusini na Kusini iwe Kaskazini. Serikali inafungia gazeti kwa sababu ya
kuandika Mapinduzi ni lazima ilhali kila siku Zanzibar wanasema
Mapinduzi daima!
Gazeti
la Mtanzania linahaririwa na Absalom Kibanda, mwandishi wa habari
ambaye bado anaponya majeraha ya mwili na kisaikolojia ya kuteswa na
watu ambao mpaka leo hawajakamatwa. Badala ya Serikali kuwakamata
watesaji wa Kibanda, inamnyima kazi Kibanda ili ateseke kwa njaa kwa
kukaa miezi mitatu bila kazi. Pia wanatutesa Watanzania kwa njaa ya
kupata habari ambayo ni haki ya msingi ya kikatiba. Hii ndio zawadi
Serikali inampa Kibanda baada ya kung'olewa kucha, kunyofolewa jicho,
kukatwa vidole na kuteswa kwa namna isiyoelezeka.
Matukio
ya hivi karibuni na namna Serikali inavyoyachukulia yanaonyesha dhahiri
kwamba Rais Kikwete kazidiwa nguvu na kundi la wahafidhina ndani ya
chama na Serikali yake. Rais ambaye alianza kwa kuhubiri uvumilivu wa
hali ya juu na hata yeye mwenyewe kupata kusema uvumilivu huu wengine
wanauona kama udhaifu lakini ameamua kujenga Taifa la kuvumiliana. Rais
alipata kulalamika hadharani kwamba kuna wenzake wanataka aongeze ukali.
Ni dhahiri kundi hili la wahafidhina sasa ndio linalomwongoza Rais
Jakaya Kikwete. Kitu kimoja tu Rais azingatie, kundi hili linaongozwa na
maslahi binafsi ya kubakia kwenye utawala wakati yeye anapaswa kuacha
'legacy'.
Rais
Kikwete asipokuwa makini atakuwa Rais karatasi (lame duck) tu
tunapoelekea mwisho wa utawala wake. Maamuzi ya hovyo na ya kidikteta ya
kufungia magazeti yanamchora vibaya mbele ya wananchi na jamii ya
kimataifa. Wahafidhina kuwa nguvu zaidi ya kiutawala ni makosa ambayo
watanzania hawapaswi kuyakubali kamwe.
Wananchi
sasa waifanye Serikali kujutia uamuzi wake wa kufungia magazeti.
Nimeamua mimi binafsi kama mbunge kesho Jumatatu tarehe 30 Septemba,
2013 kupeleka taarifa rasmi kwa Katibu wa Bunge ya kupeleka muswada
Bungeni wa kuifuta kabisa Sheria kandamizi ya magazeti ya mwaka 1976.
Sasa tupambane na kundi dogo la wahafidhina ndani ya Serikali na CCM
wasiopenda mabadiliko na iwe fundisho kwa wahafidhina wengine wowote
waliopo ndani ya Serikali au nje ya Serikali kwamba Uhuru wa habari sio
jambo la kuchezea kama golori.
No comments:
Post a Comment