Serikali imeyafungia kutochapishwa
Magazeti ya MWANANCHI na MTANZANIA kuanzia 27 Septemba, 2013 kutokana na
mwenendo wa magazeti hayo kuandika habari na makala za uchochezi na
uhasama kwa nia ya kusababisha wananchi wakose imani kwa vyombo vya dola
hivyo kuhatarisha amani na mshikamano ulipo nchini.
Gazeti la MWANANCHI limefungiwa
kutochapishwa kwa siku kumi na nne (14) kuanzia 27 Septemba, 2013.
Adhabu hii imetangazwa kwa Tangazo la Serikali (Government Notice) Namba
333 la tarehe 27 Septemba, 2013.
Gazeti la MWANANCHI limepewa adhabu hiyo kutokana na hivi karibuni kuchapisha habari zenye mwelekeo wa
uchochezi na uvunjifu wa amani, mfano
tarehe 17 Julai, 2013 katika toleo Namba 4774 ilichapisha habari isemayo
"MISHAHARA MIPYA SERIKALINI 2013" kwa kuchapisha waraka uliozuiliwa kwa
matumizi ya vyombo vya habari waraka huo ulikuwa wa Siri haukupaswa
kuchapishwa Magazetini.
Aidha, katika toleo la Jumamosi,
tarehe 17 Agosti, 2013 lilichapisha habari yenye kichwa kisemacho
"WAISLAM WASALI CHINI YA ULINZI MKALI" habari hiyo ilikolezwe na picha
ya mbwa mkali mwenye hasira.
Habari na picha hiyo ilitoa tafsiri ya
kuwa Jeshi la Polisi lilipeleka mbwa katika maeneo ya ibada ya waumini
wa dini ya Kiislam. Jambo ambalo halikuwa la ukweli.
Jeshi la Polisi katika doria siku hiyo
halikupeleka mbwa katika maeneo ya Misikiti. Serikali na jeshi la
Polisi linaheshimu na kuzingatia maadili ya dini ya Kiislamu na kwa hiyo
Jeshi lake hakiwezi kupitisaha au kuingiza mbwa katika maeneo ya ibada.
Hivyo basi, kwa gazeti hili kuchapisha
habari iliyokolezwa na picha ya mbwa ni uchochezi wa kulichonganisha
Jeshi la Polisi na waumini wa dini ya kiislam mbwa ni najisi hapaswi
kuingia katika maeneo ya ibada.
Gazeti la MTANZANIA limefungiwa
kutochapishwa kwa siku tisini (90) kuanzia tarehe 27 Septemba, 2013 kwa
kuchapisha habari zenye uchochezi.
Gazeti hili limeonywa mara nyingi
lirekebishe mtindo wake wa uandishi wa kichochezi na lizingatie maadili
na Sheria na Kanuni za fani ya Habari.
Pamoja na kuonywa gazeti hili
halikuonyesha kuzingatia maelekezo ya Msajili wa Magazeti, mfano ;katika
toleo na 7262 la 20 Machi, 2013 liliandika habari yenye kichwa
kisemacho "URAIS WA DAMU", tarehe 12 Juni, 2013, toleo Namba 7344
lilichapisha makala isemayo "MAPINDUZI HAYAEPUKIKI".
Aidha, siku ya Jumatano, tarehe 18
Septemba, 2013 katika toleo Namba 73414 ukurasa wa mbele lilichapisha
Kichwa cha habari kisemacho "SERIKALI YANUKA DAMU" taarifa hiyo
ilikolezwa na picha zilizo unganishwa kwa ustadi mkubwa kwa kutumia
kompyuta kutapakaza rangi nyekundu mithili ya damu nyingi kumwagika.
Katika habari hiyo gazeti hilo limedai
bila uthibitisho kuwa Jeshi la Polisi linahusika na wahanga waliomizwa
na watu wasiojulikana kwa kumwagiwa tindikali na waliyovamiwa na
kujeruhiwa vibaya.
Vile vile gazeti hilo limeishtumu serikali kuwa goigoi katika kushughulikia matukio yenye sura ya kigaidi.
Kwa ujumla wake habari hiyo ni ya
kichochezi ina lengo la kuwafanya wananchi wavichukie vyombo vya ulinzi
na usalama wavione kuwa haviwasaidii.
Kutokana na makosa yalitajwa hapo juu
serikali imelifungia gazeti la Mtanzania kutochapishwa kwa muda wa siku
tisini(90) kwa Tangazo la Serikali Namba 332 (Government Notice No.332)
la tarehe 27 Septemba, 2013,.
Serikali inawataka wamiliki,wahariri
na wanahabari kwa ujumla kuwa makini, kuzingatia weledi, miiko na madili
yataaluma uandishi wa habari.
Serikali inawataka wamiliki na hasa
wahariri kuhakisha kuwa habari wanazoziandika na vipindi wanavyoviandaa
vinazingatia taaluma, kuweka mbele maslahi ya taifa letu kwa kuwa na
uzalendo wa hali ya juu.
Serikali inavionya vyombo vya habari
vinavyoutumia uhuru wa habari bila wajibu kuwa haitasita kuvichukulia
hatua kali ikiwemo ya kuvifungia. Serikali haitakubali kuona vyombo vya
habari kuwa chanzo cha uvunjifu wa amani nchini.
Imetolewa na
MKURUGENZI IDARA YA HABARI
WIZARA YA HABARI, VIJANA, UTAMADUNI NA MICHEZO
28 SEPTEMBA, 2013
WIZARA YA HABARI, VIJANA, UTAMADUNI NA MICHEZO
28 SEPTEMBA, 2013
Source:
http://www.wavuti.com/4/post/2013/09/tamko-la-serikali-la-kuyafungia-kuchapishwa-magazeti-ya-mwananchi-na-mtanzania.html#ixzz2gFRTtpMz
No comments:
Post a Comment