Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa mwenendo wa Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC) kuhusu Bara la Afrika na viongozi wake, unainyima Mahakama hiyo nafasi kubwa ya kuungwa mkono na Bara la Afrika.
Rais Kikwete pia amelaani vikali mashambulizi yanayoongezeka dhidi ya vikosi vya kimataifa vya kulinda amani katika nchi mbali mbali duniani wakiwamo walinda amani wa Tanzania.
Rais Kikwete alitoa msimamo huo wa Tanzania mwishoni mwa wiki wakati alipohutubia Kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa
Mataifa (UNGA) mwaka huu, kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, Marekani.
Katika hotuba yake fupi na
iliyowavutia wasikilizaji, Rais Kikwete alisema kuwa ni dhahiri
kuanzishwa kwa ICC kutokana na Mkataba wa Rome kulikuwa ni hatua muhimu
sana katika mfumo wa kimataifa wa kupambana na makosa ya jinai.
"Kwa hakika kuundwa kwa Mahakama hiyo
kuliweka mfumo mzuri wa kuondokana na watu kutenda vitendo vya jinai na
kuweza kuepukana na kuwajibika kwa vitendo hivyo na Mahakama hiyo
ilianzishwa kwa kuungwa mkono kwa kiasi kikubwa na Afrika.
"Hata hivyo, muongo mmoja tu baada ya
kuanzishwa kwa Mahakama hiyo, ni dhahiri kuwa mvutano umezuka kati ya
ICC na Bara la Afrika. Sasa Mahakama hiyo inaonekana kama taasisi
isiyojali maoni na msimamo wa Afrika, kwa mambo ambayo kwa maoni yangu,
ni hofu halali ya Waafrika," amesema Rais Kikwete na kuongeza:
"Bado Mahakama hiyo inaendelea kupuuza
maombi ya mara kwa mara ya Umoja wa Afrika. Ni jambo la kutia huzuni
kuwa maombi ya kubadilisha muda wa kuanza kusikilizwa kwa kesi dhidi ya
Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya na Naibu Rais William Ruto yalipuuzwa na
hata hayakujibiwa kabisa."
Ameongeza Rais: "Tabia hii imekuwa ni
hitilafu kubwa ambayo inaleta kikwazo kwa ICC kushindwa kutimiza wajibu
wake wa kupambana na tabia ya watu wanaofanya makosa ya jinai
kutokuchukuliwa hatua. Kwa hakika, kugangamara kwa ICC hata katika
masuala yaliyo wazi, kumethibitika kuwa kunainyima Mahakama hiyo nafasi
ya kuendelea kuungwa mkono Barani Afrika."
Rais Kikwete alisema pia kuwa Tanzania
sasa imekuwa moja ya nchi ambazo zinashiriki zaidi katika shughuli za
kimataifa za kulinda amani chini ya Umoja wa Mataifa. Tanzania ina zaidi
ya walinda amani 2,500 katika Darfur, Sudan; Lebanon na Jamhuri ya
Kidemokrasi ya Congo (DRC) na kuwa ni nchi ya sita katika Afrika na ya
12 duniani kwa kutoa walinzi wa amani duniani.
"Kwa hakika tunaridhishwa na mchango
wetu mdogo katika shughuli hii. Na tunajua kuwa wakati mwingine tunalipa
gharama kubwa na maisha ya vijana wetu kwenye shughuli hizi kama
ilivyotokea majuzi katika Darfur na DRC. Waliopoteza maisha yao ni
mashujaa wa taifa letu ambao maisha yao hayakupotea bure."
Aliongeza Rais Kikwete: "Vifo vya
walinda amani wetu ni ukumbusho wa kutosha wa hatari zinazowakabili
walinda amani wote duniani. Ni jambo la kuudhi, kwamba vikundi vyenye
silaha na waharibifu wa amani duniani wanaongeza mashambulizi hayo dhidi
ya watumishi wa amani. Ni lazima tulaani mashambulizi haya kwa nguvu
zetu zote kwa sababu hakuna sababu yoyote ya kuhalalisha mashambulizi
haya ya kinyama ambayo ni kosa la kimataifa la jinai chini ya Sheria za
Kimataifa."
Alisisitiza: "Baraza la Usalama la
Umoja wa Mataifa ambalo wajibu wake mkuu ni kulinda amani na usalama wa
kimataifa lazima liwe mstari wa mbele katika kulaani vitendo hivyo vya
kinyama na haraka tu vinapotokea."
Rais Kikwete ambaye alikuwa katika
ziara ya kikazi katika Marekani na Canada ameondoka New York usiku wa
leo, Jumamosi, Septemba 28, 2013, kurejea nyumbani ambako atawasili
Jumatatu mchana.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
No comments:
Post a Comment