Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete
leo, Alhamisi, Septemba 5, 2013, amekutana kwa faragha na Rais wa
Rwanda, Mheshimiwa Paul Kagame katika mazungumzo yaliyokwenda vizuri na
kuwaridhisha viongozi hao wawili wa nchi jirani.
Viongozi
hao wamekutana kwa zaidi kidogo ya saa moja katika mkutano uliofanyika
kwenye Hoteli ya Munyonyo Commonwealth Resort, nje kidogo ya mji wa
Kampala, Uganda.
Katika
mazungumzo hayo, Rais Kikwete na Rais Kagame wamekubaliana kuendelea
kushirikiana katika kujenga uhusiano mzuri na wa kihistoria uliopo kati
ya nchi hizo mbili.
Viongozi
hao wawili wako nchini Uganda kuhudhuria Mkutano wa Nchi Wanachama wa
Umoja wa Kimataifa wa Maziwa Makuu – “International Conference on the
Great Lakes Region (ICGLR)” unaofanyika leo Hoteli ya Munyonyo
Commonwealth Resort.
Viongozi
wengine ambao wanahudhuria Mkutano huo ni pamoja na Rais Yoweri
Museveni wa Uganda ambaye ni Mwenyekiti wa ICGLR na mwenyeji wa Mkutano
huo, Rais Silva Kiir wa Sudan Kusini, Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa
Afrika (AU).
Rais
Kikwete na ujumbe wake amewasili Kampala asubuhi ya leo akitokea mjini
Dodoma ambako aliwasili jana jioni kwa ajili ya hafla ya kuwaapisha
Makatibu Wakuu watatu na Naibu Makatibu Wakuuu wawili iliyofanyika Ikulu
Ndogo, Dodoma.
Rais
Kikwete aliwasili Dodoma akitokea Mwanza ambako alihudhuria mazishi ya
Kiongozi Mkuu wa Kanisa la Evangelistic Assemblies of God Tanzania
(EAGT) Askofu Mkuu Dkt. Moses Samwel Kulola yaliyofanyika kwenye Kanisa
la Bugando Calvary Temple, mjini Mwanza.
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
No comments:
Post a Comment