Jana, Bingwa wa Dunia wa uzani wa kati (super middle), unaotambuliwa na Shirikisho la Ngumi Duniani (WBF), Francis Cheka alitembelea Bunge baada ya kutwaa taji hilo karibuni na jana hiyohiyo, Bunge hilo lilishuhudia ngumi kavukavu katika vurugu kubwa pengine kuliko zote zilizowahi kutokea katika ukumbi wake.Katika masumbwi hayo yasiyo rasmi, Mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi 'Sugu' anadaiwa kumpiga kichwa Askari wa Bunge na kumchania sare na kung'oa kipaza sauti.
Mbilinyi jana alisema alikuwa
anatafutwa na polisi huku akisema hilo limemshangaza akidai kwamba yeye
ndiye aliyeshambuliwa na askari huyo.
Vurugu hizo zilitokea baada ya Naibu
Spika, Job Ndugai kuamuru kutolewa nje kwa Kiongozi wa Kambi Rasmi ya
Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe.
Katika vurugu hizo Mbilinyi alibebwa juujuu na polisi hadi nje ya ukumbi huku akiwa hana viatu.
Pamoja na tafrani hiyo, Ndugai alisema
wakati akihitimisha kikao cha Bunge kipindi cha asubuhi kuwa
amewasamehe wabunge wote waliohusika na kosa hilo la utovu wa nidhamu na
kuwaruhusu kurejea kipindi cha jioni kuendelea na Muswada wa
Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba. Hata hivyo, wabunge wote
CUF, NCCR-Mageuzi na Chadema ambao baada ya tukio hilo walitoka nje ya
ukumbi, hawakurejea na baadaye walitoa msimamo wa pamoja wakisema
hawatashiriki katika mjadala huo.
Msimamo huo ulitolewa na Mbowe ambaye
pia ni Mwenyekiti wa Chadema, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia
na Mbunge wa CUF, Habib Mnyaa.
Mbowe alisema wameamua kususia majadiliano hayo kuonyesha msimamo wao wa kupinga kupitisha mambo yasiyo na masilahi kwa nchi.
"Hatuko tayari kushiriki katika
uchakachuaji wa Katiba... Matumizi ya nguvu ya polisi kamwe
hayatatupatia Katiba nzuri," alisema. Alisema kambi rasmi ya upinzani
inalaani vikali kitendo cha Ndugai kuruhusu Bunge kunajisiwa kwa
kuruhusu polisi kuingia ndani kinyume na kanuni.
Mnyaa alisema kitendo cha wadau wa
Zanzibar kutoshirikishwa katika kutoa maoni yao katika muswada huo wa
marekebisho ni dharau kubwa.
Mbatia alisema Tanzania haiwezi
kuingia Uchaguzi Mkuu wa 2015 kwa kutumia Katiba ya sasa kwa sababu
tayari kuna mgongano wa kikatiba kati ya Zanzibar na Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania.
Mnadhimu wa Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni, Tundu Lissu alimtaka Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Kuu, (Sera,
Uratibu na Bunge), William Lukuvi kutoa ushahidi kama Rais aliteua
wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba kulingana na mapendekezo ya
taasisi zao.
Kuanza kwa tafrani
Sakata hilo lilianza saa 6:45 mchana
muda mfupi baada ya kukamilika kwa kura kuamua kama Bunge liahirishwe au
la kutokana na hoja iliyotolewa na Mbunge wa Mkoani (CUF), Ali Hamisi
Seif (CUF). Waliotaka liahirishwe walipata kura 59 na waliokataa 159.
Baada ya Ndugai kutangaza matokeo hayo
na kutaka shughuli za Bunge ziendelee, Mbowe aliposimama na kusema ana
hoja Naibu Spika alimwamuru akae chini.
Baada ya Mbowe kusisitiza ana hoja na
kumwomba Spika amsikilize ndipo Ndugai alipomwamuru atoke nje na
alipokaidi alisema:" Naomba askari wote waliopo katika mazingira haya
(ya Bunge) waingie ndani ya ukumbi wa Bunge".
Baada ya kitambo kifupi, Mbowe akiwa bado amesimama alitoa maagizo atolewe nje: "Kiongozi wa upinzani atolewe nje."
Polisi waliingia ndani ya Ukumbi wa
Bunge lakini Wabunge wa Kambi ya Upinzani kwa umoja wao, walimzinga
Mbowe asifikiwe na askari hao.
Baada ya kuona polisi wanaelekea
kushindwa, Ndugai alitoa maagizo mengine: "Askari hamjaletwa humu ndani
kufanya majadiliano mnatakiwa kuhakikisha kiongozi wa upinzani anatolewa
nje".
Alisema yeye ndiye anayeendesha kikao hicho hivyo lazima Mbowe atolewe nje.
Hapo ndipo wabunge hao wa upinzani
walipoanza kuimba: "Hatutaki kuburuzwa hatutaki kuburuzwa... hatutaki
kuonewa," huku wakiendelea kumzinga Mbowe.
"Askari wote mliopo humu ndani naomba
mnisikilize... Sasa naagiza kwa mara ya mwisho... nasema kiongozi wa
upinzani atolewe nje."
Baada ya kauli hiyo ya Ndugai, ndipo
polisi walipotumia nguvu hasa kwa Mbilinyi na Mbunge wa Maswa Mashariki
(Chadema), Silvester Kasulumbai.
Katika patashika hiyo, inadaiwa kwamba
Mbunge wa Kasulu Mjini (NCCR-Mageuzi), Moses Machali alipigwa ngumi
ambayo ilimfanya apepesuke hadi sakafuni.
Kilichomponza Mbilinyi ni hatua yake ya kusogelea Siwa. Polisi waliokuwa karibu, walimbeba juujuu hadi nje ya ukumbi.
Wakati akitolewa nje ya ukumbi, alijaribu kujizuia kwa kushika kipaza sauti kinachotumiwa na upande wa upinzani hadi kikang'oka.
Mbunge wa Viti Maalumu (CUF), Mozza
Abeid, alivuliwa hijabu katika vurumai hizo wakati polisi walipokuwa
wakitumia nguvu ili kumfikia Mbowe.
Baada ya kuona hali inazidi kuwa
mbaya, Mbowe aliamua kutoka nje huku akisindikizwa na polisi pamoja na
wabunge wa vyama hivyo na alipofika nje ya ukumbi alipokewa na polisi wa
kawaida waliomweka chini ya ulinzi kabla ya kumwachia baada ya ombi la
Mbunge wa Rombo (Chadema), Joseph Selasini.
Kutokana na hali ya mambo kuwa tete,
askari wa Bunge waliwaondoa wageni waliokuwa wamekaa katika kumbi za
wageni wakiwamo wanafunzi wa shule mbalimbali za sekondari huku baadhi
ya wabunge wa CCM waliokuwa na simu za kisasa za mkononi na kompyuta
mpakato (Ipad) wakichukua picha za tukio zima.
Inadaiwa kwamba baada ya kutoka nje ya
ukumbi, Mbilinyi alimtwanga ngumi mmoja wa askari waliomtoa kwa nguvu
kabla ya kuamuliwa na wabunge na polisi.
Wakati wote huo, wafanyakazi wa Bunge
na wageni walionekana wakiwa wamejikusanya katika makundi wakitafakari
na kushangaa yaliyokuwa yakitokea.
Balaa lilivyoanza
Akitumia Kanuni ya 69(1), Mbunge wa
Mkoani (CUF), Ali Hamisi Seif, alitaka kuahirishwa kwa mjadala wa
Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba wa mwaka 2013
kutokana na ukweli kuwa Kamati ya Sheria, Katiba na Utawala ya Bunge
ilipaswa kukusanya maoni ya wadau mbalimbali nchini ikiwamo upande wa
Zanzibar jambo ambalo halikufanyika wakati wa maandalizi ya muswada huo.
"Ilipaswa sheria hii inapotaka
kufanyiwa marekebisho iende tena kulekule Zanzibar lakini jambo la
kusikitisha kamati inayohusika na masuala ya Katiba haikwenda. Mimi ni
mjumbe wa kamati na tuliitwa Dar lakini ratiba waliyotupa haikuonyesha
kama tungekwenda Zanzibar," alisema. Mkosamali naye aliomba mwongozo kwa
Spika, akisema kwa kuzingatia matakwa ya kiapo cha Spika au Naibu
alipaswa kuendesha Bunge kwa haki bila upendeleo.
"Kanuni inasema Spika ama Naibu Spika
ama Mwenyekiti ataendesha shughuli za Bunge kwa haki, uadilifu, bila
chuki wala upendeleo wowote kwa kuongozwa na Katiba ya nchi," alisema na
kuongeza: "Kwa kuwa sisi tumekuweka hapo ili uendeshe Bunge kwa
uadilifu, usiburuzwe na chama chako na uzingatie miongozo yote kwa
wakati. Kwa nini usitumie mamlaka yako kuondoa muswada huu"?
Mbunge wa Peramiho (CCM), Jenister
Mhagama aliomba mwongozo kwamba kwa kuwa bado kuna malalamiko basi waipe
Serikali nafasi ya kuthibitisha kwamba majadiliano ya kamati
yalikamilika.
Lissu katika kuomba mwongozo wake,
alisema Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Sheria, Katiba na Utawala,
Pindi Chana alilidanganya Bunge alipowasilisha maoni ya kamati kwamba
wadau wa muswada huo walishirikishwa jambo ambalo alisema si kweli.
Lissu alisema hakuna Mzanzibari aliyefika mbele ya kamati hiyo kutoa maoni kuhusu muswada wowote.
Hata hivyo, Chana alijibu akisema
wadau wa Zanzibar walitoa maoni yao na kukabidhi nyaraka mbalimbali kwa
Spika kuthibitisha kauli yake hiyo. Alivitaja vyama vya Jahazi Asilia na
ADC kuwa vilihojiwa.
Kwa upande wake, Lukuvi alimshambulia
Lissu kwa kauli yake ya juzi kwamba uteuzi wa Wajumbe wa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba uliofanywa na Rais Jakaya Kikwete ulikuwa na
walakini. "Lissu alisema jana (juzi) kwamba wapo wadau ambao walisema
ijapokuwa waliandikiwa barua ya kuwasilisha majina matatu kila moja ili
Rais ateue mmoja lakini hakuna mjumbe aliyeteuliwa".
Alitaja majina ya walioteuliwa kuwa ni
Maria Kashonda (Tec), Jesca Mkuchu (CCT), Humphrey Polepole (Civil
Society) na Profesa Palamagamba Kabudi (Kundi la Wasomi).
Lukuvi aliwataja wengine
waliopendekezwa na taasisi zao na Rais kuwateua kuwa ni Mwamtumu Malale
(Bakwata) na Dk Sengondo Mvungi (NCCR) na Profesa Mwesiga Baregu wa
Chadema.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG),
Fredrick Werema alisema katika mchakato wa muswada huo, Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar (SMZ) iliwasilisha maoni yake mbele ya kamati.
Alisema Makamu wa Pili wa Rais
Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi aliwasilisha kwa kamati mapendekezo ya
SMZ, Mei mwaka huu na mapendekezo hayo ikiwamo uteuzi wa wajumbe 166
yalizingatiwa.
Waacha muswada, wapiga vijembe
Baada ya kurejea katika kikao cha
Bunge cha jioni jana, wabunge wa CCM waliopewa fursa ya kuchangia
mjadala wa muswada huo walitumia muda mwingi kuwajadili wabunge wa kambi
ya upinzani.
Chanzo:Mwananchi
No comments:
Post a Comment